Pichani juu na chini ni baadhi ya viongozi wa mila (Laigwanan na Laiboni) na akina mama mashuhuri (Ngaigwanan) wilayani Lolilondo wakisoma na kujadili azimio la pamoja la kumlinda mtoto wa kike kabla ya kulipitisha na kusaini wakati wa kongamano kubwa la siku mbili lililofanyika katika ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
VIONGOZI wa kimila wa jamii ya Kimaasai na wanawake mashahuri wamepitisha Azimio la Loliondo lenye lengo la kumlinda mtoto wa kike na kuhakikisha maendeleo yake kiafya, kielimu na kitamaduni.
Azimio hilo ambalo limetiwa saini na viongozi hao mwishoni mwa kongamano kubwa la siku mbili lililofanyika, katika ofisi za halmashauri wilayani Ngorongoro, linapinga mila na desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike. Mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati.
Kabla ya kupitishwa na kusaini maazimio hayo viongozi hao wa kimila na mashuhuri walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kuendeleza mijadala na uelewa na hatimae kuamini kwamba baadhi ya mila na desturi zinachangia na kuchochea athari za kiafya na kijamii hasa kwa watoto wa kike na kina mama.
Viongozi hao wamepitisha azimio hilo baada ya kupitia kifungu hadi kifungu na kuridhia yaliyomo kwa kuzingatia wajibu wao ndani ya jamii na uwezo mkubwa wa ushawishi kama viongozi wa mila (Laigwanan na Laiboni) na akina mama mashuhuri (Ngaigwanan) .
Aidha walisema kwamba watatumia nafasi zao kuelimisha jamii juu ya malezi bora ikiwa ni pamoja na mahali salama pa kulala watoto wa kike na kiume na kuelimisha jamii umuhimu wa elimu kwa kuwapeleka shuleni hasa kwa watoto wa kike.
“Naomba viongozi wenzangu twende tukaelimishe jamii juu ya madhara ya tohara kama tulivyoazimia na kuanzisha mchakato utakaosaidia kupunguza au kumaliza kabisa matendo ya tohara ndani ya jamii yetu,” alisema Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai.
Viongozi hao pia wamesema ni vyema jamii ya kifugaji kuacha kuendelea na vitendo vya kuwaoza watoto wa kike wakiwa bado wadogo na wakati mwingine kwa kuwakatisha masomo na kuwalazimisha kuolewa.
“Sisi kama viongozi tusiendelee kuwa chanzo cha kuendeleza matukio haya kwani ni ya ukatili kwa watoto wetu wa kike na tutumie nafasi hii kwenda kuwaelimisha viongozi wenzetu wengine mashuhuri ili kusambaza ujumbe na jamii ijue athari zinazotokana na ukeketaji pamoja na kuozesha watoto wetu wakiwa katika umri mdogo,” alisema Laanoi Munge.
Viongozi hao pia wamedhihirisha kuwa matukio ya vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni vimechangia utoro nyumbani na kwenda kuishi kwa muda kwenye vituo maalum kwa kuogopa kufanyiwa tohara.
Watoto hao wamekuwa na hali ya kutoroka baada ya kugundua kwamba kuna matukio ya ulemavu na athari nyinginezo za kiafya zinazotokana na ukeketaji na salama yao ni kujitoa katika jamii hiyo na kutafuta hifadhi kwingine.
Azimio hilo la Loliondo ambalo pia lilitiwa saini na waganga wa tiba asilia limetoa mwelekeo wa kuboresha afya ya uzazi, elimu na malezi kwa watoto wa kike katika jamii ya Kimaasai.
Aidha limetoa namna bora ya utekelezaji na kupitisha taratibu zitakazosaidia watoto wa kike wanaokimbia tishio la ukeketaji na kuhakikisha kwamba watasoma na kupata huduma zote za afya.
Katika maeneo yao baada ya kutia saini viongozi hao wameahidi kuonyesha ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa serikali katika ngazi zote, viongozi wa dini, vyombo vya habari, walimu, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo katika maeneo yote ndani ya wilaya ili kuboresha afya ya uzazi, elimu na malezi bora kwa watoto.
Pamoja utiaji saini wa Azimio la Loliondo,viongozi hao wameliomba shirika la UNESCO na halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kushirikisha viongozi wengi zaidi, kuendelea kutoa elimu kwa viongozi wa kimila na kuendelea kuwasaidia katika majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu na kuwasaidia uratibu wa shughuli zote za kupingana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.
Katibu wa Baraza la Mila (W) Ngorongoro, Laanoi Munge akisoma azimio la kumlinda mtoto wake baada ya kulifanyia marekebisho ya pamoja mbele ya viongozi wa mila wa wilaya ya Ngorongoro.
Kongamano hilo lililozaa Azimio la Loliondo ni mwendelezo wa warsha zinazotolewa na UNESCO kwa ajili ya kutoa elimu ya kuwajengea uwezo na kugawa majukumu kwa viongozi wa kimila, wamama mashuhuri, viongozi wa dini, wakunga wa jadi pamoja na waandishi wa habari ili kutekeleza vizuri ufuatiliaji wa afya ya uzazi na malezi bora kwa watoto katika jamii ya Kimaasai.
Utiaji saini wa Azimio la Loliondo ulishuhudiwa na Katibu Tawala Wilaya ya Ngorongoro Bw. Lemuel Kileo, maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bw.Herman Mathias na Bi.Rose Haji Mwalimu.
Kongamano hilo la siku mbili lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro limeendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Katibu wa Baraza la Mila wilayani Ngorongoro, Laanoi Munge (kushoto aliyesimama) akimsomea baadhi ya maboresho ya vipengele vilivyomo ndani ya azimio hilo Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI kutoka UNESCO, Mathias Herman (kulia).
Laigwanan wa kata ya Pinyinyi, Moses Mollel akiwasilisha maboresho ya azimio hilo baada ya kulijadili kabla ya kusaini.
Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI kutoka UNESCO, Mathias Herman akifafanua jambo kwa viongozi hao baada ya kuridhishwa na maboresho ya azimio hilo katika kongamano kubwa la siku mbili lililofanyika katika ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha. Kutoka kushoto ni Mkalimani wa kwenye kongamano hilo Mchungaji, Mark Murenga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kileo, Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai pamoja na Kiongozi wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka redio ya jamii Loliondo FM nao walikuwepo kuhudhuria tukio hilo la utiaji saini wa azimio la kumlinda mtoto wa kike.
Baadhi ya maafisa wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro na waandishi wa habari waliokuwepo ukumbini kushuhudia tukio hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai (kushoto), Kiongozi wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu (wa pili kushoto) Laigwanan wa kata ya Pinyinyi, Moses Mollel (wa pili kulia) pamoja na Ngaigwanan wa Malambo, Miriam Lembirika wakisaini kwa niaba ya viongozi wengine wa mila wa Wilaya ya Ngorongoro, Azimio la Liliondo.Wanaoshuhudia (waliosimama) ni KatibuTawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kileo (kulia), Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo (wa pili kulia), Mtaalamu wa masuala ya vyombo vya habari vya kijamii na Mkufunzi kutoka UNESCO, Rose Haji Mwalimu (wa tatu kulia) pamoja na Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI wa UNESCO, Mathias Herman.
Walioshuhudia tukio hilo wakipiga makofi baada ya zoezi hilo.
Baadhi ya viongozi wa kimila na waandishi wa habari wakishuhudia tukio hilo la kusainiwa kwa azimio la kumlinda mtoto wa kike.
Zoezi la utiaji saini likiendelea kwa kila kiongozi aliyeshiriki kongamano kubwa la siku mbili lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambalo limefanyika katika ofisi za halmashauri ya wilaya Ngorongoro, jijini Arusha.
Picha ya pamoja baada ya zeozi kukamilika.
No comments:
Post a Comment