Na Anna Nkinda- Maelezo, Lindi
Wakazi wa kata ya Msinjahili
wilayani Lindi wametakiwa kutoogopa kuvuta umeme majumbani mwao kwa
kuhofu kuwa wakifanya hivyo wataonekana ni matajiri kwani matumizi ya
umeme ni ya gharama naafuu ukilinganisha na mafuta ya taa.
Mwito huo umetolea jana na Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) wilaya ya
Lindi mjini wakati akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa
Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika matawi ya Muungano,
Jitegemee, Sinde na Mnali yaliyopo katika kata ya Msinjahili wilaya ya
Lindi mjini.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa
Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema ili kuboresha maisha ya wananchi
Serikali imejitahidi kupitisha umeme wa gesi katika vijiji vilivyopo
katika kata hiyo na kupunguza gharama ya uvutaji ambazo ni nafuu jambo
la muhimu ni kwa wananchi kuutumia.
“Kuwa na umeme nyumbani kwako na
kuutumia ni mwanzo wa maendeleo, hata watoto wako wataweza kuutumia
mwanga huo kwa kujisomea hasa nyakati za usiku na hivyo kufanya vizuri
katika mitihani yao”, alisema Mama Kikwete.
Aidha Mjumbe huyo wa NEC pia
aliwataka viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi kuwahimiza watu
wanaowaongoza katika maeneo yao kutumia mvua zinazoendelea kunyesha
kulima chakula cha kutosha jambo ambalo litawafanya kuwa na chakula cha
ziada na hivyo kuepukana na kitendo cha kuomba chakula kwa majirani.
Akizungumzia kuhusu suala la
uongozi Mama Kikwete aliwahimiza wanawake kutoogopa kuomba na kugombea
nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo ili waweze kupata
nafasi ya kuongoza na hivyo kufika katika ngazi ya maamuzi.
Mama Kikwete alisisitiza , “Sisi
wanawake tunakabiliwa na changamoto nyingi na mtu pekee anayeweza
kuziongelea changamoto zetu kiusahihi ni mwanamke mwenyewe hivyo basi
msiogope kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wakati wa uchaguzi
ukifika mkifanya hivyo kutakuwa na viongozi wengi wanawake ambao
wataweza kuwakilisha matatizo na mawazo yetu katika ngazi za juu za
uongozi wa chama na Serikali”.
MNEC huyo alimalizia kwa kuwahimiza viongozi hao wa Halmashauri
kuu ya tawi ya CCM kuishi maisha ya upendo, mshikamano na amani kwani
jamii ikiishi maisha hayo itaweza kufanya shughuli mbalimbali za
maendeleo kwa kushirikiana.
Kwa upande wake katibu wa Jumuia
ya Wazazi mkoa wa Lindi Haji Tajiri aliwataka viongozi hao kuwa
waaminifu katika ndoa zao na kuepuka tabia ya kuwa na mpenzi zaidi ya
mmoja (michepuko) kwa kufanya hivyo wataepukana na ugonjwa wa Ukimwi.
“Chama Cha Mapinduzi kinahitaji
kuwa na watu wenye afya njema ili waweze kufanya vizuri kazi za chama
nawaomba muwe waaminifu kwa wapenzi wenu mkifanya hivyo mtaepekana na
Ugonjwa wa Ukimwi”, alisema Tajiri.
Katibu huyo wa Jumuia ya Wazazi
mkoa pia aliwaomba kinamama kuiga mfano wa Mama Salma Kikwete ambaye
anafanya kazi kubwa ya kujitoa katika shughuli mbalimbali za kijamii na
kutetea haki zao, wasichana na watoto na kuongeza kwamba anastahili
pongezi kwani yeye ni mama na mlezi wa taifa.
Mjumbe huyo wa NEC taifa akiwa katika kata ya Msinjahili
alifungua mashina ya wakereketwa wa CCM Jumuia ya wazazi katika tawi
namba tatu la Sinde na namba mbili la Mnali.
Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa
NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa
Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama
hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi.
No comments:
Post a Comment