Pages

KAPIPI TV

Wednesday, December 26, 2012

WAKRISTO WAHOFIA VURUGU ZA KIDINI, MAASKOFU WAITAKA SERIKALI KUCHUKUA HATUA DHIDI YA VIKUNDI HALIFU VYA KISIASA AU KIDINI,

Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.


GAZETI LA MTANZANIA DEC 26/ 2012.
JUKWAA la Wakristo Tanzania (TCF) limeitaka Serikali na vyombo vya Usalama kuchukua hatua za haraka kwa vikundi halifu vya kisiasa au kidini, vinavyochochea uvunjifu wa amani na sheria nchini.

Jukwaa hilo, ambalo linajumuisha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventisti Wasabato (SDA).

Jukwaa hilo, limesema tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea, bila hatua madhubuti kuchukuliwa ni udhaifu mkubwa unaoonyeshwa na Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, wakati wa kutoa tamko rasmi la Jukwaa hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Peter Kitula, alisema umoja huo unasikitishwa na vitendo viovu, ambavyo vimekuwa vikijitokeza kila kukicha.

Askofu Kitula ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Afrika Inland Church Tanzania, katika mkutano wa nne wa TCF, wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa uhusiano wa dini mbili za Kikristo na Uislamu.

“Katika mkutano wa nne wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tulitafakari kwa undani kuzorota kwa uhusiano baina ya dini zetu za Kikristo na Kiislamu na kutathmini wajibu wa kanisa na utume wake wa kinabii kwa taifa,” alisema Askofu Kitula.

Alisema kutokana na muono wao, kwa kauli moja walitaka lianzishwe baraza mahsusi ambalo litakuwa huru lisilo egemea chama chochote cha kisiasa wala dini, likiwa na dhumuni kuu la kulinda na kuiongoza Serikali.

“Baraza hili, litasaidia kuiongoza Serikali dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali maslahi ya wote ambayo hayatapotoshwa, liwe na uwezo wa kuvichunguza vyombo vya sheria na usalama, itakapotokea matatizo makubwa yanayoashiria uvunjifu wa haki na kuteteresha usalama wa nchi,” alisema Askofu Kitula.

Alisema viongozi wa dini zote za Kikristo, Kiislamu, Kihindu na nyinginezo, wawafundishe waumini wao katika mienendo mema, hasa vijana ili kuwajengea uelewa na utashi wa kuvumiliana kwa upendo.

Alisema kuna masuala ambayo yanatakiwa kufafanuliwa na kudhibitiwa na dola mapema, ili yasiendelee kupotoshwa.

Alisema ni dhana potofu, kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo.

Alisema maneno hayo ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waumini wenye imani kali na waliojiandaa kwa mapambano maovu kutetea dhana potofu na kinzani kwa misingi ya demokrasia na haki za binadamu, kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa.

“Pia ukiangalia kwa upande wa Zanzibar, asilimia 100 vingozi wa ngazi ya juu Serikalini ni Waislamu na sio kweli, Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza, hata viongozi wa tume ya mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu.

“Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala wa kisheria na si vinginevyo, hii ni mfano midogo tunayo mingine mingi iliyowazi,” alisema Askofu Kitula.

Alisema katika mikataba ya kumbukumbu, ‘memorandam of Understanding’ ya mwaka 1992, ambayo ilikuwa kwa ajili ya huduma za kijamii ambazo zinaendeshwa na makanisa nchini kote.

“Makubaliano hayo, yalilenga kutolewa kwa huduma za kijamii zitolewe na makanisa kwa Watanzania wote, ikiwa pamoja na huduma za hospitali, vituo vya afya, zahanati na shule mbalimbali zinazoendeshwa na makanisa nchini kote.

“Ni vema Watanzania wakaelewa makubaliano haya, yalikuwa kati ya makanisa ya Tanzania na makanisa ya nchini Ujerumani, ambapo Serikali ya Tanzania ilihusishwa kwa vile raia wake wangenufaishwa na misaada hii.

“Jukwaa la Wakristo Tanzania, tunaitaka Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya makubaliano hayo, ili Watanzania waelewe maana, makusudi na manufaa kwa wananchi wote…


Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi,” alisema Askofu Kidula.


GAZETI LA MWANANCHI. DEC 26/ 2012.
Maaskofu nchini watoa tamko zito.


Kwa ufupi
“Ukimya huu wa Serikali wakati kanisa linakashfiwa unatoa taswira kwa viongozi wa makanisa kuwa Serikali inaunga mkono chokochoko hizi…Kimsingi, unaponyamaza, maana yake unaunga mkono.”“Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivihivi inaashiria hatari kubwa ya kiuhusiano siku za usoni, Tunaitaka Serikali ichukue jukumu lake la msingi la kusimamia amani.”

MAASKOFU nchini, jana walitumia ibada za Krismasi kukemea maovu, huku baadhi yao wakiwatuhumu matajiri nchini kuwa ndiyo kiini cha vurugu zilizosababisha kuchomwa kwa makanisa yao hivi karibuni.


Wakihubiri kwa nyakati na makanisa tofauti, viongozi hao walisema uhasama huo dhidi ya Wakristo ulioanza kujengeka katika siku za hivi karibuni, unafadhiliwa na baadhi ya matajiri kwa masilahi yao binafsi.

Katika tamko lao lililotolewa na Umoja na Makanisa Tanzania, maaskofu hao wameitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya mbegu za chuki zinazopandikizwa ili kuwafarakanisha Watanzania kwa misingi ya imani za dini.

Tamko hilo ambalo litarejewa Desemba 30, mwaka huu, ni makubaliano ya pamoja kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Moravian, Anglikana, Pentekoste, Wasabato na Kanisa Katoliki.

Askofu Dk Martin Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini akisoma tamko hilo wakati wa ibada ya pamoja, alidai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vya kidini, vinawachochea watu ili wawaue maaskofu na wachungaji mbalimbali wa makanisa.


Pia, alihoji kauli zinazoenezwa kuwa nchi hivi sasa inaongozwa kwa mfumo wa Kikristo ilihali asilimia 90 ya viongozi wa juu nchini ni Waislamu.

“Labda niwakumbushe, viongozi wote waandamizi wa ngazi za juu nchini, asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi iendeshwe kwa mfumo wa Kikristo?” alihoji Askofu Shao.


Aliwataja kuwa ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

“Kule Zanzibar, asilimia 100 ya viongozi wote ni Waislamu na si kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa ya kuongoza,” alisema na kuongeza:


“Hata uwakilishi kwenye Tume kama ya kuandikwa kwa Katiba Mpya, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu…

Nchi hii haina mfumo wa Kikristo, bali ni nchi yenye mfumo wa kidemokrasia.”


Aliitaka Serikali ithibitishe ukweli kuwa haiendeshwi kwa mfumo wa Kikristo badala ya kukaa kimya wakati maneno hayo ya uchochezi yanaenezwa hadharani.


“Ni wakati wa kukubali kuwa misingi ya haki, amani na upendo katika taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Kumekuwapo na dalili za wazi za uchochezi na kashfa dhidi ya Ukristo,” alidai.

Maaskofu hao wamewalaumu baadhi ya viongozi wa dini kutumia vyombo vya habari vya kidini, vipeperushi, mihadhara na kanda za video kukashfu dini nyingine.


“Ukimya huu wa Serikali wakati kanisa linakashfiwa unatoa taswira kwa viongozi wa makanisa kuwa Serikali inaunga mkono chokochoko hizi…Kimsingi, unaponyamaza, maana yake unaunga mkono.

”“Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivihivi inaashiria hatari kubwa ya kiuhusiano siku za usoni. 


Tunaitaka Serikali ichukue jukumu lake la msingi la kusimamia amani.”

Askofu Pengo.
Katika mahubiri yake jana, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo aliwaponda matajiri wanaojivunia mali, akisema siyo kigezo cha mtu kuwa na furaha maishani.


Kadinali Pengo alisema hayo katika misa ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika juzi katika Parokia mpya ya Mongolandege, Ukonga, Dar es Salaam.

Alisema ni makosa mtu kuhesabu mali kama sehemu ya mafanikio katika maisha kwani kuna wenye mali nyingi ambao hawana furaha.


“Utajiri unaambatana na shaka, hofu na wasiwasi kwa kufikiri kuwa huenda mali hii isinitoshe au itachukuliwa na watu wengine,” alisema Kadinali Pengo na kuongeza.

“Tusitafute mali kiasi cha kuwafanya watu wengine waumie, wahuzunike.

Kila mmoja atimize wajibu wake pale alipo, matokeo yake ndiyo yatakayoleta furaha.”

Askofu Mhongolo.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati, Godfrey Mhogolo amewataka waumini kuendelea kuienzi Krismasi kwa kujali na kuwekeza katika elimu ambayo ni msingi wa mambo yote.


Kiongozi huyo alisema kwa Wakristo, kuwa na dhana ya kujenga elimu katika maisha yao itawasaidia kujiletea heshima na kwamba watakuwa juu.


Askofu huyo alisema dhana nzuri ya kuthamini elimu hadi sasa waumini wa Kikristo nchini wamekuwa ni mfano wa kuigwa na jamii na taifa kwani kati ya jumla ya vyuo vikuu 19 vilivyoko nchini vyuo saba vinamilikiwa na Wakristo, 11 na Serikali huku kimoja kikiwa cha Kiislamu.

Askofu Mkude.
Askofu Thelesphory Mkude wa Jimbo la Morogoro amewataka waumini wa dini zote kushiriki vyema katika kuendeleza na kushika neno la Mungu na kuombea nchi hasa katika kipindi hiki cha kufunga mwaka na kukaribisha Mwaka Mpya.

Katika ibada ya mkesha wa Krismasi, Askofu Mkude alisema kuwa imefikia wakati sasa wa kumshirikisha Mungu kila jambo kwani kila siku matendo maovu yanaendelea kutokea na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Askofu Sehaba.
Askofu wa Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Sehaba ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka pale inapoona kuna tishio la uvunjivu wa amani nchini kuliko kukaa kimya na kusubiri likitokea ndipo ianze taratibu za kudhibiti.

Alisema kumekuwapo na vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baadhi ya waumini wa dini kama uchomaji wa makanisa na kusema Serikali inapaswa kutovifumbia macho.

Askofu Mwombeki.
Askofu Edson Mwombeki wa Kanisa la Free Evangelism Tanzania amewataka Watanzania wote kulinda amani na utulivu.


Akihubiri kwenye ibada ya Krismasi iliyofanyika katika Manispaa ya Shinyanga, aliwaomba Watanzania wote wabadilike na kuwa na tabia njema kwani kwa sasa watu wengi wamepoteza uadilifu, amani na uzalendo.

No comments: