Pages

KAPIPI TV

Monday, July 8, 2013

MAKAMANDA WA CHADEMA WANAOKABILIWA NA KESI YA UGAIDI WAREJESHWA RUMANDE-TABORA

Makamanda  watano wa  Chadema  wakiingizwa ukumbi wa mahakama  ya  hakimu  mkazi mkoani  Tabora  kufuatia  kesi ya  Ugaidi  inayowakabili akiwemo  kaimu Katibu wa  Chama hicho mkoa wa Dar-es-Salaam  Bw.Henry Kileo aliyeshika Kitabu mkononi. 



Wanachama watano wa chama cha Demokrasia  na Maendeleo-  CHADEMA wanaokabiliwa na mashitaka ya Ugaidi wamerejeshwa tena rumande pasipo maombi  yao kusikilizwa  hadi tarehe  22/07/2013 kesi hiyo  itakapotajwa  tena.

Akitoa  uamuzi  huo  hakimu  mkazi  mfawidhi  wa mahakama  ya  mkoa  wa Tabora Issa  Magoli amesema  kuwa  kwa  vile mahakama yake haina uwezo kisheria kusikiliza shauri hilo kesi hiyo inahairishwa hadi hapo upande  wa utetezi wakiendelea  na taratibu  za  kupeleka  hoja  zao Mahakama  kuu.

Hakimu Magoli kabla ya kuahirisha shauri hilo aliwashauri mawakili wa upande wa utetezi wawasilishe hoja zao mahakama kuu ya Tanzania ndipo watakapoweza kupatiwa ufumbuzi wa kisheria.

Akizungumza nje ya Mahakama,Wakili wa washtakiwa hao,Peter Kibatala,alisema wanafanya utaratibu wa kupeleka shauri lao Mahakama Kuu baada ya kupewa nakala ya uamuzi uliotolewa na mahakama ya hakimu Mkazi Tabora.

Alisema katika maombi yao Mahakama kuu wataomba ipitie shauri hilo na pia kuona kama ni halali kisheria kwa washtakiwa hao kufunguliwa kesi hiyo baada ya awali washtakiwa wanne ukimuondoa Kilewo mashtaka yao kuondolewa na kasha kushtakiwa  tena na Kilewo.

Wakili Kibatala mbali ya kusema ana imani na Mahakama lakini alieleza wana Imani zaidi na mahakama Kuu kwa vile alidai ipo huru
Alisisitiza kama mawakili wa washtakiwa wanapambana kuhakikisha haki inatendeka na kuwaomba wana ndugu na jamaa kuwa watulivu na wawategemee.

“Nawaomba ndugu na jamaa wa washtakiwa kuwa watulivu wakituacha mawakili wao tukipambana katika suala hili na tunawatia moyo msikate tama kwani kesi ni suala la mchakato na linaweza kuchukua muda mrefu”Alisema

Kwa upande wake Mke wa mshtakiwa Henry Kilewo,Joyce Kiria,alisema yeye alipoamua kuolewa na Kilewo alijua ni mwanaharakati lakini kwa vile anampenda alikubali kuolewa naye.

Alisema yupo naye katika kipindi hiki na bado anampenda na kuwatia moyo wanawake kuwa bega na waume zao pale wanapokuwa na matatizo.
“Nataka niwaambie kuwa hii sasa ndio wanawake live ni lazima wanawake tuwe wavumilivu katika kupambana na tusibaki kulia lia”Alisema.

Shauri hilo lilivutia umati wa wapenzi wa CHADEMA waliojitokeza kwa wingi huku ulinzi ukiwa mkali ambapo Askari wa kikosi cha kutuliza Ghasia walitanda wakiwa na silaha.


Watuhumiwa  hao  watano  akiwemo  kaimu  katibu  wa  Chadema  Bw.Henry Kilewo,Evodius Justian,Oscar Kaijage,Seif Kabuta na  Rajabu  Kihawa  wamerejeshwa  rumande hadi hapo  tarehe  22 Julai mwaka  huu kesi  hiyo  itakapotajwa  tena.
 


No comments: