Na Allan Ntana, Tabora
VIJANA 3 waliotembea kwa miguu umbali wa km 1400
kutoka mkoani Geita mpaka jijini Dar es salaam ili kuwasilisha kero mbalimbali
za wananchi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameiasa jamii kuwa na
uchungu na nchi yao na kuchukia aina zote za wizi wa rasilimali na unyanyasaji.
Wakizungumza na wananchi na baadhi ya viongozi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuja kuwapokea mara baada ya
kuwasili mjini Tabora vijana hao walisema lengo la kutembea umbali wote huo ni uchungu
mkubwa walio nao juu ya vitendo vya wizi na matumizi mabaya ya rasilimali za
nchi yetu vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali.
Aidha walieleza kuwa walilenga kulaani vitendo vyote
vya unyanyasaji raia wasiokuwa na hatia vinavyofanywa na watendaji wa serikali
katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya ardhi, mifugo na vyombo vya ulinzi na usalama
wa raia hususani polisi kujichukulia sheria mkononi pasipokujali haki za msingi
za raia wa nchi hii.
Walieleza kuwa dhamira yao kuu ni kufikisha kilio
cha wananchi kwa mheshimiwa Rais ili aelewe ukubwa na athari za vitendo hivyo
kwa jamii ambayo kila kukicha inazidi kulemewa na mzigo mzito wa ugumu wa maisha
ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo na wale ambao
hawajabahatika kufika katika vyuo hivyo ila wanahitaji kuwezeshwa.
‘Ndugu zangu kitendo cha kutembea usiku na mchana
kwa muda wa siku 37, tukinyeshewa na mvua, ni kutokana na uchungu mkubwa tulionao kwa
nchi yetu, wakati tunapanga safari tulikuwa vijana 200 na tulioanza safari
tulikuwa vijana 7 lakini tuliomaliza ni sisi 3 tu, alisema Khalid Seleman
ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu.
Seleman alieleza kuwa kitendo cha maofisa ardhi
kuwanyanyasa wananchi na kuwaondoa kwa nguvu ikiwemo kuwanyang’anya ardhi
waliyorithi toka kwa mababu zao pasipo fidia au msaada wowote ni miongoni mwa
kero zinawakabili wananchi walio wengi zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani
miongoni mwa jamii.
Aliongeza kuwa Tanzania inaheshimika ndani na nje ya Bara la Afrika kwa jinsi ilivyokuwa na uchungu kwa wananchi wanaoonewa na
kunyanyaswa na hivyo kusimama kidete kutetea ukombozi wa wananchi hao katika mataifa
yao, sasa inakuwaje leo hii inashindwa kukemea vitendo vya wizi wa rasiliamli
za nchi, unyanyasaji raia, dhuluma katika miliki za ardhi na umaskini
unaowakabili vijana walio wengi mijini na vijijini kiasi cha wengine kuitwa
‘panya road’.
Juma Maganga yeye alihoji heshima ya nchi iko wapi,
thamani ya wananchi na uadilifu wa viongozi alioujenga Hayati Baba wa Taifa Mwl
JK Nyerere viko wapi, kwani ni dhahiri serikali imeanza kusahau misingi ya nchi
hii iliyoasisiwa na baba wa Taifa ya kuthamini utu wa mwananchi, usimamizi
mzuri wa rasilimali za nchi kwa faida ya wote na kudumisha amani.
Athanas Michael yeye aliwakumbusha Watanzania kuwa
huu ni wakati wa kuunganisha nguvu zao na kuwafichua au kuwakataa hadharani viongozi
wote wanaoendekeza vitendo vya rushwa, unyanyasaji, wizi na matumizi mabaya ya rasilimali
za nchi na askari polisi wanaotumia nguvu nyingi kuwatesa raia.
‘Ndugu zetu sisi tumepita hapa Tabora kuwasalimieni tu
wakati tunasubiri ahadi ya kuonana na Rais, ila tambueni kuwa huu ni wakati wa
kuonyesha uchungu wetu kwa vitendo vyote visivyokuwa na faida kwa ustawi wa
nchi yetu na wananchi wake’, aliongeza.