Pages

KAPIPI TV

Thursday, November 1, 2012

SIKONGE YAPUNGUZA KIWANGO CHA UTUMIKISHWAJI WATOTO MASHAMBANI

Na Hastin Liumba,Sikonge
 
HALI ya utumikishwaji watoto katika mashamba na kazi mbalimbali majumbani wilayanim Sikonge,mkoani Tabora ,umepungua kutoka asilimia 90, hadi kufikia asilimia 60.
 
Hayo yalisemwa na Ezekiel Basisi kwenye taarifa ya shirika lisilo la kiserikali la PROSPER kwenye hafla iliyofanyika katika vijiji vya Udongo na Makazi kata ya Ipole wilayani Sikonge.
 
Basisi alisema kushuka kwa kiwango hicho kunatokana na hamasa na ushirikiano uliopo kati ya shirika la PROSPER,wadau na Halmashauri ya wilaya ya Sikonge.
 
Aidha aliongeza kuwa licha ya kutoa elimu juu ya kuachwa kutumikishwa watoto mashambani na kazi mbalimbali majumbani,pia shirika la PROSPER limekuwa likishirikiana na halmashauri ya wilaya Sikonge kutoa elimu ya mafunzo ya kijasiliamali kwa vijana chini ya miaka 15 na 17.
 
Alisema mafunzo hayo yameanza toka mwezi julai 2012,yakiwemo mafunzo ya kilimo cha bustani ambapo vijana 40 tayari wamepata mafunzo katika vijiji vya Udongo na Makazi.
 
Naye mratibu wa mradi wa PROSPER katika wilaya ya Sikonge Jesca Maiko Kibiki alisema shirika hilo limefanikiwa kutoa mikopo kwa vikundi 10 vya kinamama mkopo wenye jumla ya sh 43.5 kwa ajili kuendesha biashara ndogo ndogo kwa wilaya ya Sikonge.
 
Kibiki aliongeza kuwa shirika hilo pia limefadhili vifaa vya shule na gharama nyinginezo kwa watoto 300 wilayani Sikonge vyenye thamani y ash milioni 15.
 
Aidha alisema elimu hiyo ya kijasiliamali imetolewa kwa wakazi wa vijiji vya Udongo,Makazi,Usesura,Mole,Mkolye,Tumbili,Kidete,Usanganya,Ukondamoyo, na Mitwigu.
 
Alisema watoto,vijana na kinamama walionufaika na ufadhili huo,wote wametoka kwenye vijiji hivyo.
 
Hata hivyo mratibu huyo alitaja changamoto zilizopo katika kutekeleza miradi hiyo kuwa ni jamii kutokuwa na uelewa athari za utumikishwaji watoto mashambani na majumbani.
 
Mratibu wa miradi ya PROSPER,Christopher Luyenga alisema madhumuni ya hafla hiyo ni kuijengea uwezo jamii na taasisi zake ili zipambane na ajira mbaya kwa watoto,ikiwa ni pamoja na kuihamasisha jamii kulima tumbaku bila kutumikisha watoto.

No comments: