Pages

KAPIPI TV

Friday, March 7, 2014

MACHIBYA ALIA NA MANISPAA KIGOMA

Na Magreth Magosso, Kigoma.

MKUU wa mkoa Kigoma Lt. Issa Machibya ameitaka Halmashauri ya Manispaa Kigoma ujiji kuboresha miundombinu ya mazingira kwa kuzingatia usafi katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo ili kwenda sambamba na mabadiliko ya uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo  alisema kuwa kwa sasa hali halisi ya manispaa hairidhishi kutokana na kuzagaa kwa uchafu pamoja na miundombinu ya barabara kutokuwa katika viwango vinavyotakiwa katika miji inayoendelea.

Alisema kuwa ni lazima uongozi wa manispaa kujifunza katika mikoa na nchi za jirani jinsi ya kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa bustani za kuvutia, kuboresha nyumba zilizopo katika maeneo ya barabara kuu ziweze kwenda na wakati.

Aidha alisema kuwa maeneo ya makaburi yamekuwa ni maficho ya wahalifu na kusababisha kujitokeza kwa vitendo vya mauaji kutokana na kutowekewa uzio na kufanyiwa usafi wa mara kwa mara ambao utasaidia kuondoa tatizo la wahalifu hao.
 

Kwaupande wake Katibu tawala mkoa wa Kigoma Eng. John Ndunguru alisisitiza kulinda misitu ya uoto wa asili pamoja na ofisi ya mipango miji kuhakikisha inawataka wananchi kuacha kuharibu mazingira ya ziwa Tanganyika kwa kujenga katika vilima mbalimbali vya mkoa wa Kigoma.

Katika kuboresha mkoa wa kigoma ni lazima manispaa itumie sheria ndogondogo kuimarisha mji kwa kupaki magari na pikipiki ili kujiandaa na uwekezaji unaotakiwa kufanyika katika mkoa wa Kigoma pamoja na kujitahidi kulipa fidia za wananchi kwa wakati muafaka ili kuepusha migogoro ya kukwamisha shughuli za maendeleo zisiweze kuendelea.

Naye meya wa Manispaa hiyo Bakari Beji alikiri kuwepo kwa tatizo hilo kutokana na baadhi ya madiwani na wananchi kuwa chanzo cha kurudisha nyuma uboreshaji wa maendeleo mkoani humo na hivyo kuahidi kulifanyika kazi suala hilo katika kipindi kifupi.
 

Hata hivyo manispaa hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 22 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ambapo katika kipindi cha Nov. 2013 ilikusanya asilimia 31 ambayo ilikuwa chini ya kiwango kilichokusudiwa na manispaa hiyo. 

No comments: