Pages

KAPIPI TV

Friday, February 21, 2014

BUNGE LA KATIBA LIBORESHE HAKI ZA WATOTO-BAVICHA


Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) limeeleza kufurahishwa na kuwapo kwa ibara ya 43 inayotamka haki za msingi za mtoto na wajibu wa jamii kwa mtoto husika katika rasimu ya pili ya katiba mpya.

“Bavicha inapongeza uwapo wa ibara hii ila ni lazima ifanyiwe maboresho kwa kuwa haijaweza kutamka bayana mtoto ni nani katika taifa hili kwa maana ya umri.

Bila kuweka umri mahsusi utakaomtambulisha mtoto kikatiba ili kumtofautisha na mtu mzima, tutaendelea kuwa na sheria mbovu na kandamizi kama zilizopo sasa, hivyo  kuendelea kuminya ustawi wa watoto nchini.,” alisema Deogratias Munishi, Katibu Mkuu wa Bavicha.

Alisema Bavicha inashauri Wabunge wa Bunge la Katiba kuhakikisha umri wa mtoto unaelezwa bayana ndani ya katiba ili kutoa mwongozo kwa sheria zitakazotungwa baadaye katika kulinda haki za mtoto kikatiba.

“Bavicha inashauri kuwa, kwa kuwa tunakubaliana na dhana ya kijana kuwa ni mtu wa kati ya miaka 18-35, basi ni vyema Katiba Mpya ikazingatia na kutambua kuwa umri wa mtoto unapaswa kuwa miaka kati ya 0-17,” alisema. Kuhusu vijana, alisema rasimu ya pili  imetamka bayana haki na wajibu wa vijana nchini kupitia Ibara ya 44.

Hata hivyo, alisema  kwa kipindi kirefu vijana nchini wamekuwa wakidai  chombo huru kwa ajili ya kusimamia na kuratibu masuala ya vijana yaani Baraza la Vijana la Taifa.

“Kwa kuwa rasimu inabainisha kuwa vijana wana haki na wajibu wa kushiriki shughuli za maendeleo ya Jamhuri ya Muungano na jamii kwa ujumla, Bavicha tunatoa rai kwa wabunge  wa Bunge la Katiba kuboresha ibara hii ya 44 kwa kuongeza kipengele kidogo cha uwapo wa Baraza la Vijana la Taifa la Tanzania kwa ajili ya kusimamia na kuratibu masuala ya vijana nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha haki na wajibu wa vijana unatekelezwa kupitia baraza hilo,” alisema Munishi.

Kuhusu ushiriki na ushirikishwaji wa vijana, Munishi alisema rasimu ya pili imeshusha umri wa mtu kugombea nafasi ya ubunge kutoka miaka 25 hadi 21.

“Bado tunaendelea kutoa rai kwa wabunge wa Bunge la Katiba kutambua kwamba kwa kuwa rasimu ya pili inatoa haki ya kijana wa umri wa miaka 18 kupiga kura ili kumchagua kiongozi na kwamba inaamini kijana huyu ana uwezo wa kusikiliza, kuchambua na kufanya maamuzi ya nani awe kiongozi wake, basi ni muhimu katiba hiyo  ikatoa haki hiyo hiyo kwa mtu wa umri kama huu kuanza kugombea nafasi walau ya ubunge,” alisema.
Kuhusu Muungano, alisema wananchi wametoa maoni yao kwenye Tume na wameonyesha kwamba wanataka kuondokana na kero na manung’uniko.

“Ili kufanya hivyo, wananchi walio wengi kama Tume ya katiba ilivyobainisha wamependekeza na kutaka serikali tatu. Bavicha inaunga mkono pendekezo hili ili kujenga taifa imara lenye misingi ya udugu na mshikamano tofauti na ilivyo sasa ambapo kila upande wa Muungano unalalamika,” alisema Munishi.
 
 

No comments: