Pages

KAPIPI TV

Saturday, August 17, 2013

UTPC YALAANI VITISHO DHIDI YA WANAHABARI.

RAIS wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, amewataka wananchi wote wanaochukizwa na vitendo vinavyowadhalilisha wanahabari nchini kuvilaani, kwani vimekuwa havina nia njema kwa Taifa. Kauli hiyo ameitoa mjini hapa jana, alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara, ambapo alisema kuwa vitendo vya udhalilishaji kwa wanahabari havipaswi kuungwa mkono na jamii.
Alisema kutokana na hali hiyo, kumekuwapo jitihada za makusudi zinazofanywa na baadhi ya wananchi wasiolitakia mema taifa, kwani wamekuwa wakitumia nafasi zao, pesa na hata vyeo ili kuwaangamiza wanahabari.

“Siku zote watu wenye nia njema ndani ya jamii huwa hawapendwi na kikundi cha watu wachache kwa maslahi binafsi, hivyo niwaombe Watanzania wote kuungana kulaani vitendo viovu ambavyo vimekuwa vinalichafua Taifa.

“Sisi kama watu tuliopewa dhamana na wenzetu kuongoza umoja wa vilabu, tutahakikisha kuwa tunapambana na udhalimu huu kwa hali na mali, tukilenga kuihudumia jamii,” alisema Simbaya.

Akizungumza vitendo vya kuwazuia waandishi wa habari kufanya kazi zao na hata wakati mwingine kujeruhiwa na kuuawa, Rais huyo wa UTPC alisema kuwa wamekwishachukua hatua za kuweza kukutana na mamlaka husika ili kuweza kupata ufafanuzi wa jambo hilo.

“Niwasihi waandishi wenzangu kupokea taarifa hii kwa nia njema, kwani kumekuwa na jitihada zilizofanywa na Klabu, hivyo pamoja na kuendelea na jitihada hizo, bado iko sababu kwa waandishi kuacha kubweteka,” alisema na kusisitiza Rais huyo UTPC.

No comments: