Pages

KAPIPI TV

Sunday, June 15, 2014

KANISA LA ‘TAG’ LATENGA MIL.270 KWA AJILI YA MISAADA YA KIJAMII


Na Allan Ntana, Tabora

IKIWA ni miaka 75 sasa tangu kuanzishwa kwa kanisa la Tanzania
Assemblies of God hapa nchini, jumla ya sh mil.270 zimetengwa kwa
ajili ya kutoa misaada mbalimbali ya kijamii katika sherehe za
maadhimisho ya Jubilee ya kanisa hilo hapa nchini.

Hayo yalibainishwa jana na Askofu Mkuu wa kanisa hilo hapa nchini Dr
Barnabas Mtokambali katika ibada maalumu iliyofanyika katika uwanja wa
ofisi mpya za jimbo mjini Tabora.

Alisema katika kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo
hapa nchini kanisa limeandaa kiasi cha sh milioni 270 kwa ajili ya
kutoa misaada mbalimbali ya kijamii kwa makundi ya watu mbalimbali
wenye uhitaji.

Dr Mtokambali alifafanua kuwa watatoa vyandarua, damu na vitu
mbalimbali kwa jamii ya watanzania wenye uhitaji pasipo kujali dini ya
mtu, rangi wala kabila, lengo likiwa ni kumshukuru Mungu kwa
kuliwezesha kanisa hilo kutimiza miaka 75.

Alisema sherehe za maadhimisho ya Jubilee ya kanisa hilo
lililoanzishwa mwaka 1932 hapa nchini na sasa likiwa na waumini zaidi
ya milioni 5 tayari zilishaanza katika makanisa ya TAG hapa nchini na
zinaendelea katika majimbo yote 32 ya kanisa hilo.

Kilele cha maadhimisho hayo ya kihistoria  yatakayohudhuriwa na maelfu
ya watu wakiwemo maaskofu , wachungaji, viongozi wa taasisi,
mashirika, dini mbalimbali, viongozi wa serikali na wananchi kitakuwa
tarehe 13Julai 2014 jijini Mbeya na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema.

Aidha Mtokambali alipongeza jitihada thabiti za kimaendeleo
zinazofanywa na uongozi wa TAG jimbo la Tabora chini ya uongozi wa
Askofu Paul Meivukie kwa kuwa na mikakati endelevu ya kuimarisha kazi
ya Mungu jimboni humo sambamba na uanzishwaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo.

‘Askofu Meivukie hongera sana kwa moyo wako wa kujituma, naomba
mwendelee kushirikiana hivi hivi ili mikakati yenu ya kuanzisha miradi
ya maendeleo kama mlivyosema ifanikiwe, naahidi kuwapeni ushirikiano
kama kiongozi wenu’, alisema.

Akizungumzia mchakato wa katiba mpya unaoendelea hapa nchini, Dr
Mtokambali alishauri kipengele cha muundo wa serikali 1,2 au 3 ambacho
kinaonekana kuwagawa wabunge wa bunge hilo maalumu kiletwe kwa
wananchi ili wao ndio waamue, kwani wananchi wanao uwezo wa kuamua kwa
busara badala ya kuendeleza malumbano.

‘Kama suala hilo limeshindikana kuamuliwa, tunaomba bunge liturudishie
tutoe uamuzi sisi wenyewe, tunahitaji katiba itakayotuletea maendeleo
katika ngazi zote vijijini na mijini na itakayodumisha uhuru na amani
katika nchi na katika kuabudu’, aliongeza.

Pia aliwataka wachungaji wote wa TAG hapa nchini kuhamasisha waumini
wao kujiunga na vyama vya siasa sambamba na kugombea nafasi mbalimbali
za uongozi huku akionya wachungaji hao kutokuwa  wanachama wa chama
chochote cha siasa.

Awali askofu wa jimbo la Tabora Paul Meivukie alimweleza Askofu Mkuu
Mtokambali kuwa wameazimia kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii
ikiwemo kuanzisha vituo 2 vya kuhudumia watoto yatima katika wilaya za
Sikonge na Uyui,  tayari vimeanza kazi.

Mradi mwingine ni mradi wa kufyatua matofali ya kuuza (interlock)
mashine yenye uwezo wa kufyatua tofali 1000 kwa siku moja tayari
imenunuliwa na ujenzi wa kituo cha jimbo la Tabora nao tayari umeanza.

Miradi inayotarajiwa kuanzishwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha
Wachungaji, ujenzi wa shule 2 za sekondari, uchimbaji visima 3 vya
maji na ujenzi wa kituo cha afya katika eneo la Ipuli katika manispaa
ya Tabora.

No comments: