Benki
ya CRDB PLC imeibuka mshindi wa tenda ya kutengeneza tiketi za
elektroniki za kuingilia uwanjani iliyotangazwa na Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF).
Kampuni
saba zilijitokeza katika hatua ya awali ya kuonesha nia (Expression of
Interest) kwa ajili ya tenda hiyo ambapo Aprili 19 mwaka huu Kamati ya
Mipango na Fedha ya TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya shirikisho
ilipitia maombi hayo na kupitisha nne kati ya hizo.
Baadaye
kampuni hizo nne; CRDB Bank PLC, Prime Time Promotions, Punchlines (T)
Limited na SKIDATA People Access Inc. zilitakiwa kuwasilisha rasmi tenda
zao zikionesha jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo pamoja na gharama ya
utengenezaji kwa tiketi moja.
Bodi
ya Tenda ya TFF ilikutana Julai 13 mwaka huu kwa ajili ya kupitia tenda
hizo ambapo kampuni zote nne zilifanya uwasilishaji (presentation) wa
jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo, na baadaye kuipa kazi hiyo benki ya
CRDB.
Uamuzi
huo wa Bodi ya Tenda uliwasilishwa mbele ya Kamati ya Utendaji ya TFF.
Kamati ya Utendaji ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Julai 14
mwaka huu iliridhia uteuzi huo wa benki ya CRDB.
Baadhi
ya vigezo ambavyo Bodi ya Tenda ya TFF iliangalia na kuipa CRDB tenda
ni uwezo wa kufanya kazi hiyo (capacity), hadhi yake mbele ya jamii
(credibility) katika shughuli inazofanya na teknolojia ya kisasa
itakayotumika kutengeneza tiketi hizo.
Uamuzi
wa TFF kutangaza tenda hizo ulilenga kuimarisha udhibiti wa mapato ya
milangoni na kurahisisha mtiririko mzima wa washabiki kupata tiketi na
kuingia viwanjani.
Rais
wa TFF, Leodegar Tenga amesema: “Hatua hii ni muhimu sana, kwani
tulikuwa tukiisubiri kwa muda mrefu. Si tu itaimarisha udhibiti wa
mapato, bali pia itaondoa matatizo ya tiketi na kuendelea kujenga
credibility (kuaminika) ya TFF. Mafanikio haya si kwa TFF pekee bali
mpira wa miguu kwa ujumla.”
CRDB
imeanza mara moja mchakato wa shughuli hiyo ambapo tiketi hizo
zinatarajia kuanza kutumika rasmi katika kipindi cha kati ya miezi
miwili na mitatu kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment