Pages

KAPIPI TV

Wednesday, May 25, 2016

WANACHAMA WAPYA 200 WAJIUNGA CHADEMA

Na Allan Ntana, Tabora

ZAIDI ya  watu 200 wamejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo na
kukabidhiwa kadi za uanachama katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika uwanja wa stendi ya mabasi katika kata ya Tutuo wilayani
Sikonge Mkoani Tabora.

Akikabidhi kadi mpya kwa wanachama hao katika mkutano huo
uliohudhuriwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya wa chama hicho wakiwemo
madiwani wote wa CHADEMA wilayani humo, Mwenyekiti wa Mkoa wa CHADEMA
Fransis Msuka alisema zama za kulegalega zimeisha kazi yao ni moja tu
ya kuisimamia serikali ya awamu ya tano kwa vitendo ili haki za
wananchi zipatikane kwa wakati.

Alieleza kuwa mara zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu
unaochochea umaskini hivyo akawataka wakazi wa kata hiyo kushikamana
na viongozi wao wa serikali ya kijiji na diwani wao ili kuharakisha
maendeleo ya kata hiyo.

'Nawapongeza sana ndugu zangu wa Tutuo kwa kuchagua viongozi wa
CHADEMA kuongoza serikali yenu ya kijiji na udiwani wa kata hii,
hamkufanya makosa, na dhamira yenu ya kutaka maaendeleo tayari diwani
ameshaanza kuitekeleza kwa vitendo', aliongeza.

Aliwahakikishia kuwa viongozi wao wamebeba kauli mbiu ya hapa kazi tu
na hawako tayari kwa namna yoyote ile kuona wananchi hao
wananyanyasika au kunyimwa haki yao ya msingi na kuongeza kuwa kasi
hiyo hakuna atakayeweza kuizuia na wako tayari kuwatumika usiku na
mchana.
 

Kada Mhamasishaji wa CHADEMA mkoani Tabora Elisha Daudi alisema
watendaji wa serikali iliyoko madarakani hawawezi kuleta mafanikio
makubwa kwa kuwa wametokana na CCM na wengi wao hawana moyo wa dhati
wa kuwatumikia wananchi bali kujinufaisha tu ndio maana hata Rais John
Pombe Magufuli anawatumbua majipu.

Alisema ili kata hiyo ipate maendeleo makubwa hawana budi kuachana na
CCM na kujiunga na CHADEMA na washirika wake wote ili kuunganisha
nguvu ya pamoja na kuanza mikakati mipya ya kuibadilisha Tutuo na
maeneo mengineyo.

Aidha alitahadharisha baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa
wilaya hiyo Hanifa Selengu kwa kuendekeza propaganda mbaya za
kukwamisha juhudi za madiwani wanaotokana na chama hicho za kutetea
maslahi ya wananchi kwa kusimamia ukweli na uwazi hasa kunapokuwa na
maamuzi yanayotia shaka.

'Baadhi ya viongozi wa CCM hawapendi kasi ya madiwani wa upinzani ndio
maana wanakuja juu pale wanapoambia ukweli, kama tukio la juzi la DC
kuamua kumwekwa rumande diwani wetu wa kata hii kisa kuhoji suala la
kutowapa nafasi za kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
vijana wa Sikonge, viongozi wa namna hiyo hawafai hata katika serikali
ya Rais Magufuli, 'aliongeza.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

WAKATI huo huo wananchi wa kata ya Tutuo wilayani Sikonge Mkoani
Tabora wamelalamikia kitendo serikali kuzuia kurushwa LIVE vikao vya
Bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma.

Wamesema kutooneshwa bunge hilo ni dhuluma kwa Watanzania kwani
mijadala yote inayoendelea imebeba dhamana ya maendeleo ya wananchi
hivyo wakabainisha kuwa Rais John Pombe Magufuli anapaswa kuingilia
kati suala hilo kama
alivyofanya katika Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es salaam.
 

‘Hili bunge ni la wananchi, tuna haki ya kuona jinsi wabunge wetu
wanavyotetea maslahi yetu ya kimaendeleo, sasa wametuzuia, hii sio
sawa, ni kutunyima haki yetu', alihoji Juma Athuman mkazi wa Tutuo.
 

Akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo, Mzee Rashid Mzelu alisema wananchi wengi wanafuatilia sana kila
kinachoendelea bungeni tofauti na viongozi wanavyodhani, na hili linasaidia
kuona mbunge wao anavyowatetea na yule anayesubiri posho tu.

‘Kama hatuoni kinachoendelea bungeni tutajuaje kama mwakilishi wetu yuko
bungeni au kaenda kwenye mambo yake, kuna mambo tumemtuma ayalete bungeni,
sasa hatujui kama kayafikisha au la kwa sababu hata bungeni watoro wapo
pia, sasa akirudi tutampongeza kwa lipi’, alihoji.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Tutuo Philipo Arcado Kayumba alisema
wakati wa sherehe za kumwaga Mwenyekiti wa Kwanza wa Chama cha Mapinduzi
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema kwa sasa dunia inahitaji
nuru katika kila jambo ili wananchi waamue wenyewe, bunge ni nuru ya
wananchi.

Kada Mhamasishaji wa CHADEMA mkoani Tabora Elisha Daudi alisema kitendo cha
vikao vya Bunge kutooneshwa LIVE ni dhuluma kubwa kwa Watanzania, hivyo
akamwomba Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati suala hilo kama
alivyofanya katika Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es salaam.

Viongozi wengine wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa Fransis Msuka,
Mratibu wa Kanda Christopher Nyamwanji na diwani wa kata ya Tutuo Clemence
Msumeno walibainisha wazi kuwa vikao vya bunge ni muhimu sana  kwa
mustakabli wa maendeleo ya Taifa na ni kipimo sahihi kwa mbunge kama kweli
anatekeleza wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali ipasavyo au la.

No comments: