Na Allan Ntana, Sikonge.

WATUMISHI wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, wametakiwa kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza tija na ufanisi  katika shughuli zote za kimaendeleo zinazofanyika katika idara zao.

Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu, alipokuwa  akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri  ya wilaya hiyo kilichofanyika mjini Sikonge.

Akizungumza katika kikao hicho, Selengu alisema huu ni wakati wa kila mtumishi kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kufanikisha mpango wa maendeleo ulioidhinishwa katika vikao mbalimbali vya halmashauri hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha kila mradi uliokusudiwa utekelezwe na kufanikishwa.

‘Huu ni wakati wa matokeo makubwa sasa (BIG RESULTS NOW!), hatuhitaji kuendelea kusukumana sukumana  katika utendaji…..kila mmoja anatakiwa kujituma anapotekeleza majukumu yake , hili sio suala la kubembelezana, watumishi  walio wengi wanafanya kazi kwa kusukumwa sukumwa kwanza, nataka kila mtu afanye kazi yake kama inavyopaswa, alisema Selengu.

Aidha, Selengu alisema uzembe unachangia  baadhi ya watendaji wakuu wa  idara kushindwa kusimamia vyema ufanisi wa miradi  ya maendeleo iliyoko chini ya idara zao hali ambayo imekuwa ikisababisha miradi hiyo kuwa na mapungufu kadha wa kadha ikiwemo kutokamilika kwa wakati uliopangwa.

‘Kuanzia sasa tunataka matokeo ya kila kazi inayofanyika yaonekane …..tunataka matokeo makubwa sasa sio kesho!’ alibainisha.

Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama katika wilaya hiyo, Selengu alivitaka vikundi vyote vya sungusungu kushirikiana kwa karibu zaidi na jeshi la polisi ili kudhibiti uharifu na mauaji ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo hususani katika kata ya Kipili.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Shadrack Mhagama, akizungumzia hali ya utendaji, alisema idara zote ambazo zimeonekana kuwa na mapungufu kadha wa kadha, wakuu wake wametakiwa kurekebisha kasoro hizo mara moja kama zilivyoainishwa katika taarifa ya mkaguzi wa hesabu za ndani .

‘Tumebaini mapungufu yaliyopo yanasababishwa na kasoro za kiutendaji katika idara husika, hivyo tukiyafumbia macho yatatuharibia utendaji mzima wa halmashauri na hatimaye kupata hati mbaya kutoka kwa wakaguzi, ni lazima mapungufu haya tuyakomeshe’, alisema Mhagama.

Aidha Mhagama aliongeza kuwa watendaji wote wa idara zenye  mapungufu  watatakiwa kutueleza ni kwa nini mapungufu hayo yamejitokeza katika idara zao na sababu zilizochangia mapungufu hayo.