Pages

KAPIPI TV

Monday, April 25, 2016

WAZAZI WAPONGEZA MAFANIKIO NEW ERA SEKONDARI

Na Allan Ntana, Tabora

WAZAZI Mkoani Tabora wamepongeza walimu na wafanyakazi wa shule ya Sekondari New Era iliyopo katika Manispaa ya Tabora kwa jitihada zao kubwa zilizowezesha shule hiyo kuwa na mafanikio makubwa kitaaluma tangu kuanzishwa kwake.

Pongezi hizo zimetolewa juzi katika mahafali ya 7 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo.

Walisema jitihada za walimu na watumishi wa shule hiyo zimewezesha watoto wao kuwa na nidhamu nzuri ikiwa ni pamoja na maendeleo mazuri kitaaluma.

'Kwa kweli nawapongeza sana walimu, mtoto wangu alikuwa na nidhamu mbovu sana lakini tokea ajiunge na shule hii tabia yake imebadilika, amekuwa mtoto mzuri hata nyumbani anafanya kazi kwa kujituma na hata maendeleo yake kitaaluma yamekuwa mazuri tofauti na alivyokuwa awali', alisema mzazi mmojawapo.

Mzazi mwingine aliyejitambulika kwa jina la mama Mary alisema shule hiyo sasa ina mazingira mazuri ya kusomea yanayowafanya watoto wasome kwa bidii, na kitendo cha kuanzisha shule ya awali na msingi katika shule hiyo kinawarahisishia wazazi hao, kwani mtoto anaweza kuanza chekechea hapo hapo na kuendelea hadi kidato cha sita tena kwa gharama nafuu.

Akitoa taarifa ya shule hiyo Mkuu wa shule Efel
Mbata alisema mafanikio makubwa ya shule hiyo ilianzishwa mwaka 2004
yamechochewa na ushirikiano mzuri wanaopata toka kwa wazazi wa watoto
wanaosoma shuleni hapo.

Alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2004 ikiwa na kidato cha kwanza
lakini baada ya kupata mwitikio mkubwa wa wanafunzi kutokana na
ufundishaji mzuri wa walimu shuleni hapo walilazimika kuanzisha kidato
cha tano huku msukumo mkubwa ukitoka kwa wazazi wa watoto hao.

Alifafanua kuwa chachu kubwa ya mafanikio ya shule hiyo katika kipindi
hicho kifupi yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya walimu na
wafanyakazi wengineo hali inayowafanya wanafunzi kujituma zaidi katika
masomo yao.

 Aidha alisema shule hiyo imekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wa
kidato cha kwanza hadi cha sita kwa kipindi kifupi kutokana na huduma
bora za kitaaluma zinazotolewa shuleni hapo sambamba na uwepo wa
maabara za masomo yote ya sayansi tofauti na shule zingine.

Mbali na masomo yanayofundishwa kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza
hadi cha nne, alitaja michepuo ya masomo inayofundishwa shuleni hapo
kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita kuwa ni PCB, PCM, ECA, CBG,
EGM, HE, CBM, HGL, HGK na HKL masomo ambayo yamewavuti wanafunzi wengi
zaidi.

Ili kuendelea kutoa huduma nzuri na taaluma bora kwa wanafunzi shuleni
hapo aliwataka wazazi wenye watoto katika shule hiyo kulipa ada kwa
wakati ili kufanikisha malengo mbalimbali ya shule hiyo.

Alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule yake kuwa ni upungufu
wa vitabu kwa baadhi ya masomo na vifaa vya maabara.</div>

No comments: