Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
amesema alichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kujielewa kwa muda baada ya
kupigwa risasi.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na Mwananchi kwenye wodi binafsi ya Taasisi ya
Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) alikolazwa, Sheikh Ponda alisema
kutokana na hali hiyo hakumbuki matukio yaliyofuata baada ya hapo.
"Sikumbuki
hata nilipata huduma ya kwanza hospitali gani kwa sababu sikuwa katika
hali ya kawaida. Mambo mengine yaliyotendeka kabla ya kujeruhiwa
ninayakumbuka vizuri," alisema Ponda ambaye inasadikiwa kwamba alipigwa
risasi ya begani, Ijumaa iliyopita mjini Morogoro.
Alisema
alihutubia katika Kongamano la Waislamu kwa muda mfupi akizingatia muda
uliokuwa umetolewa kumaliza mkutano huo na baada ya hapo alishuka na
kupanda kwenye gari binafsi ambalo lilizingirwa na polisi ndipo akaamua
kushuka na kuanza kutembea kabla ya kujeruhiwa.
Mahojiano maalumu na Sheikh Ponda.
Swali: Je, watu waliokupa huduma ya kwanza mara baada ya kujeruhiwa walikuta risasi iliyokujeruhi?
Jibu:
Nilipigwa risasi kwa nyuma ikatokea mbele kwa hiyo haikubaki mwilini
wala haikuonekana ilipoangukia kwa wakati huo maana kulikuwa na
purukushani.
Swali: Ulipata wapi huduma ya kwanza?
Jibu: Kwa
kweli kwa sasa siwezi kukumbuka nilihudumiwa wapi kwa sababu mara baada
ya kujeruhiwa sikuwa katika hali yangu ya kawaida, nilichanganyikiwa.
Swali: Utathibitisha vipi kama ulipigwa risasi?
Jibu:
Bahati nzuri ni kwamba tukio hili lilitokea kweupe wapo wengi
walioshuhudia, kwa hiyo wanaweza kusaidia kuthibitisha na ushahidi
mwingine ni jeraha hili.
Swali:
Nini msimamo wako baada ya tukio?
Jibu: Nitaendelea kuzungumzia haki za
Waislamu na siwezi kurudi nyuma. Pamoja na kwamba wananiona mimi ni mtu
mchochezi lakini wanaeneza chuki dhidi yangu kwa njia wanazojua wao.
Nitaendelea, risasi haitaninyamazisha.
Swali: Umehusishwa kufanya uchochezi Zanzibar, unalizungumzia vipi hilo?
Jibu:
Zanzibar nilichozungumza ni kuhusu kesi dhidi ya viongozi wa Kundi la
Uamsho. Watu wamewekwa ndani kwa miezi tisa sasa, kwa mujibu wa sheria
za nchi yetu, kesi wanayoshtakiwa ina dhamana, sasa nikauliza kwa hao
viongozi, kwa nini hawazingatii sheria? Kesi zina muda mrefu hazitolewi
uamuzi, nikawasisitiza wazingatie misingi ya sheria kwa kuwa hivyo
wanavyowatendea wananchi wajue kwamba hawastahili kupewa tena ridhaa ya
kuongoza nchi, nilifikisha ujumbe wangu.
Swali:
Kuna tukio la kumwagiwa tindikali mabinti wawili wa Uingereza
lililotokea Zanzibar, ambalo wewe pia unahusishwa, hili
unalizungumziaje?
Jibu:
Sijaona huo ushahidi ambao wanahangaika kunihusisha na tukio hilo,
nahusishwa vipi? Matukio ya kumwagiwa tindikali yamekuwa yakijitokeza
mara kwa mara huko kabla sijakwenda kuhutubia. Vyombo vya dola vifanye
kazi yake vyema ili kubaini ukweli wa jambo hili.
Pia Mwananchi ilizungumza na mke wake, Sheikh Ponda, Hadija Ahmad ambaye alikuwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa mumewe.
Swali: Unazungumziaje tukio hili la kujeruhiwa kwa mumeo?
Jibu:
Hili ni dhumuni la Serikali, lililenga moja kwa moja kumdhuru ili
kunyamazisha harakati zake za kutetea wanyonge. Ni tukio la kupangwa,
halijatokea bahati mbaya. Serikali inamfuatilia sana hivyo ililenga
kumnyamazisha.
Namshauri
Rais (Jakaya Kikwete), kuhakikisha kwamba haki za wanyonge zinawafikia,
asije akafikiri hili lililotokea kwa Sheikh Ponda ni suluhisho, ni
vyema kufanya mazungumzo ili kuweka mabadiliko.
Alivyowaponyoka polisi
Mtu wa
karibu wa Sheikh Ponda alisimulia jinsi walivyomsafirisha kiongozi huyo
kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na kukwepa vizuizi vya polisi ambao
walikuwa wakiendelea kumsaka.Msafara ulikuwa na magari mawili. Moja
lilitumika kwa uangalizi, lingine lilimbeba Sheikh Ponda.
Tulipofika
Chalinze tulikuta kizuizi tukakikwepa kwa kupitia Msata kisha Bagamoyo
hadi Dar es Salaam na kumfikisha Muhimbili," alisema.
Waigomea polisi
Msemaji
wa familia ya Sheikh huyo, Isihaka Rashid alisema hawaitambui tume
iliyoundwa na polisi kwa kuwa jeshi hilo ndilo linalotuhumiwa.
"Tunachofanya
hivi sasa ni kukusanya ushahidi wetu, kwa bahati nzuri tayari tumepata
mkanda wa tukio lenyewe ambao utatuwezesha kumbaini aliyemshambulia
Sheikh Ponda.
"Hatuwezi
kuhitaji majibu ya hiyo tume yao na hata leo kuna maofisa wa polisi
kutoka Makao Makuu na Kituo cha Kati, Dar es Salaam walifika wakitaka
kumhoji eti kuhusu uchochezi lakini alikataa kuzungumza hadi mwanasheria
wake awepo, wakaondoka," alisema Rashid.
:chanzo mwananchi
No comments:
Post a Comment