Pages

KAPIPI TV

Friday, November 9, 2012

WATATU WAMEUAWA KIKATILI,SMG YAHIFADHIWA KABURINI -TABORA

Na Mwandishi wetu-Tabora

Watu watatu wameuawa kikatili na wananchi wanaodaiwa kujichukulia sheria mkononi  baada ya  kuwahisia kuwa ni  wizi wa mifugo  huko katika kijiji cha Ishihimulwa kitongoji cha Bwera wilayani uyui mkoani  Tabora.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora ACP Anthony Rutha amewataja watu hao waliofanyiwa mauaji hayo ya kinyama kuwa ni Busanda Mkola(32),Bundala Mayunga(49) na John Mayunga(48)

Kamanda Rutha alisema mnamo tarehe 8 Novemba mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ishihimulwa wakiongozwa na mwenyekiti wa Kitongoji cha Bwera John Busanda walivamia nyumbani kwa Bundala Mayunga wakimtuhumu alikuwa ameleta waharifu wawili ambao walikuwa ni wageni wake na kuanza kuwashambulia kwa maneno pasipo kuwapa nafasi ya kujieleza.

Katika vuta nikuvute hiyo Mwenyekiti na wafuasi wake hao ambao tayari walikuwa wamejitayarisha kwa kubeba silaha za aina mbalimbali yakiwemo marungu na mapanga,waliwachukua watu hao watatu waliokuwa wakiwatuhumu kuwa ni wizi wa mifugo na kuwapeleka porini ambako waliwashambulia kwa kipigo pamoja na kuwachoma moto hatua ambayo ilisababisha kifo chao

Kufuatia  mauaji hayo ya kikatili kamanda Rutha ameapa  kuwasaka vikali wahusika baada ya kumkamata  mwenyekiti  wa kitongoji cha Bwera  John Busanda  huku  baadhi  ya wanaume wa vijiji vya Ishihimulwa na Bwera wakiwa wametelekeza  familia zao na kukimbilia kusikojulikana.

Aidha katika hatua nyingine Jeshi la Polisi mkoani Tabora limefanikiwa kukamata  bunduki aina ya SMG yenye nambari za usajiri 0J2208 iliyokuwa  imechimbiwa  katika moja ya makaburi huko  shule ya msingi Rufita hapa manispaa ya Tabora.

Rutha alisema kupatikana kwa silaha hiyo imetokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa raia mwema mmoja ambaye akiwa nyumbani kwake jirani na makaburi ya Rufita huko maeneo ya Mwanza road manispaa ya Tabora,(jina limehifadhiwa)aliwaona watu usiku wakija makaburini hapo na kuchagua moja ya kaburi na kuanza kuchimbia kitu kilichofungwa kwenye mfuko wa sandarusi hatua ambayo ilimtia shaka na kuamua kutoa taarifa polisi.

Makachero wa Jeshi la polisi kwa kushirikiana na baadhi ya raia wa eneo hilo walichimbua bunduki hiyo huku ikielezwa licha ya kuwa ilikuwa nzima na inafanya kazi mara kwa mara lakini haikuwa na risasi hata moja. 

No comments: