Pages

KAPIPI TV

Thursday, February 13, 2014

WANANCHI WA MANISPAA YA IRINGA WASHAURIWA KUJIUNGA NA TIKA

dkt_a075b.png
Mganga Mkuu Manispaa ya Iringa Dkt. May Alexander 
Na Martha Magessa
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa, Dkt. May Alexander amewaomba wananchi wa Halmashauri hiyo kujiunga katika Mfuko wa Afya wa Tiba kwa Kadi (TIKA) ili kuweza kupata huduma ya matibabu kwa gharama Nafuu katika vituo vya Afya.

Dkt. Alexander amesema, TIKA itasaidia wanachama kuweza kupata matibabu pamoja na dawa kwa gharama ya shilingi 10,000 kwa mwaka kwa kila mmoja.

Ameongeza kuwa, hadi sasa ni wanachama 677 waliojiunga katika mfuko huo, wakiwemo watoto wanaolelewa katika vituo mbalimbali vya Manispaa ya Iringa pamoja na wafanyakazi katika vituo hivyo.

Aidha, amesema Halmashauri imeunda tume ya uamasishaji na kuweza kuifikia jamii kujiunga na TIKA ili kuweza kutanua wigo wa huduma ya afya pamoja na dawa za kutosha katika Manispaa ya Iringa.

Dkt. Alexander amewaahidi wanachama wa TIKA kupata huduma bora na dawa za kutosha katika vituo vya Afya ili kuweza kutofautisha huduma zingine za afya na tiba zinazotolewa kwa bima ndani ya manispaa hiyo.

Hata hivyo, Mganga Mkuu huyo ametoa wito kwa wananchi waishio ndani ya manispaa hiyo kujiunga na TIKA ili kupata huduma ya matibabu na dawa pasipo usumbufu.

No comments: