RAIS Jakaya Kikwete
amesema ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa ambayo itafanana na
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), utaanza Januari, 2013 katika eneo la
Mloganzila, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Ujenzi huo wa hospitali hiyo unatokana
na mkopo wa Dola za Marekani 60,000 milioni sawa na Sh96 bilioni ambazo
Tanzania imepata kutoka Korea ya Kusini.Kikwete alisema hayo jana wakati
akifungua majengo matatu ya hospitali za Mnazimmoja (Ilala), Sinza
(Kinondoni) na Mbagala Rangitatu (Temeke).
Ujenzi wa majengo ya hospitali hizo
yenye maabara za kisasa, vifaatiba na magari ya wagonjwa yamefadhiliwa
na Korea Kusini kwa gharama ya Sh6.7 bilioni.
Alisema Hospitali ya Mlonganzila itakuwa
ikitoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi na kwamba kila mwaka itakuwa
ikifundisha madaktari 12,000 kuanzia itakapokamilika Januari 2015.
“Chuo Kikuu cha Muhimbili kinatoa
madaktari 5,000, Dodoma wanatoa madaktari 5,000, Mloganzila wakitoa
12,000 tutakuwa na madaktari 22,000 kwa mwaka,” alisema Kikwete.
Alisema ujenzi wa hospitali hiyo utasaidia kumaliza tatizo la madaktari linaloendelea kuwepo hapa nchini.
“Madaktari waliopo ni wachache wanazunguka kutoa huduma katika hospitali zaidi ya mbili kwa siku,” alisema.
Akitoa takwimu, Kikwete alisema nchi
zilizoendelea daktari mmoja anahudumia wagonjwa 500 wakati Tanzania
daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
“Bado tuko mbali sana tunahitaji kukimbia wakati wenzetu wanatembea, tunapofikiria kujenga zaidi hospitali tunatakiwa tuendelee kusomesha ili kupata madaktari,” alisema Kikwete.
Akizungumzia hospitali za kisasa alizozifungua, Kikwete aliishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa msaada huo na kutaka Halmashauri za Kinondoni, Ilala na Temeke kutenga fedha za kutosha kila mwaka ili kuvifanyia matengezo vifaa hivyo.
Alisema Serikali inaendelea na juhudi zake katika kuhakikisha kwamba huduma za afya zinafika jirani na wananchi.
Balozi wa Korea nchini, Chung II alisema
, Serikali yake inathamini umuhimu wa afya katika juhudi za Tanzania
katika kujiletea maendeleo.
Alisema wananchi wanapopata huduma za afya za uhakika huwasaidia kushiriki katika kazi mbalimbali na hivyo kujiimarisha kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Meck Sadiki alimwomba Kikwete kutenga Sh1.2 bilioni kwa
ajili ya kuwafidia wananchi wa Mbagala Rangi tatu ili kupisha upanuzi wa
hospitali hiyo.
“ Licha ya hospitali hii ya kisasa
kujengwa na Wakorea bado imezungukwa kwa karibu na nyumba za watu,
tunaomba fedha ili tuweze kuwalipa fidia wananchi hawa waweze kupisha
upanuzi zaidi,” alisema Sadiki.
No comments:
Post a Comment