Pages

KAPIPI TV

Tuesday, September 17, 2013

"NGOMA YA MIZIMU YA JADI YA WABISA IPO HATARINI KUPOTEA TABORA?

WABISA


Na Mwandishi wetu Tabora.
 
ZAMANI  wakati nikiwa mdogo nilikuwa nikiambiwa kuwa Wabisa wakati mwingine usiku huwa wanageuka Simba,Jambo hili lilikuwa likinihofisha sana hata kufikia hatua ya kuwaogopa kabisa watu hao ambao kutokana na utamaduni wao hupandisha mizimu wakati wakitekeleza Mira zao hizo za Jadi.

Ingawa nilikuwa nikishuhudia wakifanya shughuli zao katika matukio mbalimbali kama  Matambiko,Harusi na tiba mbalimbali za Jadi,lakini hilo halikuondoa dhana ya mimi kuendelea kuwaogopa kwani watu waliokuwa wakinihadithia kuwa hiyo ni mizimu ambayo hujigeuza kuwa simba walikuwa ni watu wazima na wenye akili zao timamu.

Lakini haikujalisha kwa wale waliokuwa wakithibitisha kuwa mizimu hiyo husaidia kwa kutoa tiba za Jadi kwa kutumia mitishamba na hata kufanya hayo matambiko kwa kupiga na kucheza ngoma kwa zaidi ya mwezi mzima usiku na mchana kwa maana kwamba Mbisa akipandisha mizimu yake huchukua zaidi ya siku 30 bado anakuwa yupo katika hali hiyo pekee huku akiongea Lugha ambayo wanayoielewa wao wenye kushiriki Utamaduni huo wa Wabisa.

Kwa siku za hivi karibuni ngoma hii ya mizimu ya Jadi ya Wabisa  imeanza kuonekana kwa nadra sana ukilinganisha na miaka ya 1985 kurudi nyuma,kwani mbali ya kukutana na mtu ambaye amepandisha hiyo mizimu ya Wabisa,hata  kabla hujamuona lakini unaweza kusikia sauti ya kengele za miguuni ambazo huambatana na vazi rasmi lenye rangi nyekundu lililonakshiwa na rangi nyeusi na nyeupe huku machoni akiwa amejipaka rangi nyeupe kuzunguuka ukingo wa jicho hali inayofanya macho yao kuonekana mekundu kupindukia.

Kama ikiwa ndio mara yako ya  kwanza kukutana nao halafu hujawahi kuwaona wala kusikia habari zao unaweza kukimbia kwakuwa huwa hawasalimii mtu wasiyemjua na mara nyingi wawapo barabarani katika safari zao hutembea mstari mmoja kwa kiongozi mmoja kuwepo mbele na mwingine nyuma kabisa na hakuna kitu kinachosikika zaidi ya kengele za miguuni.

Ni wazi kwamba unaweza kuamini kuwa ni mizimu maana hata kama kuna mtu anafahamiana na mtu huyo aliyepandisha mizimu huwa hawezi kuongea naye zaidi ya kutizama kwa macho makali kabisa mithiri ya mtu anayekusudia kufanya kitu kibaya na cha hatari.

Pamoja na hayo yote lakini Jadi hii ya Wabisa ilikuwa ni sehemu ya utambulisho wa watu hao na kwakweli walikuwa wanapendeza sana hasa wakati ukiwakuta wanafanya mira zao ambazo kwa maana moja ama nyingine zilikuwa zikionesha ustaarabu walionao pamoja na maadili ya kudumu.

Sasa hapa nakusudia kuangalia namna gani hii asili ya utamaduni wa Wabisa inavyoenndelea kutoweka kwa kile ninachobaini kuwa siku hizi siwaoni hata wakiitwa kufanya burudani kwenye harusi au sherehe nyingine yeyote iwe ni ya serikali au vinginevyo.

Lakini pia zamani tulikuwa tukishuhudia hata matambiko yakifanyika mara kwa mara katika kaya mbalimbali na Wabisa wanakuwa ndio wahusika wakuu jambo ambalo sasa halipatikani kabisa sijui ni kwa hii hatua ya kuzagaa kwa utandawazi na pengine watu kujiona kuwa wamestaarabika na hivyo hawaoni umuhimu wa matambiko hayo.

Sikusudii kuhamasisha watu warudie matambiko ambayo kwasasa wameyatelekeza,lakini dhamira yangu ni kutaka kujua nini kimebadirika na hata kufikia hatua ya kuona masuala haya ya Jadi hayana nafasi tena kwetu?

Mtu mmoja ambaye umri wake umekwenda kiasi nilipokuwa nikimuuliza kuhusu jambo hili alinijibu kwamba kila JAMBO NA WAKATI WAKE,wewe jaribu kuangalia tu hata maadili kwa watu yakoje kwasasa,...kisha uangalie matukio mbalimbali yanayojitokeza,...Yaliyo ya maana hayapewi nafasi kwa umuhimu wake na yasiyo ya maana yanakumbatiwa,hii ni dalili tosha kuwa WAKATI UKUTA.

Hapa tena mimi sikuwa na namna ya kuendelea kuuliza  ila ninachosikitikia ni kupotea kwa Mira na Desturi ambazo kumbe ndio chimbuko la Maadili kwa baadhi ya Mira na Desturi hizo.

        

No comments: