Pages

KAPIPI TV

Monday, April 21, 2014

CRDB YAKOPESHA WAKULIMA WA TUMBAKU TABORA DOLA MIL.42


Na Mwandishi wetu, Tabora

BENKI ya CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya dola za Kimarekani
mil. 42 katika mwaka wa fedha 2012/13 kwa vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku vipatavyo 143 vilivyo chini ya Chama kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi, WETCU Ltd.
 
Mkuu wa Kitengo cha Mikopo cha benki hiyo,Taitus Tumaini alisema kiasi hicho kilikopeshwa kwa Vyama hivyo vya msingi msimu wa mwaka 2012/13 na Vyama 85 tayari vimefanikiwa kurejesha mikopo yake.
 
Alieleza kuwa urejeshwaji wa Mikopo hiyo ni kiasi cha asilimia  85 wakati kiasi kilichobaki cha dola za kimarekani mil 7.4 bado zinadaiwa kwa Vyama vya Msingi.
 
Alisema kutokana na hali hiyo Benki hiyo imeamua kuviongezea muda wa kulipa deni hilo Vyama  vya msingi ambavyo vimeshindwa kulipa deni kutokana na uzalishaji mdogo wa zao la tumbaku.
 
“Benki imeamua kuviongezea muda zaidi vyama vya Msingi hamsini na nane kutokana na kushindwa kulipa deni kwa wakati hivyo watalipa deni lao katika kipindi cha Miaka Mitatu” alisema.
 
Aidha aliweka bayana kuwa pamoja na Vyama hivyo vya msingi kuongezewa muda wa kulipa deni hilo pia vimepewa mikopo ya ziada ili wanachama wake waweze kulima tumbaku.
 
Tumaini aliongeza kuwa mazungumzo yalifanyika baina ya Benki hiyo na Chama Kikuu cha ushirika wa wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi na kukubaliana namna ya kulipa deni hilo.
 
Alieleza kwamba benki ya CRDB inamjali mkulima na ndio maana inahakikisha anawezeshwa ili aweze kunufaika na kilimo chake.
 
Mwenyekiti wa bodi ya WETCU, Hassan Wakasuvi katika mkutano mkuu wa 21 wa wakulima wa tumbaku uliofanyika hivi karibuni mjini Tabora, alivitaka Vyama vya msingi ambavyo havijalipa madeni yake vilipe kwani dawa ya deni ni kulipa na sio kulikimbia.

No comments: