
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Usoha Njiapanda iliyopo Mbeya Vijijini.

Mwenyekiti
wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, , Willson Mwamunyila (katikati)
akizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini kwake.

Baadhi ya wanakijiji wa Kijiji cha Usoha Njiapanda wakiwa katika mkutano na mwanahabari hizi.
VITISHO
na hofu ya vitendo vya ushirikina imebainika kuwa vikwanzo vya
mapambano ya baadhi ya watu wanaowatia mimba wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari katika Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini,
mkoani Mbeya.
Kauli hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na baadhi ya
wanakijiji kutoka katika baadhi ya vijiji vya Kata ya Tembela
walipofanya mahojiano kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi
alipotembelea vijiji hivyo.
Akizungumza
mkazi wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Maria Kolneri alisema baadhi ya
wazazi hushindwa kuwawajibisha watu waliowatia mimba wanafunzi kwa
kuhofia usalama wao kwani familia iliyotuhumiwa hujenga uhasama na
familia ya mwanafunzi na hata kutoa vitisho. Alisema katika kijiji hicho
ni vigumu kwa familia ya mwanafunzi aliyetiwa mimba kufuatilia ili
sheria ichukuwe mkondo kwani huwa kuna vitisho na vingine kutoka kwa
majirani wa familia hizo.
“…Hapa
ukianza tu kumfuatilia mtu aliyefanya kosa kama hilo unasikia
wanakijiji wanaanza kulalamika anataka kumfunga mwenzake sasa mtoto
atakaye zaliwa atalelewa na nani…? Watakusema huku familia yenye kosa
ikitoa vitisho hadi utaacha kufuatilia,” alisema.
“Ukitaka kupata kesi (uhasama)
hapa kijijini kwetu mfunge kijana aliyempa mimba mtoto wako…, kila
mwanakijiji anayekujua atakuona hufai kwa madai kuwa umemwonea kijana
uliyemshtaki,” alisema mama huyo.
Aidha
aliongeza kuwa baadhi ya familia uhofia vitendo vya ushirikina
(kulogwa) endapo utaendelea kufutilia kesi za mimba hivyo kukata tamaa,
jambo ambalo kwa sasa kijijini hapo limekuwa la kawaida.
Naye
Nazareti Kibaga mkazi wa Kijiji cha Simambwe alisema kutokana na hali
hiyo wananchi wamekuwa wagumu kufuatilia kesi za mimba jambo ambalo
limefanya matukio hayo kuendelea licha ya changamoto zingine
zinazochangia uwepo wake.
“…Hali hii imefanya mimba
ziendelee na hakuna kesi yoyote dhidi ya wanaowatia mimba wanafunzi…,
wazazi hawawajibiki, wananchi hawawajibiki na viongozi nao
hawawajibiki,” alisema Kibaga.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Usoha Njiapanda, Willson Mwamunyila
alikiri uwepo wa matukio ya mimba kwa kiasi kikubwa kijijini hapo
lakini alisema kikwazo katika kushughulikia matukio ya mimba ni uongozi
kukosa ushirikiano kutoka kwa wazazi na mwanafunzi.
“…Matatizo
ya mimba yapo lakini wazazi na wanafunzi waliotiwa mimba hugoma kutoa
ushirikiano kwa viongozi ili wahusika washughulikiwe kisheria. Unakuta
mtoto kapata mimba baada ya taarifa kukufikia unaenda kwa mzazi wa
mwanafunzi kuomba ushirikiano lakini wazazi wengine wanakuzunguka
wanazungumza na mwalimu kwenye shule husika na wanamalizana wenyewe,”
alisema Willson Mwamunyila.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TGNP


No comments:
Post a Comment