Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Idadi
ya maiti za ajali ya kuzama kwa Meli ya MV Skagit zimeongezeka na
kufikia 89 baada ya miili mingine 11 kupatikana leo katika maeneo manne
tofauti ya visiwa vidogovidogo vilivypo mwambao wa Zanzibar.
Afisa
Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina,
amesema kuwa miili iliyopatikana leo, sita ni wanaume akiwemo kijana
mdogo na mingine mitatu ya wanawake.
Inspekta
Mhina amesema, maiti zote zimezikwa katika makaburi ya pamoja ya Kama
yaliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar chini ya usimamizi wa Jeshi la
la Wananchi wa Tanzanaia JWTZ, Jeshi la Polisi, MKMK, JKU na Varantia.
Amesema
miili hiyo ilipatikana katika viisiwa vya Pungume, Fumba, Chumbe na
eneo linalokupwa na kujaa maji la Funguyasini maeneo jirani na kisiwa
mama cha Unguja.
Naye
Mkuu wa Polisi Kikosi cha Wanamaji na Bandari Zanzibar SP Martin Lisu,
amesema kuwa kunauwezekano mkubwa kuwa maiti hizo zinaibuka kutoka
katika meli hiyo ya Skagit.
Kamanda
Lisu, amesema kuwa kutokana na kuendelea kuibuka kwa maiti hizo,
Maafisa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wanaendelea na zoezi lao la
kutafuta miili mingine na kupokea taarifa za kuonekana kwa mwili kutoka
kwa watu wenye vyombo binafsi vya uvuvi na kuzifuatilia.
Hivi
karibuni akizungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya
Kikwete, Daktari Mkuu Mwelekezi wa Jeshi la Polisi nchini Dk. Ahamed
Makata, alisema kuwa maiti nyungi zitaweza kupatikana ifikapo siku ya
nne tangu kuzama kwa meli hiyo.
Alisema
tabia ya maiti ya binadamu aliyekufa maji na kuzama, haiwezi kukaa
chini ya maji kwa muda mrefu kama haikufungwa na kitu kizito kabla ya
kuzama.
"Kwa
kawaida maiti ya mtu aliyekufa maji haiwezi kukaa ndani ya maji wakati
wote na kwamba hata kama itaendelea kubaki majini lakini katika muda wa
kuanzia siku tatu na nne mwili ama miili hiyo nilazima ianze kuibuka na
kuelea juu ya maji". Alisema Dk. Makata.
No comments:
Post a Comment