Na Juma Kapipi Tabora
Jeshi la Polisi mkoani Tabora
linawashikilia watu watatu akiwemo mganga wa kienyeji kwa tuhuma za
kufanya jaribio la kumtolea ujauzito na kusababisha kifo chake
mwanafunzi wa Chuo cha biashara CBE Dodoma kilichotokea mkoani Tabora.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Anthony Rutha amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo mnamo tarehe 6 Novemba 2012 majira ya saa 12 na dakika 57
jioni baada ya mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Jesca Rafael
kufikishwa katika Hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete akiwa mahututi
kutokana na jaribio hilo la kutolewa ujauzito ambapo muda mfupi baadae
alifariki dunia.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake
kamanda Rutha alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu Jesca
ambaye ni mwanafunzi wa CBE Dodoma alikuja Tabora akiwa na Martin
John(24)ambaye ni mwanafunzi mwenzake waliokuwa wakiishi wote Dodoma
wakiwa wamepanga chumba kimoja kama wapenzi na hata kufikia hatua ya
marehemu kupata ujauzito hali iliyosababisha kutafuta namna ya kuutoa
ujauzito huo.
KUTAFUTWA KWA MAREHEMU HUKO DODOMA
Baada
ya wazazi kukosa mawasiliano baina yao na marehemu Jesca waliamua
kumtafuta chuoni CBE Dodoma ndipo wakagundua binti yao hakuwepo
chuoni,wakaamua kutoa taarifa Polisi Dodoma na uchunguzi wa kina ulianza
ikiwemo kuhoji baadhi ya wanachuo ambao walikuwa wakiishi na kuwa na
ukaribu na marehemu.
Aidha katika mahojiano na Polisi
ilibainika kuwa marehemu Jesca alikuwa mjamzito aliopewa na Martin John
na kwamba mnamo tarehe 4/10/2012 wanachuo hao walipanda basi kuja Tabora
kwa dada yake na Martin kutafuta mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa
jina la Mahadhi Razaro(40) kwa ajili ya kutekeleza kwa siri zoezi la
kuutoa ujauzito huo.
TABORA.
Siku chache mara baada
ya kufika Tabora na kupata ufumbuzi wa adha hiyo iliyokuwa ikiwakabili
wanachuo hao wawili, jaribio la utoaji ujauzito lililongozwa na mganga
huyo wa kienyeji ambaye ni mwenyeji wa Kigoma kwa kusimamiwa na Martini
John na dada yake Ritha John ambaye ndiye mwenyeji wao,majira ya saa
kumi na mbili jioni marehemu Jesca alizidiwa na kulazimika kupelekwa
Hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete ambapo walimkuta muuguzi wa zamu
aitwaye Charles Christopher(37).
MAELEZO YA MUUGUZI.
Kwa
mujibu wa maelezo ya muuguzi huyo Charles Christopher,marehemu aliletwa
hospitalini hapo na wanaume wawili na mwanamke mmoja akiwa mahututi
ambapo waliandikisha jina la mgonjwa Prisca Rwakatare badala ya Jesca
Raphael huku dada wa Martini John akijitambulisha kwa jina la Maria
Rwakatare kama msimamizi wa mgonjwa huyo waliyemleta.
Muuguzi
huyo wakati akiendelea kumpima mgonjwa aligundua kuwa tayari alikuwa
amekwisha poteza maisha na alipotoka nje kuwaangalia waliomleta yaani
Ritha,Martin na Mganga huyo wa kienyeji maarufu Dr.Mahadhi tayari
walikwisha toweka na kumtelekeza waliyemleta ambaye kwa wakati huo sasa
alikuwa amekwisha fariki dunia.
Hata hivyo baada ya mwili
wa marehemu kukosa ndugu wa kuuchukua ulilazimika kuhifadhiwa katika
chumba cha maiti hospitalini hapo na baadaye idara ya afya halmashauri
ya manispaa ya Tabora kwa kushirikiana na hospitali ya mkoa wa Tabora
Kitete waliamua kufanya mazishi.
Kwaupande wa jeshi la
Polisi kwa kushirikiana na baba wa marehemu Jesca kwa kibali cha
mahakama,mwili wa Jesca ulifukuliwa na kurudishwa tena chumba cha
kuhifadhia maiti cha hospitali ya Kitete kwa ajili ya uchunguzi wa kina
na kubaini waliohusika na tukio hilo Martini John,Ritha John na huyo
mganga wa kienyeji Mahadhi Razaro ambao kwa sasa wanashiliwa na Polisi.
No comments:
Post a Comment