Pages

KAPIPI TV

Thursday, September 12, 2013

RAIA WA KIGENI WALIA NA OPARESHENI YA KUWAREJESHA MAKWAO

Na Magreth Magosso,Kigoma
 
Jumla ya raia wapatao 90 wa jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Congo waliokuwa wakiishi nchini Tanzania  kinyume na sheria wamekamatwa  katika operesheni  maalumu  ya kuwasaka na kuwarejesha makwao raia wa kigeni walioingia hapa nchini kinyume cha sheria.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma balozi msaidizi,  ubalozi mdogo wa Congo  uliopo  mkoani Kigoma  Bw.Ricky Molema  alisema, raia hao 90, ambapo  baadhi yao 16 wamekwisharudishwa makwao katika mkoa wa Kalemie, Uvira na ng`ambo ya Baraka,huku  tayari  wakiwa  wameandaliwa mazingira ya kuishi huko nchini mwao.
 
Alisema hadi  sasa  kuna  wahamiaji  wapatao 10 watapanda meli gamba ili kuwafikisha maeneo yenye asili yao ikiwa ni hatua ya kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Jakaya Kikwete la kutaka kurejeshwa  makwao  wahamiaji haramu ambao imedaiwa kuwa ndio chanzo cha kuzagaa kwa silaha haramu na uharifu kwa raia wema.
 
Aidha kufuatia zoezi hilo raia wengine wa Congo,Rwanda na Burundi ambao wameshikiliwa katika uwanja wa Lake Tanganyika  mjini Kigoma ambako shughuli ya mahojiano na utambuzi inafanyika,wataendelea kusubiri kurejeshwa makwao.
  
Kwa upande wa wahamiaji hao walidai kuwa  zoezi hilo wanaomba  lifanyike kwa kuzingatia  haki  za binadamu ikiwa ni pamoja na kuonyesha vithibitisho  vya uraia wao  kutokana na  baadhi ya taarifa zinazotolewa na  wananchi za uwepo wa raia wa kigeni zimekuwa zikigubikwa na wimbi la hila za kutaka kuwakomoa raia hao wa kigeni  ambao miongoni mwao wapo wanaoishi kihalali wakiwa na vielelezo muhimu kama vitambulisho vya kupigia kura vya Tanzania,vyeti vya kuzaliwa na uanachama  wa vyama vya siasa hapa nchini.

Walisema  baadhi ya wananchi wanaitumia fursa hiyo vibaya kwa  kuwakandamiza raia wa kigeni wenye uhalali wa kuishi  hapa nchini  ambao wengi wao ni wafanyabiashara hali inayoibua chuki binafsi na huku mianya ya vitendo vya rushwa ikiendelea kudhihiri kwa baadhi ya askari wasio na uzalendo kuwakamata na kuwaingiza kwenye kundi la wahamiaji haramu pasipo hata kutoa vitambulisho vyao na wengine wamenyang`anywa  nyaraka zao muhimu.
 

No comments: