Kazi
ya uwakilishi wa wananchi kwenye vyombo vya maamuzi sio kukaa ofisini na
kutembelea gari lenye kiyoyozi bali ni kuyajua matatizo na
changamoto zinazowakabili na kisha kuzipatia ufumbuzi.
Imekuwa
mazoea mara baada ya uchaguzi wabunge na madiwani wa vyama vyote kusahau
wajibu wao kwa wananchi jambo linalowafanya kuhaha unapokaribia wakati wa uchaguzi.
Hebu jaribu kukumbuka nyakati za mwisho wa Bunge hili lililopita la mwisho lililokuwa na bajeti,lilikuwa halina wawakilishi wa kutosha kwa kuwa wengi wao
walijaribu kujirudisha majimboni kwao ili kuanza kujenga upya imani ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu
baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa miaka minne na nusu.
Tabia
ya kutowajali wananchi imegharimu kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo kuwa
ndogo, Miradi kutokukamilika kwa wakati, Miradi kutekelezwa kwa viwango duni na
matumizi mabaya ya fedha za umma na madaraka.
Mmoja kati ya vijana mahili anayeteka kuwani nafasi ya ubunge jimbo la Tabora
mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi, Bandora Salum Mirambo (40) ambaye ni mkurungezi
wa kampuni ya Salu Security Services Ltd ya Tabora imemkera sana hali hiyo na hata kufikia hatua ya kutoa kauli hiyo.
Anasema
wabunge wengi kwa makusudi wamekuwa hawawatumikii wananchi waliowachagua
ipasavyo jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya maeneo husika.
Anasema,
“Mimi nikipewa ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo la Tabora mjini nitahakikisha
navitumia vizuri vyombo vya maamuzi kwa maana ya baraza la madiwani na bunge la
Jamhuri ya Muungano kutatua matatizo na kero mbalimbali za wananchi.”
Anasema
vyombo hivyo vya maamuzi vikitumiwa vizuri vinaweza kuleta matokeo chanya na
kuharakisha maendeleo ya wananchi kwa kuwa ndipo maamuzi ya kibajeti ufanyika.
Anasema
wabunge wengi wanaomaliza muda wao wameshindwa kuwatetea wananchi wao bungeni
na wala hawakuonekana kwenye vikao vya mabaraza ya madiwani na hivyo kushindwa
kujua kinachoendelea kwenye ngazi ya halmashauri.
Anasema
ubunge au udiwani unahitaji kiongozi ambaye ni mbunifu, mwenye maono na dira ya
kuwavusha watu wake kutoka kwenye umasikini kwa kuzibadili changamoto kuwa
fursa.
Bandora
anasema suala hilo limekuwa gumu kwa wabunge wengi ambao wamekuwa wakisubiri
fedha za kibajeti au za mfuko wa jimbo ambazo zinaukomo na hivyo kushindwa
kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi.
Kazi ya uwakilishi inahitaji mtu mwenye upeo wa kupambanua na kuchambua mambo
mbalimbali kuanzia ngazi ya kitongoji hadi ngazi ya vikao vya kamati za
maendeleo za mitaa, vijiji na kata.
Aidha
anasema mtu huyo anapaswa kuutumia upeo wake kuchambua mambo kwenye vikao vya
ushauri vya wilaya DCC na mkoa RCC ili kushawishi mwelekeo wa kuzipatia
ufumbuzi kero za wananchi wa jimbo lake.
Vikao hivyo muhimu vimekuwa vikipuuzwa na wabunge wengi na hata wanapohudhuria
wamekuwa hawatoi mchango chanya au kutoongea kabisa.
Anabainisha
kuwa kwa muda mrefu wabunge wengi wameshindwa kuonekana majimboni sio kwa
sababu ya vikao vya bunge au vya kamati za kudumu za bunge bali wanaogopa
kuombwa misaada na wapiga kura wao.
Jambo hili la kihekima linapaswa kutatuliwa na mbunge kwa kuwaonesha wapiga
kura wake fursa zinazowazunguka ili waanzishe shughuli za uzalishaji mali
badala ya kuwakimbia kwa hofu ya kuombwa.
Anasema,
“Nikifanyikiwa kuwa mbunge nitasimamia upatikanaji wa mikopo ya fedha ,zana za
kazi pamoja na maarifa ambayo yatawafanya wananchi kuziona fursa za uzalishaji
mali na kuzitumia.”
Anasema
kwa kuwashirikisha wananchi wa kada zote tutaimarisha shughuli za VICOBA
uanzishwaji wa SACCOS zenye nguvu ambazo zitapambana na masharti ya dhamana
yanayotolewa na taasisi za kifedha.
Bandora
anasema jambo lingine atakalo lifanya ni kuibana halmashauri ya Manispaa ya
Tabora kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo
kwa vijana na wanawake.
Anasema
endapo halmashauri hiyo ingekuwa ikitenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani
kwa mujibu wa sheria ingesaidia kubadili maisha ya wananchi wake kwa kiwango
kikubwa.
Anabainisha
jambo lingine atakalolipa kipaumbele ni uwazi katika kutekeleza majukumu yake
ya kibunge kwa maana ya wapiga kura kujua utaratibu na ratiba ya mikutano ya
kibunge, na vikao vya kamati za bunge ili kuondoa visingizio vya kutowajibika
kwao.
Jambo lingine atafanya mikutano ya hadhara na wananchi na makundi mbalimbali ya
kisekta ili kujua matatizo na changamoto zinazowakabili kabla ya kwenda bungeni
tofauti na ilivyosasa ambapo mbunge anakwenda Bungeni kuwasilisha mambo anayoyawaza kutoka kichwani kwake.
Anasema
wananchi wa Manispaa ya Tabora wamekabiliwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu
ambayo imedhoofisha shughuli zao za uzalishaji mali na uwekezaji wa makazi na
mambo mengine.
Anasema,
“Jambo hili nitalisimamia kwa kuwakosoa na kuwakemea waziwazi watu wanaotumia
madaraka yao ya utumishi wa umma au ya kisiasa kutengeneza migogoro ya ardhi
kwa manufaa yao.”
Kwa kuwa njia nyingine bora ya kukabiliana na vitendo vya dhuluma kwenye ardhi ni
kuwawezesha wananchi kuzijua sheria za ardhi za mwaka 1999 na sheria ya mipango
miji ya mwaka 2007.
”nitahakikisha
wakazi wa mji wa Tabora wanarasimisha shughuli zao pamoja na makazi kwa kupata
hati zitakazowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.”
Anabainisha
kuwa atahakikisha vyombo vya kisheria vinavyoshughulikia migogoro ya ardhi
vinawezeshwa kwa kupatiwa wataalamu,vitendea kazi na kutekeleza majukumu yake
kwa uwazi na haki.
Anavitaja
vyombo hivyo kwa mujibu wa sheria kuwa ni mabaraza ya Ardhi ya kijiji,
kata, mabaraza ya Ardhi na nyumba ya wilaya , mahakama kuu kitengo cha Ardhi na
mahakama ya Rufaa.
Bandora
anaweka wazi kuwa akiwa mbunge ataweka daraja la wazi kati yake na asasi za
kiraia, makundi maalumu ya watu wenye ulemavu ambayo yamesahauliwa na wabunge
na madiwani.
Aidha
anaeleza kuwa ataimarisha misingi ya utawala bora kwa kujenga ofisi za
wenyeviti wa mitaa kila kata kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji kwa wananchi.
Anasema
kwa kufanya hivyo kutapunguza malalamiko ya rushwa na kwamba atawawezesha
kupata posho na vitendea kazi kila mwezi.
Anasema atasimamia kikamilifu sekta za maji, elimu na afya ambazo
zinagusa na kuchochea ustawi wa sekta nyingine.
Bandora anasema atahakikisha zahanati zinakuwa na watumishi wa afya, dawa, vifaa tiba ili kupunguza msongamano kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete.
Aidha atahakikisha mpango wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya
Tabora unaanza mara moja kwa fedha kutengwa na pia kutafuta misaada kwa wadau
wa sekta ya afya.
Mkakati huo anasema ni wa makusudi utasaidia kupunguza vifo vya
watoto wenye umri chini ya miaka mitano na akinamama wajawazito.
Atahimiza uimarishwaji wa mpango wa damu salama
ambao umepuuzwa na wabunge na madiwani wengi huku wahitaji wakubwa ni watoto na
akinamama wajawazito.
Bandora anasema kama wanawake ni jeshi kubwa linalotumika kwenye
uchaguzi kwanini limekuwa likisahaulika mara baada ya uchaguzi kwa kuruhusu
vifo vyao wakiwa wajawazito?.
Anasema atasimamia mipango ya uboreshaji wa huduma ya maji
kutoka mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira TUWASA pamoja na kuhimiza
serikali kulipa madeni ya taasisi zake ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni
moja.
Atahimiza pia utekelezaji wa mradi wa maji ya ziwa Victoria
kutokea kijiji cha Solwa Shinyanga kupitia Nzega kuja Tabora na wilaya nyingine
za mkoa wa Tabora.
Aidha kwenye elimu atahakikisha hakuna mtoto anayekaa chini
katika shule za msingi za manispaa ya Tabora ambako kuna miti ya mbao na mbao
za kutosha.
Akizungumzia
michezo anasema kwamba atashirikiana na vyama vyote vya michezo kuinua michezo
kuanzia ngazi za mitaa, vijiji na kata tofauti na ilivyosasa nguvu zisizo
na utaratibu zimewekwa kwenye soka la wanaume pekee.
Anasema
ameamua kufanya hivyo ili kurudisha hadhi ya michezo ya mkoa wa Tabora
iliyokuwepo miaka ya nyuma.
“Kukosekana
kwa mikakati madhubuti katika michezo kumefanya vipaji vingi vya vijana wa
Tabora kupotea jambo ambalo limesababisha kupoteza ajira kupitia
michezo.”anasema Bandora.
Anasisitiza
kukitumikia Chama Cha Mapinduzi na kukifanya kuwakomboa wananchi na wanachama
wake kwa kuwaletea maendeleo halisi.