Mkuu wa mkoa wa Tabora Bi.Fatma Abubakar Mwassa wakati wa ufunguzi wa tawi la benki ya Access mjini Tabora ambalo tayari limeanza kutoa huduma kwa wakazi wa Tabora hasa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu.
Na Mwandishi wetu, Tabora
WAKAZI wa manispaa ya Tabora na halmashauri zake
zote wameanza kunufaika na huduma za benki ya ACCESS yenye makao yake makuu
jijini Dar es salaam baada ya kuzinduliwa kwa tawi la benki hiyo mkoani humo.
Sherehe za uzinduzi wa tawi hilo jipya zilifanyika
juzi mbele ya ofisi za benki hiyo zilizoko katika jengo la NSSF mjini Tabora
ambapo ziliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Fatma Mwassa aliyeambatana na Mkuu
wa wilaya ya Tabora Suleiman Kumchaya na baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya
mkoa.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Mwakilishi wa Mkurugenzi
wa benki hiyo kutoka makao makuu jijini Dar es salaam Emanuel Evans alisema
wameanzisha tawi hilo kwa lengo la kuwainua wananchi kiuchumi hususani wakulima
na wajasiriamali wadogowadogo.
Alisema benki hiyo imeanza kutoa huduma zake mkoani
Tabora tangu tarehe 15 Januari mwaka huu na tangu mda huo mpaka sasa wameweza
kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 950 kwa wananchi zaidi
ya 400 na wateja wapya zaidi ya 1,800 wamefungua akaunti.
Alisema kitendo cha wananchi kujitokeza kwa idadi
kubwa namna hiyo katika kipindi kifupi cha miezi miwili tu tangu kuanza kwa
huduma za benki hiyo ni jambo la kujivunia sana na benki imeahidi kuendelea
kuwasaidia ili kutimiza ndoto zao kiuchumi.
‘Kuanzishwa kwa tawi la benki hii hapa Tabora ni
habari njema kwa wakazi wote wa mkoa huu na mikoa ya jirani, tunaomba wananchi
wote mjitokeze kwa wingi kufungua akaunti na kujipatia mikopo pasipo usumbufu
wowote, kufungua akaunti ni sh 1000 tu’, alisema.
Katika taarifa yake mwakilishi huyo alisema Access
ni benki iliyodhamiria kuwasaidia Watanzania wenye kipato cha chini na cha kati
na pia imelenga kuwa kimbilio la wananchi wote hapa nchini kwa kuwapatia huduma
bora za kibenki zitakazowainua kimaisha.
Aliongeza kuwa Access Bank Tanzania (ABT) ni benki
ya kibiashara inayokua kwa haraka sana, ilianzishwa mwaka 2007 hapa Tanzania
ikilenga kuwasadia wakulima na wajasiriamali wadogo na wakati ambapo mpaka sasa
ina jumla ya matawi 10 katika mikoa mbalimbali na imeweza kutoa mikopo kwa
zaidi ya wateja 85,000 yenye thamani ya zaidi ya sh bil.325.
Afisa huyo alimwambia Mkuu wa mkoa kuwa ABT
imejiwekea utaratibu uliotofauti na taasisi nyingine hapa nchini ambapo huajiri
vijana wanaomaliza vyuo na kuwapa mafunzo bila kujali uzoefu wao wa kazi lengo
likiwa kuwajengea mshikamano, weredi na utamaduni wa benki.
Mpaka sasa ABT imeajiri wafanyakazi wapatao 600
tangu kuanzishwa kwake hapa nchini wakiwemo wafanyakazi zaidi ya 50 wa tawi la Tabora
jambo linaloifanya benki hiyo kuwa moja kati ya benki zilizoajiri wafanyakazi
wengi zaidi hapa nchini.
Akizungumzia huduma mbalimbali zinazotolewa na benki
hiyo, Evans alisema ABT inatoa mikopo ya kuanzia sh.100,000 hadi sh.900,000
kulingana na uwezo wa mwombaji, mikopo ambayo hutolewa kwa masharti nafuu sana.
Huduma nyingine ni akaunti ya akiba, akaunti ya
hundi, akaunti ya mda maalumu, akaunti ya malengo maalumu, akaunti ya
wanafunzi, akaunti ya wafanyakazi, huduma za utumaji na uhamishaji fedha ndani
na nje ya nchi kwa kutumia M-PESA, WESTERN UNION, TISS na SWIFT.
No comments:
Post a Comment