Baadhi ya watoto wanafunzi mchanganyiko na wale wenye ulemavu wakiandamana katika maadhimisho hayo.
Na sisi tunahaki sawa kama walivyo wanafunzi na watoto wengine!
Siku
ya Mtoto wa Afrika Oyeeeeeee!Nyuma ya wanafunzi hawa ni gari la kisasa
limelotolewa kama msaada kwa Shule ya Msingi Makalala inayosomesha
watoto wenye ulemavu.
Walemavu tukiwezeshwa tunaweza! Pichani aliyeshika kipaza sauti ni mmoja wa wanasheria wa CCBRT ambaye ni mlemavu wa macho.
Wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wakipewa tafsiri ya maneno kwa ishara katika maadhimisho hayo.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com- Mafinga
Wanafunzi
wenye ulemavu anuai katika Shule ya Msingi Makalala wameiomba Serikali
na wadau wengine kuwasaidia kuwajengea mazingira bora ya kujifunzia kwa
watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu bora kama ilivyo kwa watoto
wengine.
Kauli
hiyo imetolewa katika risala ya wanafunzi hao iliyosomwa Wilayani
Mafinga kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika
kiwilaya kwenye Shule ya Msingi Makalala nje kidogo ya Mjini wa Mafinga.
Katika
maelezo yao watoto hao wameiomba Serikali na wadau wengine kuwatizama
kundi la watoto wenye ulemavu anuai kwa jicho la karibu, hasa katika
uboreshaji wa mazingira jumuishi ya kujifunzia katika shule zenye watoto
wenye ulemavu.
Pamoja
na hayo wanafunzi hao walemavu wameomba kuboreshewa mazingira ya
lijifunzia katika Shule yao ya Makalala, ikiwa ni pamoja na kuwajengea
chumba maalumu kwa ajili ya kujifunzia kitakachokidhi mahitaji ya kundi
hilo maalumu.
Akizungumza
katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Mafinga, Bi. Farida Mwasumilwe alisema licha ya Serikali kujitahidi
kuboresha huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu bado kuna changamoto
nyingi hivyo kuomba wadau kushirikiana kwa pamoja kuwasaidia watu wenye
ulemavu hasa watoto.
Bi.
Mwasumilwe aliwataka wadau mbalimbali kusaidiana kutoa elimu kwa baadhi
ya wazazi ambao bado wamekuwa na kasumba ya kuwaficha watoto wenye
ulemavu ndani hivyo kukosa haki za msingi ikiwemo elimu, ambayo ndio
mkombozi pekee kwa kundi hilo.
“Naomba
tusaidiane kuwafichua watoto wote walemavu ambao baadhi ya wazazi
wamekuwa wakiwaficha ndani hivyo kukosa haki yao ya msingi. Pia jamii
haina budi kusaidia malezi ya watoto kwani mzigo huu sio waserikali
pekee,” alisema Mwasumilwe ambaye ni Ofisa wa Elimu Shule za Msingi
Wilaya ya Mafinga.
Katika
maadhimisho hayo yalioambatana na michezo mbalimbali kwa makundi ya
watu wenye ulemavu, Shirika la Sightsavers limeahidi kumalizia ujenzi
darasa la kisasa pamoja na baadhi ya vifaa vya kujifunzia litakalokuwa
na uwezo wa kufundishia wanafunzi wenye ulemavu shuleni hapo.
Shirika
hilo mbali na kukabidhi fimbo 35 maalumu za kutembelea kwa wanafunzi
wasioona pia limeahidi kutoa gari la kisasa kwa shule ya Makalala ili
kuwasaidia wanafunzi walemavu hasa wasioona kupata huduma zao nje ya
kituo hicho pale inapohitajika. (kila fimbo moja ina thamani ya sh
50,000 za kitanzania).
Maadhimisho
hayo yaliandaliwa na taasisi anuai zinazofanya kazi na watu wenye
ulemavu, zikiwemo Chama cha wasioona Tanzania (TLB), Kituo cha Habari
Kuhusu Walemavu nchini (ICD), Sightsavers, CCBRT, INUKA, SHIVYAWATA kwa
kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku
ya Mtoto wa Afrika mwaka huu inasema, “Haki za Watoto wenye Ulemavu; Ni
Jukumu letu Kuzilinda, Kuziheshimu, Kuziendeleza na Kuzitimiza”.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Kituo cha Habari Kuhusu Walemavu Tanzania (ICD)
No comments:
Post a Comment