ZITTO ADAI HATUWEZI KUKOPA KULIPANA POSHO
KAMBI ya
Upinzani Bungeni kupitia kwa Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe,
imependekeza bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2012/13, isijadiliwe
bungeni, badala yake iondolewe ili ikatayarishwe upya.
Katika
msimamo wao mzito bungeni jana mjini hapa, walidai kuwa bajeti ya
serikali kwa mwaka ujao ina upungufu mkubwa wa mambo ya msingi
yaliyokubaliwa na kupitishwa na Bunge lililopita.
Akiwasilisha
bajeti mbadala ya kambi hiyo inayoundwa na CHADEMA, Zitto alisema Bunge
haliwezi kuipokea bajeti ya serikali iliyosomwa na Waziri wa Fedha,
William Mgimwa, wiki iliyopita kwani haikutenga fedha zozote za mpango
wa maendeleo wa miaka mitano kama ilivyokubaliwa na Bunge.
Zitto
alisema kuwa Bunge lilikubali kuwa serikali itenge kiasi cha sh trilioni
nane kila mwaka kwa ajili ya mpango huo uliozinduliwa kwa mbwembwe na
Rais Jakaya Kikwete, lakini katika hali ya kushangaza hakuna fedha
zozote zilizotengwa.
“Serikali
imeshindwa kuheshimu uamuzi uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba
ya
Jamhuri ya Muungano….imeshindwa kusimamia ahadi zake yenyewe, hivyo
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iiondoe bungeni, bajeti
iliyoileta ili ikatayarishwe upya ikidhi matakwa ya mpango huo kama
ulivyoidhinishwa na Bunge,” amesema Zitto.
Deni la taifa
Kuhusu
deni la taifa, Zitto alisema hawawezi kukubaliana na bajeti iliyosheheni
uzito mkubwa wa deni la taifa ambalo kwa kila dalili haliwezi kulipika
na hawako tayari kuiacha serikali iendelee kukopa bila mpango na hivyo
kuliweka taifa rehani.
Alidai
kuwa kama serikali ingekopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii
kama zinavyofanya nchi nyingi zilizoendelea, wasingekuwa na pingamizi,
lakini wanashindwa kukubali kwa vile sehemu kubwa ya mkopo wa fedha hizo
zinalenga katika matumizi ya kawaida ya serikali.
Kambi hiyo
ya upinzani ilisema kuwa deni hilo halilipiki na ndio maana hata
serikali yenyewe inajichanganya katika kuelekeza malipo ya deni hilo.
“Wakati
serikali ikidai kuwa deni hilo linalipika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) anaonyesha mashaka makubwa sana kutokana na
kasi ya kukua kwa deni la taifa.
Taarifa ya
mkaguzi na mdhibiti mkuu wa serikali inaonyesha kuwa deni la taifa
linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka sh trilioni 10.5 kwa mwaka
2009/2010 hadi sh trilioni 14.4 kwa mwaka 2010/2011. Ukisoma taarifa ya
Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, deni la taifa sasa limefikia sh
trilioni 22,” alisema.
Alisema
kutokana na serikali kukiri kuwa itakusanya mapato kidogo ya sh trilioni
8.7 kama makusanyo ya ndani huku ikitumia sh trilioni 10.6 kama
matumizi ya kawaida, ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ya nje itatumika
kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya ndani.
“Hatutaki
mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari ya
kifahari. Hatuwezi kukubali serikali iwaishi wazee wetu kwa kuwafanya
waishi maisha magumu, na kizazi cha sasa ambacho kinapigika; na ikope
maisha ya watoto wetu ili baadaye waje walipe madeni kutokana na uzembe
wa kizazi cha sasa!” alisema Zitto.
Matumizi ya mwaka jana
Waziri
huyo kivuli, alieleza sababu nyingine ya utata wa bajeti ya mwaka huu ni
kutofahamika hasa fedha zilizotolewa na kuidhinishwa na Bunge kwa
baadhi ya wizara zilivyofanya kazi.
Zitto
alisema Wizara ya Miundombinu na ile ya Uchukuzi ilitengewa fedha katika
bajeti iliyopita, lakini hadi sasa haijulikani zilitumikaje kwa kuwa
makandarasi wanadai malipo hayo, na kibaya zaidi fedha kwa ajili ya reli
hazikutolewa zote kama zilivyoidhinishwa na Bunge.
Alisema
wizara nyingi hazikupewa fedha za maendeleo kama zilivyoidhinishwa na
Bunge, huku halmashauri za wilaya zikiwa zimeathirika vibaya, ambapo ni
asilimia 47 tu ya fedha zilipelekwa katika halmashauri, miji na
manispaa.
Alisema
ndio maana baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge zilikataa makadirio ya
wizara kadhaa, kama vile Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Uchukuzi
na ile ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti, kabla Bunge lako halijajadili makadirio ya matumizi kwa
mwaka unaokuja, ni vema serikali itueleze kwanza fedha zilizotengwa
mwaka uliopita na hazikufika hatima yake nini,” alihoji.
Vipaumbele vyao
Zitto
alitangaza bajeti mbadala aliyoiita ya ukombozi, akisema namba moja ni
kujenga mazingira ya ukuaji wa uchumi vijijini kwa kurekebisha
miundomnbinu ya umeme, barabara, maji na miundombinu ya umwagiliaji.
Ili
kutimiza hilo, walipendekeza kutumia sh bilioni 600 kila mwaka, na fedha
hizo zitasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo Vijijini itakayokuwa chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pili ni
kukarabati Reli ya Kati na matawi yake ya Tanga/Arusha na Mpanda, ambapo
watatenga sh bilioni 443, lengo likiwa ni kuhakikisha reli ya kati
inasafirisha tani milioni 1.5 ya bidhaa kwa mwaka ambazo zitaliingizia
taifa fedha za kigeni kiasi cha dola za Kimarekani 1.5 bilioni, badala
ya dola 0.5 bilioni za sasa.
Vipaumbele
vingine ni afya, elimu kwa shule na zahanati vijijini kwa kutoa motisha
kwa walimu, madaktari na manesi kwa nusu ya mishahara yao. Aidha
wataongeza mishahara ya walimu na manesi kwa asilimia 50 pamoja na
kuboresha stahiki zao.
Kuongeza
kima cha chini cha mshahara hadi sh 315,000 kwa mwezi, kuanzisha pesheni
kwa wazee wa umri wa kuanzia miaka 60, kujenga uwezo wa viwanda vya
ndani, kupunguza mzigo wa matumizi ya magari ya kifahari ya serikali kwa
kuyapiga mnada, kufuta posho za vikao na kuanzisha Chuo Kikuu cha
Mtwara ili kuzalisha wataalamu katika sekta ya nishati.
Vipaumbele
vingine ni kupunguza safari za viongozi nje ya nchi na ukubwa wa
maafisa katika misafara ambayo imekuwa ikiigharimu serikali kiasi
kikubwa cha fedha.
Vingine
kupunguza misamaha ya kodi kutoka asilimia tatu hadi moja ya pato la
taifa, kuboresha kodi katika sekta ya madini ili taifa lipate asilimia
25 ya mauzo yake, kushusha kiwango cha kodi ya wafanyakazi (PAYE) kutoka
asilimia 14 ya sasa hadi 9 ili kupunguza makali ya maisha kwa
mfanyakazi.
Kamati ya Fedha na Uchumi
Mapema
akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Mwenyekiti wake,
Andrew Chenge, aligusia kuwa mfumko mkubwa wa bei za bidhaa ambao
umeongezeka kufikia asilimia 19.8 katika kipindi cha Desemba 2011,
kutoka asilimia 5.6 Desemba 2010, ni jambo la hatari kwa maendeleo ya
taifa.
Alisema
hadi kufikia Aprili, 2012 mfumko wa bei ulikuwa asilimia 18.7 ambao
ulisababishwa na kupanda kwa bei ya vyakula na hasa mchele, unga wa
sembe, mafuta ya kula na sukari.
Sababu
nyingine ni kupanda kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, gharama ya
nishati ya umeme pamoja na kuongezeka kwa gharama ya uzalishaji wa
bidhaa muhimu za viwandani na usafirishaji.
Chenge
alisema ingawa serikali ilijaribu kudhibiti kasi ya kupanda kwa bei za
bidhaa na huduma, bado kuna changamoto kubwa katika kumpunguzia
mwananchi makali ya maisha.
Aidha
thamani ya sh ya Tanzania dhidi ya dola ya Kimarekani ilishuka kufikia
dola 1599.98 katika kipindi cha mwaka 2011 kutoka dola 1449.5 kwa
kipindi cha mwaka 2010.
Kwa upande
wa sekta ya kilimo kamati hiyo imeitaka serikali ichukue uamuzi wa
makusudi na kuweka vivutio katika kilimo vitakavyogusa wakulima wote
nchini ili wazalishe zaidi ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika mabonde
mengine yaliyo katika ukanda wa ziwa na maeneo mengine nchini.
No comments:
Post a Comment