Serikali
imetakiwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali kwa
kushirikiana na taasisi za hapa nchini katika kupiga vita utumikishwaji
wa watoto katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwani hali hii
inawakandamiza watoto ikiwa ni pamoja na kuwanyima haki zao za msingi za
kielimu.
Hayo
yalibainishwa na wadau mbalimbali waliohudhuria katika mkutano wa siku
moja uliofanyika juzi katika ukumbi wa White Sands Hotel ulioko Kunduchi
jijini Dar es salaam, ambapo wadau hao kwa kauli moja waliitaka
serikali kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na wadau hao ili
kuhakikisha suala zima la utumikishwaji wa watoto katika ajira mbaya
linatokomezwa.
Mkutano huo wa pili wa kitaifa ulioandaliwa na taasisi ya PROSPER ulilenga kuwakutanisha wajumbe
wote wa kamati ya ushauri ya taasisi hiyo (Prosper National Advisory
Committee) na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na watendaji kutoka
serikalini ili kuzungumzia mikakati ya namna ya kupambana na kuzuia
utumikishwaji wa watoto katika ajira mbaya hasa kwa wakulima wa zao la
tumbaku.
Akitoa taarifa katika
mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa mradi wa PROSPER Bw. Bahati Nzunda
alisema kuwa mkutano huu ni mahsusi kwa ajili ya kuzungumzia mapana ya
tatizo hili la ajira mbaya kwa watoto ili kurahisisha harakati zake,
kwani viongozi walio wengi bado hawajawa na ufahamu wa kutosha wa kuweza
kutofautisha juu ya kazi anazopaswa kushirikishwa mtoto na zile ambazo
hapaswi kushirikishwa ili kutoathiri haki zake za msingi.
Aidha Bw. Nzunda aliongeza kuwa mradi wa PROSPER tayari umeshachukua hatua kwa kuanzisha miradi kadha wa kadha ili kuwakomboa watoto wanaotumikishwa katika mashamba ya tumbaku katika wilaya za Urambo na Sikonge mkoani Tabora.
Aidha
Bw. Nzunda alisema kwamba zoezi hili limeonyesha mafanikio makubwa sana
kwani watoto wengi waliokuwa wamenyimwa haki ya kusoma shule tayari
wamepelekwa shule kwa ufadhiri wa mradi huu, na wale waliomaliza darasa
la saba na kushindwa kuendelea wameanzishiwa miradi ya kilimo na ujasiriamali kwa vikundi mbalimbali vya akina mama.
‘‘……tunaomba serikali ituunge mkono katika hili ili kurahisisha jitihada zetu, naamini wizara
zikishirikiana na sisi kwa moyo wa dhati, tutafanikiwa kutokomeza
utumikishwaji huu na kutokomeza umaskini kwa wazazi wa watoto hawa,’’
aliasa Bw. Nzunda.
Akichangia
mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa sera wa mradi wa PROSPER, Bi.
Mary Kibogoya, alisema kuwa tatizo la ajira kwa watoto linazidi kuwa
kubwa na linasababishwa na umaskini wa familia zilizo nyingi hapa
nchini, jambo ambalo limewafanya watoto wengi kuendelea kukimbilia
katika ajira hizi za mashamba ya tumbaku hasa kutoka mikoa ya Kigoma,
Tabora, Singida, Katavi, na Rukwa.
Bi.
Kibogoya aliongeza kuwa mkutano huu utaleta mwamko mpya kwa kila mmoja
wetu juu ya nini kifanyike na hatimaye kuunganisha nguvu ya pamoja ili
kutokomeza utumikishwaji huu wa watoto, na akatoa wito kwa serikali na
wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada zinazofanywa na mradi wa PROSPER ili kutokomeza ajira hizi mbaya kwa watoto.
Naye
Bi. Cindy Serre ambaye ni Meneja miradi wa taasisi ya ECLT toka Geveva,
nchini Uswisi, ambao ni wafadhiri wa mradi wa PROSPER hapa nchini,
alisema kuwa lengo la mkutano huu ni kuifanya serikali na wadau wengine
wajue ukubwa wa tatizo hili la utumikishwaji wa watoto na kuweka mikakati ya nini kifanyike ili
kutokomeza hizi ajira mbaya na kuboresha maisha ya watoto hawa, lakini
hili haliwezi kufanikiwa pasipo serikali kuunga mkono jitihada hizi.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa mradi wa PROSPER Bw. Bahati
Nzunda, Meneja wa Sera Bi. Mary Kibogoya na maofisa waandamizi wa mradi
huo kutoka mkoani Tabora, wengine ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Urambo Bw. Adam Malunkwi na Mwakilishi wa Shirika la kazi duniani (I.L.O) Bi. Noreen Toroka.
Wengine
ni Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya ECLT toka Geneva , Uswisi, Bi. Sonia
Velazquez, Ofisa Mkuu–Mipango wa taasisi ya Winrock International toka
Marekani, Bi. Vick Walker, Meneja miradi wa ECLT toka Geneva , Uswisi,
Bi. Cindy Serre, wawakilishi wa taasisi na makampuni ya tumbaku hapa
nchini na maofisa toka serikalini waliowakilisha wizara mbalimbali.



No comments:
Post a Comment