Pages

KAPIPI TV

Sunday, December 29, 2013

WATATU WAFARIKI KWA KULA UYOGA - URAMBO

WATU watatu wamefariki dunia baada ya kula uyoga unaodhaniwa kuwa na sumu wilayani Urambo.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dk.Kheri Kagya, watu hao walikuwa nane na walikula ugali kwa mboga aina ya uyoga ambao unadhaniwa kuwa na sumu wakiwa kijijini Igunguli, katika Kata ya Uyogo.

Mmoja wa wazazi katika familia hiyo Makoye Tongele (35) aliamua kuwapeleka Hospitali ya wilaya ya Urambo, watoto Kija Makoye (3) aliyefariki njiani na Wande Mahinge (5) na Mahigi Tongele waliofariki wakipata matibabu katika Hospitali hiyo. 

 
 Dk. Kagya amebainisha kuwa wengine waliokula chakula hicho walisalimika akiwemo Baba wa watoto hao Makoye pamoja na watoto wengine Gimili Makoye(miezi kumi) na Talekwa Mahigi(3) akiwemo pia aliyepika chakula hicho Nyanzobe Mswahili(25).

Dk.Kagya amesema wameshindwa kuchukua sampuli ya chakula hicho kinachohisiwa kuwa na sumu kwa vile kililiwa chote na hata aina ya uyoga wameshindwa kuutambua kwa vile nao ulichumwa wote.

Ameeleza kuwa Nyanzobe aliwaeleza kuwa uyoga aliochuma  porini ulikuwa unafanana na uyoga waliowahi kula na hivyo kukwama kuutambua uyoga huo.

Kamamda wa Polisi Mkoani Tabora,Kamishna Msaidizi wa Polisi Peter Ouma alisema wamepata taarifa za tukio hilo.

No comments: