Na:George Binagi-GB Pazzo
Mvua
zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Jijini
Mwanza, zimesababisha Uwanja wa ndege wa Jiji hili kufungwa kwa muda wa masaa
matano kutokana na kujaa maji.
Meneja wa Uwanja huo Easter Madale alisema kuwa
shughuli za usafirishaji uwanjani hapo, hii leo zilikwama kuanzia majira ya saa
tatu asubuhi hadi saa nane mchana, baada ya maji ya mvua kujaa katika maeneo
mbalimbali ikiwemo eneo la kukimbilia ndege.
Alisema kuwa tatizo la maji kujaa uwanjani hapo
halikusababishwa na ubovu wa miundombinu, bali ni kutokana na uwanja huo
kuzungukwa na vilima vipatavyo saba ambavyo wakati wa mvua za masika
hutiririsha maji ambayo huingia hadi uwanjani.
Madale alibainisha kuwa mara ya mwisho maji
kujaa uwanjani hapo ilikwa mwaka 2012 na kwamba tatizo hilo lilishughulikiwa
kwa kujengewa mifereji mikubwa kwa ajili ya kuzuia maji kuingia katika uwanja
huo huku akiongeza mvua iliyonyesha leo imesababisha mifereji na mitaro
kuharibika.
Baadhi ya wasafiri wamelalamikia hali hiyo kwa
kile walichoeleza kuwa ni ratiba zao za kusafiri kwa ajili ya shughuli zao
kukwama na hivyo kuingia kupata usufumbu mkubwa.
Katika hatua nyingine,Mvua hiyo zimesababisha
athari mbalimbali kwa wakazi wa Jiji la Mwanza wakiwemo wakazi wa Kihewa, baada
ya nyumba zao kujaa maji na hivyo baadhi ya kaya kuhifadhiwa katika shule ya
Msingi Kilimahewa.
Kwa mjibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari na Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Charles Mkumbo, mvua hiyo
imesababisha vifo vya watu wawili, mmoja akifahamika kwa jina la Zainab Shaban (18) ambae alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari
Nyamanoro aliesombwa na maji wakati akijaribu kuwahi kwenye mtihani wa kuhitimu
kidato cha nne pamoja na dereva pikipiki ambae jina lake halikufahamika mara
moja.
Alfajiri ya leo Jiji la Mwanza lilikumbwa na
mvua ambayo ilidumu kwa zaidi ya masaa matano, hali iliyosababisha adha
mbalimbali kwa wakazi na wageni wa Jiji hili.
Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya hali ya hewa
Kanda ya Ziwa Augustino Duganda amebainisha kuwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa itaendelea
kuwa na mvua nyingi hadi kufikia mwezi wa 12 mwaka huu hivyo ni vyema wananchi
wanaoishi katika maeneo hatarishi ikiwemo yenye mafuriko na mkondo wa maji
wakahama kutoka kwenye maeneo hayo ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Karibu Uwanja wa ndege wa Mwanza ila si wakati wa Mvua
BINAGI MEDIA GROUP, KWA PAMOJA TUIJUZE JAMII
Picha Zaidi BONYEZA HAPA
No comments:
Post a Comment