Pages

KAPIPI TV

Thursday, February 20, 2014

WATOTO MAPACHA WALIOTENGANISHWA NCHINI INDIA WAREJEA JIJINI DAR

Picha na 1
 Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.
……………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa – MAELEZO
 Dar es salaam.
Hatimaye watoto mapacha kutoka wilayani Kyela mkoani Mbeya waliokuwa wamepelekwa na serikali chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha jana jioni wamerejea nchini wakitokea nchini India katika hospitali ya watoto ya Appolo walikokuwa wanapatiwa matibabu.
Mara baada ya kuwasili katika  Uwanja ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wakiwa wameambatana  na mama yao mzazi Grace Joel na Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India ambaye pia alikuwa masomoni akisomea magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt. Glory Joseph wamepokewa na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Nje wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Edward Sawe  na baadhi ya wauguzi kutoka Taasisi ya Mifupa (MOI) .
Mapacha hao wa kiume wakiwa wenye  furaha na afya njema walichukuliwa katika gari maalum na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) ambako watakaa kwa muda mfupi na kisha kuruhusiwa kuelekea wilayani Kyela jijini Mbeya ambako ndiko walikozaliwa.
 Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao akizungumza kwa furaha mara baada ya watoto wake kupatiwa matibabu ya kuwatenganisha kwa mafanikio makubwa amesema kuwa sasa maisha yake yamebadilika na ataishi kwa furaha na watoto wake.
“Najisikia furaha sana kwa hatua niliyofikia mpaka hapa watoto wangu Eliudi na Elikana sasa ni wazima naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa msaada ilionipatia” amesema.
Kwa uipande wake Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini India ambaye pia alikuwa masomoni akisomea magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt. Glory Joseph akizungumzia matibabu ya watoto hao nchini India amesema kuwa hatua ya kuwatenganisha imekamilika na mwezi wa 8 mwaka huu watarudi tena nchini India kwa 
ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi ya afya zao.
“Ni kwamba watoto hao wametenganishwa, kwa wakati huu wanaelekea MOI ambako watakaa kwa muda na baadaye wataruhusiwa kwenda kwao Mbeya kujumuika na jamaa zao” amesema.
Kwa upande wake msemaji wa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bw. Nsachris Mwamwaja amesema kuwa watoto hao waliwasili jana jioni na ndege ya shirika la ndege la Oman baada ya kumaliza matibabu ya awamu ya kwanza.
Amesema upasuaji huo mkubwa wa kuwatenganisha watoto hao ulichukua saa 18 na kufafanua  kuwa kati ya hizo  saa 13 zilitumika kutenganisha viungo vilivyoungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo,sehemu ya utumbo mpana,njia ya mkojo,kibofu cha mkojo na sehemu za uume huku saa 5 zikitumika kuunganisha sehemu zilizotenganishwa.
“Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mpaka sasa duniani upasuaji wa aina hii umefanikiwa mara tano  kutenganisha mapacha watoto wa kiume walioungana” amesisitiza.
Ameongeza kuwa matibabu hayo ni juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinatolewa  kwa kila mwananchi kila inapowezekana na kutoa wito kwa jamii kujenga utaratibu wa kuwafikisha mapema kwenye vituo vya afya wale wote wenye matatizo ya kiafya badala ya kuwafikisha pindi hali zao zinapokuwa mbaya.

No comments: