Pages

KAPIPI TV

Monday, March 4, 2013

SERIKALI HAIKUTENDA HAKI KWA REDIO IMANI NA KWA NEEMA!

startimes f28f0
Kitendo cha serikali kuzifungia redio mbili za kidini hapa nchini si kitendo cha kufumbiwa
macho, kwa vile ukichunguza sababu zilizotumiwa kama vigezo vya kuzifungia redio hizo
vimeangalia upande mmoja tu ambao ni upande wa serikali, lakini serikali haikujiangalia
yenyewe kwa upana na marefu kwamba imekuwa sahihi kiasi gani mpaka matatizo ya kuchinja
na sensa kufikia katika kiwango yaliyofika.

Nikianza na tatizo lililosababisha redio Kwa Neema kufungiwa ambalo ni kuhusu redio hiyo
kuwashawishi waumini wa dini ya kikiristo kuchinja kama ambavyo waislamu wanavyochinja;
 
kama ningelikuwa mimi ndiye kiongozi wa serikali ningeliamua kama ifuatavyo: Wakristo miaka yote ya nyuma walikuwa wanakula nyama iliyochinjwa na muislamu, lakini sasa hivi wanaona kwamba kuendelea kula nyama iliyochinjwa na muislamu si haki kwa vile na wao wanadai wana haki ya kuchinja; katika hali kama hii ambayo inagusa imani za kidini ni vigumu na pia hairuhusiwi serikali kutumia nguvu, bali ni swala la kuweka taratibu maalumu ili kila upande uridhike na imani au miiko ya dini isivunjwe kwa kuhakikisha kwamba waislamu na wakristo wanaendelea kuishi kwa amani na upendo kama ndugu kwa kufanya mambo yafuatayo:
 
Hapa nchini tuna mabucha ya nyama ya nguruwe ambayo mabucha haya yapo kila kona ya nchi yetu, na haya mabucha ni kwa ajili ya wakristo tu basi, sasa ni kwanini nyama watakayochinja wakiristo isiuzwe kwenye mabucha haya ya nguruwe; kwa vile mabucha haya kulingana na imani na dini ya kiislamu muislamu haruhusiwi hata kuingia kwenye bucha la nyama ya nguruwe, kwa hivyo nyama ya ngombe itakayochinjwa na wakristo pia iuzwe kwenye mabucha haya, na iwe ni sheria inayoheshimika na kila mtu kwamba bucha la nguruwe pia ndilo tu ambalo linaloruhusiwa kuuza nyama ya ng’ombe aliyochinja mkiristo; na kwenye mabucha haya yaandikwe kwa maandishi makubwa “Bucha la Nyama ya Nguruwe (Ng’ombe)” ili muislamu akiona tu anajua kwamba nguruwe ni haramu na pia nyama ya ng’ombe inayouzwa kwenye bucha hilo ni haramu kwa vile imechinjwa na mkiristo. Hakuna muislamu anayeruhusiwa kuchinja nguruwe, na wala hairuhusiwi kabisa hata kumgusa! 

Kama serikali ingelitumia utaratibu huu sioni kama kungelikuwa na tatizo lolote la waumini kuanza kulumbana na hata kusababisha vifo! Maswala yanayohusu imani za kidini hayatatuliwi kwa nguvu kwa vile tukitumia nguvu tunaendelea kulifanya tatizo kuwa kubwa na hata kuiingiza nchi katika vurugu.

Kuhusu kufungiwa kwa redio Imani kwasababu walijihusisha kuwashawishi waislamu
wasishiriki katika sensa ya mwaka jana (2012); serikali haiko sahihi kuifungia redio hiyo ya wananchi kwa kigezo kama hicho kwa vile hata mimi ungeliniuliza kama madai yao ya kushinikiza kipengere cha udini kiingizwe kwenye takimu za kitaifa zilikuwa za kimsingi au hapana, ningeliwaunga mkono kabisa, tena walifikiri kitaalamu zaidi kulingana na taratibu za sensa kote duniani. Wote tunajua sensa maana yake ni nini? Sensa ni takwimu za kitaifa ambazo 1 hufanyika mara moja tu kwa kila baada ya miaka 10; na kwa vile sensa hufanyika kila baada ya miaka 10; kulingana na uzoefu wa dunia unatuambia kwamba sensa yoyote ile ya nchi yoyote makini ni lazima izingatie mambo muhimu yafuatayo: Idadi ya watu; Jinsia zao; Umri wao;Imani zao za kidini; Elimu zao; Michango yao katika jamii (ameajiriwa au hakuajiriwa); Vipato vyao kwa mwaka; Afya zao (kama wana maradhi yoyote ya kudumu au vilema vya mwili); Mali wanazomiliki wananchi zikiwemo assets na mifugo.

Huu ni utaratibu wa dunia nzima na hii sensa tunayoifanya hapa nchini hatukuibuni sisi bali tumeiga toka nchi zilizoendelea; sasa kama tumeiga kwanini tusiige vitu vyote vizuri? Kwa vile ili upange mipango ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi ni lazima uwe na takwimu ya vipengere vyote nilivyovitaja hapo juu; kuna mipango mingine ya serikali au hata kijamii ambayo inahitaji kujua idadi ya waumini wa dini fulani! Sasa unapokuwa unakibaka kipengere cha imani za kiroho tayari unakuwa bado hujakamilisha utaratibu mzuri wa kuweka takwimu zako sawa kwa maendeleo ya jamii. Na kitendo cha serikali kutokukiweka kipengere hicho kwenye takwimu za kitaifa (sensa) kumeiweka serikali katika mazingira magumu kwa vile ikiulizwa na jumuiya za kimataifa kama vile UN, AU, EAC, World Bank, au IMF kwamba itoe idadi ya Watanzania kulingana na imani zao za kidini, haitaweza kufanya hivyo, bali itaishia tu kupeleka idadi za kukisia kitu ambacho si sahihi na ni makosa kabisa kwa nchi yoyote makini duniani.
 
Ukiangalia hata kwenye riporti za nchi zote za dunia utaona kwamba kila nchi imeonyesha idadi ya wananchi wake na imani zao za kiroho, na wakati mwingine pia huonyesha hata maeneo wanayoishi wananchi kulingana na imani zao za kidini.

Sasa kitendo cha serikali kuifungia redio Imani kwa vile imeshawishi waislamu wasisitize kuwepo kipengere cha udini si sahihi kabisa, kwa vile kipengere hicho cha udini kipo kila sensa ya nchi yoyote ile duniani! Sasa kwanini hapa kwetu kipengere hicho kiondolewe!? 

Hata kama serikali itatumia madaraka na nguvu za dola ilizokuwa nazo kuudhibiti umma, lakini ukweli ni kwamba nchi hii ni nchi ya Waislamu na Wakristo, hivyo hata kama serikali itaficha idadi kamili ya Waislamu na Wakristo ni kwamba inaonyesha udhaifu wake ni jinsi gani ambavyo imeshindwa kulidhibiti tatizo la udini hapa nchini (Weakness on controlling religion fanaticism).

Naiomba serikali ifikirie tena uamuzi wake wa kuzifungia redio za wananchi kwa miezi sita kwa sababu ambazo kama nilivyoelezea hapo juu zimesababishwa na serikali yenyewe. 

Kuzifungia redio za umma kwa miezi sita hasa kwa kipindi hiki ambacho umma unazihitaji sana redio hizi kwa ajili kuhamasishwa kwa sababu za kutoa maoni sahihi juu ya mchakato wa kutafuta katiba mpya itakuwa si sahihi kabisa na kama serikali itasimamia msimamo wake huo itakuwa inakiuka taratibu za utawala bora. Kifungo cha redio kimelenga zaidi KATIBA kuliko Mabucha na Sensa!

Dr. Noordin Jella (Ph.D. in Economics)
Former Lecturer of Mzumbe, Open & KIU – Dar, Universities.
Currently: Freelance Journalist & Seasonal Economical &
Political Analyst
Email: norjella@yahoo.com
Mobile: +255 782 000 131

No comments: