Na Allan Ntana, Tabora
NI DHAHIRI abiria walio wengi hawajui
haki zao ni zipi wanapokuwa safarini na hata ajali inapotokea au gari
kuharibika au kukatishwa safari kabla ya kufika mwisho wa safari iwe kwa
usafiri wa majini au nchi kavu hawajui haki zao ni zipi au wafanye nini.
Kwa mantiki
hiyo Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
( SUMATRA) mkoani TABORA
imedhamiria kutoa elimu ya
matumizi bora ya vyombo vya usafiri na haki za abiria wanaotumia vyombo hivyo.
Afisa mfawidhi
wa SUMATRA mkoani Tabora Joseph Michael
anabainisha kuwa mamlaka hiyo imeamua kuchukua hatua hiyo ili kupunguza
kero mbalimbali zinazowakabili watumiaji wa vyombo hivyo vya moto ambazo
zinapelekea wengi wao kupoteza haki zao za msingi ikiwemo kupoteza mali, kupata
ulemavu au kifo.
Michael
anaongeza kuwa kama watumiaji wa vyombo hivyo watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya haki zao na uelewa
wa sheria na kanuni za usalama wa barabarani ajali na misuguano kati ya abiria,
makondakta au mwenye chombo itapungua kwa kiasi
kikubwa.
Aidha anasema katika mwaka
wa fedha wa 2014/2015 SUMATRA
imeweka mkakati wa kutoa mafunzo kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri
ili wasafiri hao waweze kujua wajibu na haki yao ya kupata taarifa mbalimbali pindi
wanapokuwa safarini.
Anasema kama
wasafiri hao wakijua haki zao pindi wanapokuwa safarini watakuwa na uwezo wa
kugomea chombo hicho cha usafiri pale
watakapoona hakina vigezo vya kusafirisha abiria pia watakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya
nauli stahiki wanazostahili kulipia ambazo pia
zimeidhinishwa na SUMATRA.
Haki za abiria safarini;
Akifafanua
baadhi ya haki za msingi kisheria kwa watumiaji vyombo vya barabarani kwa
mujibu wa mamlaka hiyo, Michael anasema;
Abiria ana haki
ya kurudishiwa nauli yake chombo cha
usafiri kinapochelewa kuanza safari saa mbili baada ya muda uliopangwa kwenye ratiba
na tiketi (kanuni No.21-(2)), pia ana haki
ya kupewa tiketi ndani ya ofisi ya mtoa huduma ya usafiri husika na siyo vinginevyo (kanuni ya 17- (1p ) na ya 24–(1 ).
Anataja haki
nyingine kuwa ni kutonyanyaswa au kutumia lugha
za matusi au vitendo vyovyote kinyume na taratibu au kwa mujibu wa haki
za binaadamu iwe kwa abiria mtu mzima au
mwanafunzi kama kanuni ya 18-(1a,g,h ).
Haki nyingine ni ya kufikishwa mwisho wa
safari yaani kituo husika anakoelekea abiria (kanuni ya 18-(1d), haki ya kutosimamishwa
ndani ya chombo cha usafiri hasa kwa mabasi ya mikoani awapo
safarini (kanuni 17- 1f) ), Haki ya kulipa nauli iliyoidhinishwa na mamlaka
ya SUMATRA na si zaidi
ya kiwango husika (kanuni ya 34-1, 2, 3) ).
Haki ya kutoendeshwa na dereva mmoja (kwa mabasi ya
mikoani ) zaidi ya saa nane (kanuni ya
17-1g), kulindwa kwa mikanda ya usalama
(Passengers seat belt ) wakati wote wa
safari (kanuni ya 17-1i ), kupata huduma muhimu za usafiri, afya na taarifa zinazohusiana na safari yake (kanuni ya 17-
11,m,n).
Pia
anaongeza kuwa abiria ana haki ya kurudishiwa nauli pungufu ya 15% tu ya kiasi
alicholipa kama ilivyoainishwa
kwenye tiketi endapo abiria atavunja safari ndani ya muda chini ya saa 24 kabla ya muda wa chombo cha usafiri kuanza
safari (kanuni ya 24-3).
Wafanyakazi katika gari la abiria wanakatazwa nini;
Michael
anaeleza kuwa kanuni ya 18 ya sheria za SUMATRA [GN] NO.218/2007 inaelezea
wafanyakazi katika gari la abiria wakiwa kazini wanakatazwa kutofanya mambo
yafuatayo;
Kutumia
lugha chafu ya
uhasama kwa abiria, kuwaziba au kuwazuia
kwa makusudi wahudumiaji wenyewe wa usafiri,
kuendesha gari zaidi ya vikomo vya spidi kwa
kushindania abiria au kukatisha safari
kabla ya kufika kituo cha mwisho.
Mfanyakazi au dereva wa gari haruhusiwi kuendesha
gari la abiria akiwa amekunywa
pombe au kutumia madawa ya kulenya kiasi chochote kile pia haruhusiwi kuendesha gari la abiria kwa uzembe au namna
ya hatari au kinyume na sheria ya usalama
barabarani au sheria nyinginezo.
Aidha
haruhusiwi kubughudhi au kusumbua abiria kwa namna yoyote ile hata kama ni mwanafunzi,
kuendesha gari la abiria hali dereva anazungumza na simu za kiganjani na kupakia wanyama hai au vitu vya hatari
kwenye gari la abiria.
Aidha
Michael anabainisha kuwa mmiliki wa leseni ya gari la abiria au mtumishi wake
ambaye atavunja au kushindwa kutekeleza kanuni ndogo ya [1] atakuwa anatenda kosa la jinai na
anapaswa, kutiwa hatiani, kutozwa
faini isiyo chini ya laki tano, au kufungwa jela kwa muda usiyopunguwa mwaka 1 na
usiozidi miaka miwili au vitu kwa pamoja.
Gari la abiria likiharibika njiani
abiria afanye nini;
Michael
anaeleza kuwa Kanuni ya 22 ya sheria za SUMATRA [GH] No. 218/2007 inayohusu kuharibika
kwa gari la abiria inasema ikiwa gari la abiria litaharibika au haliko
katika hali ya kuanza au kuendelea na safari, mmiliki wa
leseni ya gari au mfanyakazi wake lazima atafute mbadala wa usafiri ndani ya
dakika 10 au arudishe nauli.
Anaongeza
kuwa gari likiharibika linatakiwa kuondolewa barabarani na kama gari hilo
linatoa huduma ndani ya mji na mji basi litengenezwe ndani ya muda usiozidi
masaa.
Ikiwa baada ya matengenezo ya gari la abiria kwa
mujibu wa kanuni ndogo ya 1[b] gari hilo bado
haliko katika hali ya kuanza au kuendelea na safari, mmiliki wa leseni au mfanyakazi
lazima atoe usafiri mbadala.
Haki ya kulipia Mzigo.
Michael
anaeleza kuwa kanuni ya 23 ya sheria za
SUMATRA [GN] No. 218/2007 inasema abiria
ana haki kubeba mzigo wenye uzito wa kilo 20 na mtoto mzigo wenye uzito
wa kilo 10 bila malipo ila akibeba mzigo zaidi ya ule unaoruhusiwa kubebwa bila
malipo mmiliki wa leseni ya gari la abiria ana haki ya kumtoza kwa kilo ya
ziada kwa mujibu wa viwango vilivyoruhusiwa.
Haki ya Kufuta oda ya safari na Kurudishiwa
Nauli.
Michael
anasema Kanuni ya 24 ya sheria za SUMATRA
[GN] No 218/2007 inatoa haki kwa abiria kufuta oda yake ya safari ndani ya masaa
24 au zaidi kabla ya muda wa kuanza
safari ya gari la abiria na kurudishiwa nauli yake.
Abiria ana
haki ya kurudishiwa nauli baada
ya kukatwa asilimia 15 ya nauli
hiyo endapo oda ya safari itafutwa ndani ya muda unaopungua masaa 24 kabla ya muda uliopangwa.
Haki ya Kupewa Tiketi.
Michael anabainisha
kuwa Kanuni ya 25 ya sheria za SUMATRA
[GN] No.218/2007 inazungumzia haki ya abiria kupewa tiketi yenye jina lake pamoja na namba ya kiti chake na haki ya
kufahamu muda wa kuwasili kituoni na kuanza safari.
Abiria pia ana haki ya kufahamu kituo aendacho, tarehe ya kutolewa tiketi na tarehe ya safari, kufahamu namba
ya usajili wa gari hilo la abiria,
kufahamu nauli ya safari hiyo, kufahamu
jina la njia ihudumiwayo, na kufahamu
anuani na namba ya simu ya mmiliki wa leseni ya gari hilo.
‘Kwa huduma za usafiri ndani ya mji, mmiliki
wa gari la abiria atatoa tiketi zilizochapishwa ambazo zinaonesha namba ya usajili wa gari lenye leseni, njia, nauli
iliyoidhinishwa, jina na anuani ya gari au mmiliki wake na tarehe ya kutolewa’, aliongeza.
Nauli za Watoto na Wanafunzi.
Anafafanua
kuwa Kanuni ya 26 ya sheri za SUMATRA
[GN] No.218/2007 inabainisha kuwa kila mtoto na mwanafunzi atakayepanda gari la
abiria atakua na haki ya kusafiri kwa kulipa nusu ya nauli anayotozwa mtu mzima kwa safari hiyo hiyo.
No comments:
Post a Comment