Pages

KAPIPI TV

Wednesday, March 5, 2014

KIJANA ALIYEUA BILA KUKUSUDIA AFUNGWA MWAKA MMOJA.-TABORA

Kijana Sanane Machimi akiwa mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Tabora  muda mfupi baada ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja kufuatia kosa la mauaji ya bila kukusudia.


Mahakama ya hakimu  mkazi  mfawidhi mkoa wa Tabora  imemuhukumu  kutumikia kifungo cha mwaka mmoja Jela  kijana anayefahamika kwa  jina la  Sanane  Machimi baada ya kupatikana  na  hatia ya kuua bila kukusudia.



Akisoma  maelezo ya kosa mbele  ya mahakama hiyo,Mwanasheria upande wa Jamhuri  Bw.Nestory  Paschal  aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa  Sanane  Machimi akiwa na umri wa miaka  17 mnamo  tarehe  7 mwezi wa 5 mwaka  2012 alimuua bila kukusudia  mtu  mmoja aliyefahamika kwa jina la Kweji  Ntuvilo kwa kumpiga kwa fimbo kichwani na ubavuni  baada ya kumfumania  anafanya  mapenzi na mkewe  eneo la  vichakani  huko wilayani  Sikonge.


Mshtakiwa  alikiri  kutenda  kosa  hilo   kinyume na kifungu  namba  195 kanuni ya adhabu  sura  namba 16  marejeo  ya  sheria ya  mwaka  2002 ambapo  alieleza kuwa  baada  ya  kumkuta  marehemu  akifanya tendo  la  zinaa na  mkewe  haikuwa  rahisi  kwake  kuvumilia  kitendo  hicho na hivyo  kushikwa  na  ghadhabu  ya  kumshambulia  hali iliyosababisha kifo cha marehemu  Kweji  Ntuvilo aliyekuwa na umri wa miaka 30.


Akisoma  hukumu   baada  ya  kusikiliza  maelezo ya pande zote mbili, hakimu mkazi  mwandamizi  mwenye mamlaka ya ziada Bw.Thomas  Simba  alisema mahakama hiyo  tukufu  imepitia kwa makini shitaka hilo na kumtia hatiani  Sanane  Machimi ambapo alimhukumu kutumikia kifungo cha kwenda Jela  kwa muda wa mwaka mmoja ili iwe fundisho kwa mtu mwingine atakayediriki kufanya kosa kama hilo.


Hata hivyo  mshtakiwa  mara  baada  ya  kusomewa  adhabu  hiyo  alisikika akimshukuru  Mwenyezimungu  akidai kuwa  adhabu  aliyoipata imekuwa na nafuu  sana  kwake  kwakuwa  tayari  alikuwa  amekaa  mahabusu  tangu  mnamo  mwaka  2012.   

   

No comments: