Pages

KAPIPI TV

Wednesday, December 12, 2012

IRINGA WASHINDWA KUPATA SENENE LEO ALFAJIRI

Baadhi ya  wananchi  wa Manispaa ya Iringa  leo  wameamka asubuhi na mapema kwenda maeneo mbali mbali ambayo usiku wa  kuamkia jana senene  wengi  zaidi  walianguka.

Licha ya wananchi hao kuchukua jitihada kadhaa za kusaka kitoweo hicho kinachopatikana mara moja kwa mwaka, leo hii wamejikuta wakiambulia patupu kufuatia kukosekana kwa wingi kwa wadudu hao hali iliyosababishwa na ukosefu wa miundo mbinu ya taa ambayo ni kivutio kikubwa cha wadudu hao.

Imeelezwa kuwa baadhi ya  wamiliki  wa nyumba  zinazowasha  taa usiku kwa ajili ya ulinzi binafsi wa nyumba hizo katika manispaa ya Iringa hawakuwa  wamewasha taa na hivyo kusababisha wadudu hao kushindwa kufika na kutokuwa rahisi kwa wananchi kuwapata.

Uchunguzi  wa mtandao  huu umebaini hali hiyo baada ya  kuzunguukia maeneo mbali mbali maarufu ambayo jana  Senene  walianguka na  kusababisha  kuwepo kwa msongamano mkubwa  wa  wananchi  ambao  walifika  kukusanya  senene hao.


Baadhi ya  watu  waliokutwa katika  jengo la Asas eneo la Ngangilonga kwenye barabara  kuu ya Iringa - Dodoma  walisema  kuwa  walilazimika  kufika mapema  eneo  hilo ili  kuokota  senene  ila cha kushangaza  baada ya  kufika hao walishuhudia  giza nene na hakuna  senene wanaoanguka  hapo hali  iliyowakosesha  kitoweo hicho.


Zaidi ya  watu 20  waliokutwa hapo asubuhi  majira ya saa 11;30 asubuhi ya  leo  walikuwa na mifuko  mikubwa ya naironi kwa ajili ya  kukusanya  senene na  kwenda  kuwauza na  baadhi yao  kusaka  kitoweo hicho.


Pamoja na jengo  hilo la Asas kukosa  mwanga na kuwa  giza  kiasi cha  senene  kushindwa  kuanguka bado maeneo mbali mbali ya uhindini ambayo jana  senene  wengi  zaidi  walianguka  leo hali  imekuwa  tofauti zaidi baada ya  senene kutoanguka kwa  wingi.


Hata  hivyo baadhi ya  walinzi  wanaolinda katika  eneo hilo la Asas na maeneo mengine ambayo jana yaliongoza kwa  kuanguka  senene wengi  zaidi wamedai kuwa  wenye nyumba hizo  waliamua kuzima  taa ili  kuepusha uchafu  wa kuta  zao na maeneo yao  kama  ilivyojitokeza jana .

No comments: