…………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurungenzi Mtendaji mpya wa
Shirika la Madini la Taifa, Mhandisi Edwin Ngoyani ameahidi neema kwa
wachimbaji wadogo wa madini na vito nchini kwa kuwawezesha kupata masoko
ya bidhaa zao pamoja na kuwapatia zana za kisasa za uchimbaji madini.
“Malengo yangu makuu katika
shirika hili ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanawezeshwa kunufaika na
rasilimali za nchi yetu pamoja na kuhakikisha kwamba STAMICO linatoa
mchango wa mapato katika mfuko mkuu wa hazina kwa kujiendesha kwa
faida,” Mhandisi Ngonyani alisema katika mkutano na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa kujiamini,
Mhandisi Ngonyani alisema anatarajiwa malengo yake katika STAMICO
yataanza kuzaa matunda ndani ya miaka miwili mpaka mitatu ijayo.
Akizungumzia mkakati kwa
wachimbaji wadogo, Ngonyani alisema,ndani ya miaka miwili ijayo, shirika
hilo litanunua mitambo miwili ya uchimbaji wa madini ya kisasa
(drilling rigs) ambayo itatumiwa na wachimbaji wadogo.
“Lengo ni kuwafanya wachimbaji
wadogo wanufaike na wawe sehemu ya uwekezaji kwenye rasilimali zao, kama
ambavyo hao wawekezaji wa nje wanavyowekeza, na sasa watanzania nao
watawekeza, ila lazima tuwawezeshe,” Ngonyani alisisitiza.
Alisema lengo la STAMICO kwa
wachimbaji wadogo ni kuhakikisha wanawezeshwa kuwekeza na kuchimba
kisasa ili pia watoa mitaji ambao ni benki wawe na uhakika wa fedha zao
kurejeshwa, na kwamba hata ikibidi, shirika hilo litawawekea dhamana ili
wawezeshwe kibenki.
Alisema hilo litawezekana baada ya
mkakati wao wa kuanzisha na kuboresha takwimu za wachimbaji wadogo
ambazo zitakuwa na taarifa zao ikiainisha mahali walipo,aina ya madini
wanayochimba na mahitaji yao.
Pia mkakati mwingine ni kubaini
vyanzo vya migogoro kwenye maeneo ya wachimbaji na kutafuta suluhu ikiwa
ni pamoja na kutenga maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo ili kuepusha
migogoro isiyo ya lazima.
Katika hatua nyingine, Ngonyani
alizungumzia mradi wa uchimbaji madini kwenye mgodi dhahabu wa Tulawaka
ambao hivi sasa umenunuliwa na shirika hilo na kuitwa Biharamulo
unaosimaimamiwa na kampuni ya StamiGold.
Alifafanua kwamba mgodi huo
utaanza kazi rasmi Agosti 8, mwaka huu na kwamba baada ya miaka miwili
na nusu, wanatarajia kupata faida ya shilingi bilioni saba.
Awali mgodi huo ulikuwa
ukimilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG) na mwishoni mwa
mwaka jana STAMICO ikaununua kwa dola za Marekani milioni tano.
ABG iliuza mgodi huo kutokana na
kwamba kiasi cha wakia 100,000 kilichopo katika eneo la mradi ni kidogo
kwa uchimbaji mkubwa kwa kampuni hiyo kubwa ya madini duniani.
“Hata hivyo tuna matumaini kwamba
katika eneo la kilometa nne kutoka kwenye eneo la mradi kuna uwezekano
wa kuwapo mashapo ya kati 150,000 mpaka 200,000. Tutaendelea na utafiti
katika eneo hili,” Mhandisi Ngonyani alisema.
Kwa upande wake, Meneja
Uchorongaji wa Stamico, Alex Rutagweleka alisema hivi sasa miradi mitano
iko kwenye ubia na shirika hilo kwa ajili ya uwekezaji na kuitaja
miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa Itetemia mgodi wa dhahabu ambao
Stamiko wameingia ubia na Kampuni ya Madini ya Tancan Ltd.
Mradi mwingine ni wa Buckreef wa
dhahabu ulioko Geita ambao Stamico wameingia ubia na Kampuni tanzu ya
TANZAM 2000, ambapo Stamico wana hisa asilimia 45 na 55 iko kwa kampuni
hiyo na kwamba wanategemea uzajishaji utaanza Novemba mwama huu.
Aidha mradi mwingine ni Kiwira ambao unazalisha makaa ya mawe kwa ajili ya kufua umeme utakaounganishwa kwenye gridi ya taifa.
Akizungumzia mradi huo,Meneja
fedha na Utawala wa Stamico, Peter Gembe alisema lengo la mradi huo ni
kufua megawati 200 za umeme kwa ajili ya kuunganisha kwenye gridi ya
taifa kutoka kwa kiwango cha awali cha megawati 6.
Stamico ni shirika la umma
lililoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kuongeza mchango wa sekta ya
madni katika pato la taifa na kuzalisha nafasi za ajira kwa watanzania.
No comments:
Post a Comment