Pages

KAPIPI TV

Sunday, April 13, 2014

CAG LUDOVIK UTOUH AONYA BAHASHA KIGOMA!!!

Na Magreth Magosso,Kigoma

MKAGUZI  wa mahesabu wa kitaifa(CAG) Ludovik  Utouh amewataka Viongozi wa halmashauri za wilaya Mkoa wa Kigoma waache  kuwashawishi kwa bahasha za fedha watendaji wake, pindi wafanyapo ukaguzi wa mahesabu katika maeneo yao.

Akifafanua hilo kwenye mkutano na viongozi wa serikali za hapa, Utouh alisema  amepewa malalamiko toka kwa vijana wake kuwa,wanashawishiwa kwa takrima na bahasha ili kubatilisha uhalisia wa matumizi ya fedha za serikali katika miradi husika kwa lengo la kukwepa kupata hati chafu .

Aliwasihi wakurugenzi wachane na kasumba ya kuogopa wakaguzi wa mahesabu kwani wakaguzi ni chachu ya kuboresha mfumo wa utendaji kazi  wa mazoea na wafanye kazi kwa kufuata kanuni,taratibu za kifedha ili kuubadilisha maisha ya wananchi kupitia miradi husika.

“ imarisheni vitengo vya ukaguzi wa ndani na kamati za ukaguzi kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika kubadilisha mfumo wa kimazoea na badala yake viongozi muwe wabunifu na wazalendo wananchi wanalaumu serikali lakini ukweli watendaji ni shida”alisema Utouh

Kwa upande wa naibu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Bernad Balishinga alisema,halmashauri zinachangamoto za kufanya kazi kwa mazoea kutokana na wakuu wa idara na watumishi kufanya kazi kwa muda mrefu katika kituo kimoja hali inayochangia kuacha kufuata sheria,kanuni na taratibu za kazi.

Naye Mkuu wa wilaya ya Uvinza Hadija Nyembo akiri ubadhirifu wa fedha za miradi  za wananchi waishio katika kata na vijiji zinatafunwa na watendaji wa kata wakishirikiana na wenyeviti wa vijiji hali inayochangiwa na kutokuwa na watendaji maalum ili wakipotoka iwe rahisi kushtakiwa.

Aidha Mkuu wa wilaya Venance Mwamoto alimuomba mkaguzi huyo kuwa uwekwe utaratibu wa mkataba wa kuwashirikisha wananchi katika mchakato wa miradi ili waondokane na hulka ya miradi kuachiwa wachache na hatimaye miradi ya umma kujengwa chini ya kiwango .

Mkaguzi huyo alizitaka halmashauri ziwe na maboresho ya mfumo wa matumizi ya fedha IFMS-Epicor,lengo kuweka utunzaji sahihi na kumbukumbu juu ya matumizi ya fedha na kushauri watoe mafunzo kwa wahazina na wahazini ili wawe na viwango vya utunzaji fedha kwa kiwango cha kimataifa(IPSAS).

No comments: