Mke
wa mwandishi mkongwe wa habari nchini marehemu, Aidan
Libenaga (64), Elizaberth Libenanga (59) katikati akifarijiwa na
waombolezaji nyumbani kwake mtaa wa Sabasaba wakati wa kifo cha mume
wake aliyefariki dunia hafla majira ya saa 1:00 asubuhi ya leo kwa ugonjwa wa shinikizo la damu (pressure) katika hospitali ya mkoa wa Morogoro mjini hapa.
Na Venance
George, Morogoro.
MWANDISHI
mwandamizi na ambaye amewahi kufanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari
ikiwa ni pamoja na shirika la habari Tanzania (SHIHATA), Aidan Libenanga,
amefariki dunia jana.
Kwa mujibu wa
mtoto wa marehemu huyo, Ramadhani Libenanga, marehemu alifariki dunia baada ya
kufikishwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro majira ya saa 1.00 asubuhi ya
jana akiwa anasubuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu (pressure).
Alisema kabla ya
kufikwa na umauti huo, mzee Libenanga kama jinsi ambavyo wanahabari wenzake
walivyozoea kumwiti aliamka alfajiri majira ya saa 11.30 nyumbani kwake katika
kata ya Sabasaba kwa ajili kufua nguo zake
lakini baada ya kuingia bafuni alidodoka chini na kulazimika kukimbizwa
hospitali.
“Baba huwa anapenda
kufua nguo zake mwenyewe, sasa na asubuhi hiyo aliamka kufua nguo hizo lakini
alipoingia bafuni ghafla alidondoka na tukampeleka hospitali ya mkoa kwa
matibabu,” alisema Libenanga.
Alisema kuwa cha
kusikitisha sana baada ya kufika hospitalini hapo huduma za matibabu kwa baba
yake zilichelewa kutokana na kuwepo kwa wagonjwa wa ajali ya barabarani
waliofikishwa hospitalini hapo muda huo na hivyo kusababusha mwandishi huyo
mkongwe kupoteza maisha akiwa katika harakati za kupatiwa matibabu.
Kuhusu wasifu
wake mzee Libenanga alizaliwa katika kijiji cha Libenanga tarafa ya Mwaya,
wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na alipata elimu yake katika shule ya msingi
Mwaya kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana ya Kwiro iliyoko mji
wa Mahenge wilayani humo.
Baada ya
kuhitimu elimu hiyo, mzee libenanga alichaguliwa kujiunga na sekondari ya
Mzumbe kwa kidato cha tano na sita na hatimaye kuajiliwa kama mtumishi wa
shirika la posta na simu nchini.
Mwaka 1975, mzee
Libenanga alikuwa miongoni mwa waandishi wachache waliochaguwa na chama na
serikali kwenda kusomea taaluma ya uandishi wa habari ambapo alikwenda nchini
Yugoslavia na kufaulu kwa ngazi astashahada (certificate) na stashahada
(diploma) ya uandishi wa habari.
Marehemu
aliajiriwa na serikali katika shirika la habari Tanzania kama mkuu wa habari
(Bureau chief) katika mikoa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Iringa, Kigoma,
Shinyanga, Rukwa na Morogoro na baada ya kustaafu kazi alibaki kuwa mwandishi
wa kujutegemea akifanya kazi na vyombo mbalimbali vya habari hususan magazeti.
Mungu ailaze
mahali pema peponi roho ya marehemu, Aidan Libenanga, Amina.
Marehemu ameacha
mjane, watoto 10 na wajukuu 10.
No comments:
Post a Comment