Na Allan Ntana, Urambo
BARAZA
la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Urambo limepitisha bajeti ya
maendeleo kwa mwaka 2013/2014 kiasi cha sh. bilioni 39.9 ambayo imeweka
kipaumbele zaidi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika
bajeti hiyo, halmashauri ya wilaya ya Urambo imepanga kuboresha na
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoanishwa katika idara zake
zote ikiwemo idara ya elimu ya msingi na sekondari, afya, maendeleo ya
jamii, maji, utawala na idara ya ujenzi. Miradi yote itatekelezwa katika
wilaya zote mbili za Urambo na Kaliua.
Baadhi
ya miradi iliyopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni matengenezo ya
barabara na madaraja, ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za waalimu,
mabweni ya wasichana, kuongeza matundu ya vyoo, ujenzi wa zahanati,
vituo vya afya na wodi za watoto.
Miradi
mingine ni kukamilisha ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi mjini Urambo,
kukamilisha ujenzi wa ofisi ya mtendaji kata ya Songambele, jengo la
utawala la wilaya ya Kaliua na nyumba ya mkuu wa wilaya na kuimarisha
utoaji elimu ya huduma za afya ya uzazi, VVU na UKIMWI na stadi za
maisha kwa vijana.
Akizungumza
katika kikao cha baraza hilo wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya
wilaya hiyo kwa mwaka 2013/2014, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
hiyo, Mhandisi Richard Ruyango, alisema kuwa halmashauri imelenga
kukusanya jumla ya sh. 39,909,472,300.00 ambapo kiasi cha sh.
4,189,755,000.00 kitatokana na vyanzo vya mapato ya ndani.
Mhandisi
Ruyango alibainisha kuwa katika bajeti hiyo kiasi cha sh.
25,233,686,300.00 ni ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya mishahara
na matumizi mengineyo na sh.10,073,335,000 ni kwa ajili ya miradi ya
maendeleo inayogharamiwa na fedha toka serikali kuu na kiasi kilichobaki
sh. 412,696,000.00 ni fedha za hisani kutoka kwa mashirika na taasisi
mbalimbali.
Akifafanua makadirio ya kiasi
cha ruzuku kitakachotolewa na serikali kuu na michango mbalimbali
inayotegemewa kutoka kwa wahisani, mhandisi Ruyango alieleza kuwa
wanatarajia kupokea fedha kama ifuatavyo; mishahara sh.22,443,997,300,
matumizi mengineyo sh. 2,789,689,000, miradi ya maendeleo sh.
10,073,335,000, na wafadhiri sh. 412,696,000.
Aidha,
akizungumzia matumizi ya fedha itakayopatikana kutokana na vyanzo vya
mapato yake ya ndani, mhandisi Ruyango alisema kuwa wanatarajia kutumia
mapato hayo kama ifuatavyo; mishahara sh.304,467,200, matumizi mengineyo
sh.1,643,410,400 na miradi ya maendeleo sh. 2,241,877,400.
Aidha
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa bajeti ya mwaka huu imeongezeka kidogo
ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ambapo halmashauri ililenga
kukusanya kiasi cha sh. bilioni 29.3 toka vyanzo vyake vya mapato ya
ndani na ruzuku ya serikali na hadi kufikia mwezi februari mwaka huu
halmashauri iliweza kukusanya jumla ya sh. billion 14.3.
Mhandisi
Ruyango aliongeza kuwa katika bajeti hiyo ya mwaka jana halmashauri
ililenga kutumia kiasi cha sh. bilioni 29.3 kutoka katika makusanyo yake
yote lakini hadi kufikia mwezi februari mwaka huu halmashuri iliweza
kutumia kiasi cha sh. bilioni 10.8 tu ikijumuisha fedha za bajeti
timilizi.
Akizungumzia
jitihada za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, mhandisi Ruyango
alisema kuwa halmashauri hiyo itaendelea kuongeza nguvu zaidi katika
ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vyanzo vyake vya ndani ili kuongeza
ufanisi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika
halmashauiri hiyo.
No comments:
Post a Comment