Pages

KAPIPI TV

Monday, April 21, 2014

‘MSEA’ YAJIPANGA KUPAMBANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA TABORA


Tabora

KASI ya uharibifu wa mazingira katika mkoa wa TABORA imeelezwa kuwa ni kubwa mno  kutokana na kukithiri kwa shughuli mbalimbali za kijamii zisizozingatia kanuni za utunzaji mazingira katika manispaa ya Tabora na maeneo mengineyo.

Hayo yameelezwa na meneja miradi wa taasisi ya MSEA (Mwanza Sustainable Environment Association) kanda ya Magharibi Bw. Stan Fusi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora.

Alisema kuwa hali hiyo inatokana na wananchi walio wengi kutokuwa na elimu ya utunzaji wa mazingira katika maeneo yao na kutoelewa matumizi bora na uhifadhi wa maeneo yanayowazunguka.

Aidha alisema taasisi yake kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa TABORA wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya  umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa kuwawezesha kushiriki  zoezi la upandaji miti kupitia mradi wa miombo.

Akifafanua zaidi alisema elimu hiyo imelenga kuwasaidia wananchi kuzalisha mazao ya ‘timbau’ ambayo yanatokana na misitu zikiwemo mbao, magogo na mazao mengine yasiyo ‘timbau’ mfano ufugaji nyuki na kilimo cha mseto bila kuathiri mazingira katika maeneo hayo.

Meneja huyo alibainisha kuwa jitihada za kutoa elimu hiyo mpaka sasa zimefikia kaya 12,500 kwa wilaya nne  za mkoa wa TABORA lengo likiwa  kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira kuanzia maeneo yanayowazunguka hadi katika misitu.

Alizitaja wilaya hizo kuwa ni Urambo,Tabora Manispaa, Uyui na Sikonge ambapo aliwaasa wananchi wake kuzingatia elimu wanayoipata kwa kuepuka athari za uharibufu wa mazingira

Akizungumzia shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira Fusi alisema ni ukataji miti ovyo na uchomaji misitu na mkaa unaofanywa na wakulima na wafugaji kwa ajili ya kilimo na maeneo ya kulishia mifugo yao pamoja na uchimbaji holela mchanga wa kufyatulia tofali.

Hivyo akaasa wakulima na wafugaji hao kufuata kanuni, taratibu na ushauri unaotolewa na maofisa kilimo na mifugo na wadau wengineo ili shuguli hizo zisiendelee kuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira badala ya kuboresha mazingira hayo.

Aidha aliwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na uongozi wa serikali ya mkoa zikiongozwa na mkuu wa mkoa huo  Fatma Mwassa, Katibu Tawala Kudra Mwinyimvua na wadau wengine ili kuboresha mazingira ya mkoa huo.

Aliongeza kuwa pamoja na elimu inayoendelea kutolewa na serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wa misitu ikiwemo MSEA bado wananchi walio wengi hawana mwamko wa kutosha wa kusimamia miradi hiyo.

No comments: