Mkuu wa wilaya ya Tabora mjini Bw.Suleiman Kumchaya akisikiliza malalamiko ya ardhi toka kwa wananchi wa kata ya Ipuli manispaa ya Tabora. |
Wananchi wakitoa malalamiko kwa viongozi |
Wananchi wakitoa walalamiko yao kwa viongozi huku wakishutumu watendaji wa Serikali kutoshughulikia malalamiko yanayotolewa. |
Na Allan Ntana, Tabora
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora hapa nchini imeanza
kuboresha huduma zake kwa jamii baada ya kuanzisha huduma mpya ya kupokea
malalamiko ya wananchi kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia simu za kiganjani.
Hayo yalibainishwa jana na Maofisa wa Tume hiyo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa stendi ya zamani mjini Tabora
ambao ulilenga kutambulisha na kuhamasisha matumizi ya huduma hiyo kwa wananchi
na wadau mbalimbali wenye malalamiko yoyote au kutotendewa haki mkoani hapa.
Afisa uchunguzi na mwanasheria wa tume hiyo Caroline Shayo
alisema tume hiyo iliyoanzishwa Julai 2001hapa nchini imelenga kulinda na
kutetea maslahi ya wananchi ambapo imejiwekea utaratibu wa kupokea na
kushughulikia malalamiko mbalimbali ya wananchi kuanzia ngazi ya serikali kuu
mpaka ngazi ya vijiji.
‘Mpaka sasa tume hii ina ofisi katika kanda 4 tu ambazo ni Lindi, Mwanza, DSM na Zanziba,
lengo letu ni kuelimisha umma ili wafahamu wajibu wao ni nini, haki zao ni
zipi, wanawezaje kuzipata na kwa utaratibu gani’, aliongeza Shayo.
Mchambuzi Mkuu wa mifumo ya habari na mawasiliano wa tume
hiyo Wilfred Warioba, alisema ili kurahisisha mawasiliano ya tume hiyo na
wananchi, wameamua kuanzisha teknolojia hiyo ya kutuma malalamiko moja kwa moja
kupitia mitandao ya simu zao kwa njia ya ujumbe mfupi yaani ‘sms’.
Aliongeza kuwa tume ya haki za binadamu na utawala bora ni
chombo huru ambacho kiko kwa ajili ya kutetea wananchi wote na hakitozi gharama
yoyote ya kuwasilisha malalamiko.
Mtaalamu huyo aliongeza kuwa tume inapokea malalamiko ya
aina yoyote ile bila kujali yameletwa na nani ili mradi yawe na ukweli ndani
yake, kinachotakiwa ni mhusika kuandika malalamiko yake kwenye sehemu ya
kuandika ujumbe mfupi kwenye simu yake ya mkononi na kisha kuutuma kwenye namba
0754 460 256.
Ujumbe huo ukishapokelewa mhusika (mlalamikaji) atapigiwa
simu na kuulizwa baadhi ya mambo ili kujua kiini cha malalamiko yake kwa lengo
la kujiridhisha ikiwa ni pamoja na kufahamu anaitwa nani, yuko wapi na mambo
mengine yatakayoturahisishia kushughulikia malalamiko yake kwa wepesi zaidi,
aliongeza.
Aidha Warioba alisema mwananchi yeyote atakayeleta
malalamiko yake kwa ‘sms’ anatakiwa kutumia majina yake halisi na kutaja mahali
alipo na si kusema uongo lengo likiwa kurahisisha kazi ya kushughulikia
malalamiko yake.
Alifafanua kuwa tume hii haina upendeleo wowote wa kijinsia
katika kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayopokelewa huku akibainisha
kuwa wananchi walio wengi bado hawajajua
wajibu wao kwani wanayo matatizo mengi ila wanayanyamazia tu ndio maana
tumewatembelea ili waseme waziwazi.
Naye Catherin Malimbo, Afisa Uchunguzi Mwandamizi idara ya
haki za binadamu, aliwataka wananchi wote wenye malalamiko ya masuala ya ardhi,
viwanja, biashara na ndoa kuleta malalamiko yao pia kwani wapo tayari
kuyafanyia kazi sambamba na kutoa ushauri kwa mamlaka husika namna ya kumaliza
kero hizo kisheria.
No comments:
Post a Comment