Pages

KAPIPI TV

Wednesday, June 25, 2014

WAKAZI WA MAGALA WAMKUMBUSHA RAIS JAKAYA KIKWETE AHADI YA DARAJA

Na Magreth Magosso, Manyara.

WAKAZI wa kijiji cha Magala kata ya Magala wilaya ya Babati mkoa wa Manyara wamemuomba  mh. rais Mrisho Jakaya Kikwete na mbunge wa jimbo hilo kutimiza ahadi waliyoitoa wakati wa kamapeni zao  juu ya ujenzi wa Daraja la Magala ambalo ni kero kwa utekelezaji wa shughuli za kijamii na kuchangia ongezeko la vifo wakati wa masika.

Wakizungumzia hilo wakazi wa kijiji hicho kwa nyakati tofauti Mwidini Said na Edward Michael na kuungwa mkono na mhifadhi mkuu wa ujirani mwema hifadhi ya Manyara Ibrahimu Minga walisema kuwa ahadi hiyo ilitolewa na mh. Kikwete pamoja na mbunge wakati wa kampeni mwaka 2010 ambapo ahadi zimekuwa zikitolewa tangu mwaka 1960 bila kuwepo utekelezaji.

Walisema daraja hilo limekuwa kero kwa muda mrefu hasa wakati wa masika ambapo shughuli za uzalishaji mali husimama, kuharibika kwa mazao ya wananchi pamoja na masomo kwa wanafunzi kutokuwepo kwa kipindi hicho hadi hapo mto Magala utakapokauka ndipo wanafunzi wanaweza kwenda shule.

Alisema licha ya kujitokeza kwa matatizo hayo lakini pia wananchi hupoteza maisha wanapohitaji kuvuka pamoja na magari kuzama katika mto huu na kusababisha umaskini kwa wamiliki wa magari hayo kuingia hasara ya matengenezo na wakati mwingine magari hayo yanakuwa hayana uwezo wa kufanya kazi na kusababisha umaskini kwa wakazi hao.

“mto huu  ni kero kubwa kwa wakazi na watalii ambapo kipindi cha masika hali ya utalii inakuwa ngumu ukizingatia hifadhi ya Manyara inavivitio vingi na watalii wanakuja kwa wingi na kuongeza pato la taifa hivyo msimu wa mvua utalii unakuwa mgumu katika hifadhi hiyo na kusababisha kushuka kwa mapato na watalii kupungua” alisema mhifadhi Minga.

Aidha wakizungumzia tatizo hilo mwalimu wa shule ya sekondari Magala Stella Ezekieli na wanafunzi wa shule hiyo Ruth Paulo na Osiana Thadei wa kidato cha nne walisema kipindi cha mvua hulazimika kukaa nyumbani hadi hapo mto utakapo kauka hali inayoadhiri maendeleo ya masomo na kusababisha ufaulu kuwa wa kiwango cha chini.

Waliiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kuwajengea daraja katika mto huo ili shughuli mbalimbali zifanyeke katika kipindi cha masika sambamba na mazao ya kilimo kubebwa na maji, na mto huo kuongezeka kila mwaka nyakati za mvua.

Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Karatu Fidelix Kijiko alisema licha ya mto huo kutopitika ambao uko mbali na wilaya yake lakini mto huo unaadhari ziwa Manyara ambapo husababisha kujaa kwa kina cha maji kutokana na shughuli za kibinadamu zinazo endelea karibu na mto huo.

Alisema serikali ni sikivu na itafanyia kazi malalamiko ya wakazi wa kata hiyo ili kuwaondolea adha wanazozipata wakati wa masika licha ya kujitahidi katika wilaya ya Karatu kuhakikisha wananchi wanatunza mazingira ili kuhifadhi ziwa hilo ambalo ni kivutio kikubwa kwa kuongeza watalii mkoani humo.

Jimbo hilo kwa muda mrefu limekuwa likitawaliwa na chama cha mapinduzi CCM na kila anayeomba kura anaahidi kufanya ujenzi wa daraja hilo na kuwa sehemu ya kuwapatia watu kura za bure jambo ambalo wakazi wa eneo hilo kuona kama wanafanyiwa mchezo na kutangaza ni bora kutoa kura kwa vyama pinzani ili waweze kupigania ujenzi wa daraja hilo.

No comments: