Mzee mmoja mkazi wa Kitopeni mkoa
wa Kaskazini Unguja Zanzibar Bw. Ali Khamis Ali (65), ameuawa kwa kuchomwa na
kitu chenye ncha kali shingoni na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini
Unguja, ACP Ahmada Khamis, alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa
8.00 mchana huko kwenye eneo la Kitope mashambani.
Alisema Marehemu Mzee Ali ambaye
pia ni imamu wa Msikiti wa Kitope mkoani hapo, alikuwa amekwenda shambani kwake
kukagua mazao yake ikiwemo minazi.
Amesema alipofika shani hapo
aliwaona vijana waliokuwa wakiangua nazi na wengine wakiwa chini ya mnazi wakiziandaa
ili kuondokanazo kwa maana ya kuziiba.
Kamanda Ahmada amesema baada ya
Marehemu kuwabaini wezi hao, inaonekana kuwa alianza kupandana nao lakini walimzidi
nguvu na kumchona na kitu hicho chenye ncha kali ambacho kinaaminika kuwa ni kisu.
Amesema eneo la tukio walikuta
rungu na ala la kisu ninachoaminika kumuulia marehemu. Amesema eneo la tukio hilo
pia kulikuwa na damu nyingi na lilikuwa limevurugwa
kutokana na mapambano.
Kamanda alisema baadhi ya wananchi
wameitambua rungu hiyo kuwa ilikuwa ya marehemu aliyokuwa akiitumia kwa
kulindia mazao yake ambayo mara kwa mara yamekuwa yakiibwa na wezi.
Kamanda Ahmada amesema kuwa pamoja
na marehemu huyo kuuawa lakini inaonekana pia mmoja wa wezi hao wa mazao naye
amejeruhiwa katika mapambano hayo kwani kulionekana michirizi na matone ya damu
ya mtu aliyeondoka eneo la tukio na kutokomea kusikojulikana.
Amesema uchunguzi wa tukio hilo
umeanza na amewataka wananchi kutoa taarifa Polisi endapo watawaona watu ama
mtu mwenye majeraha ili akamatwe kwa kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo Kamanda Ahmada alisema
kuwa mauaji hayo ni ya kuwania mali na ametaka kutohusishwa na hisia za imani yoyote
ama za kisiasa, kishirikina, wivu wa kimapenzi, kulipiza kisasi ama imani za kidini.
“Haya ni mauaji ya kawaida na
hayana hisia zozote. Ni mauaji kama mauaji mengine yanayotokea katika maeneo
mengine ya nchi yetu.” Alisema Kamanda Ahmada na kuwaonya wananchi kutoweka
hisia tofauti na tukio lenyewe.
Amewaomba pia Waandishi wa Habari
kutowema maoni yao binafsi wanaporipoti taarifa za tukio hilo ili kuepuka kuwatia
hofu wananchi.
No comments:
Post a Comment