Pages

KAPIPI TV

Wednesday, September 2, 2015

MMLIKI WA ST. MATHEW ACHOMOLEWA KESI YA TALAKA NA MGAWANYO WA MALI

court_gavel
Na Mwandishi wetu
MAHAKAMA ya Mwanzo Mbagala, Dar es Salaam imesema haiwezi kumuamuru Mmiliki wa nne za Shule za Sekondari, St Mathew na St Marks ,Thadei Mtembei kutoa talaka kwa Magreth Mwangu kutokana na ndoa yao kuwa batili.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Rajab Tamambele alisema ndoa aliyofunga Mwangu pamoja na Mtembei ambayo ni ya kimila ni batili kwa kuwa mdai hakutoa cheti cha ndoa hiyo ilipofungwa.
Alisema kwa misingi hiyo, mahakama haiwezi kumuamuru Mtembei kutoa talaka kwani aliwasilisha cheti cha ndoa ya mke mmoja aliyoifunga mwaka 1985.
pia alisema mahakama hiyo haiwezi kugawa mali kama ambavyo mdai ameiomba mahakama, ambapo amesisitiza kuwa mgawanyo wa mali unatokana na ndoa halali ambayo baba na mama wanaishi pamoja.
‘’Mashahidi wote wameeleza kuwa Mtembei na Mwangu walikuwa wanakutana hoteli ya Sleep Inn. Kwa hivyo mahakama inaona kuwa uhusiano kati ya mdai na mdaiwa ulikuwa wa kimapenzi pekee au hawara na kwa lugha ya kistaarabu tunaita mzazi mwenzie,’’ aliongeza Tamambele.
Alifafanua kuwa kulipa mahari ambapo mdai aliieleza mahakama kuwa alitolewa ng’ombe watano, sio njia ya kufunga ndoa bali ni kuelekea kufunga ndoa.
Aliendelea kusema kuwa kitendo cha baba kupewa mahari akiwa peke yake bila ya kuwa na mzee wa kabila hilo kuthibitisha, sio sahihi katika sheria za ndoa.
Akisoma hukumu hiyo kwa saa moja, Hakimu Tamambele alisema kuwa watoto watatu kati ya Mtembei na Mwangu ni batili kwani wamezaliwa nje ya ndoa, hivyo mahakama haiwezi kuamuru watoto hao kupatiwa matunzo.
‘’Mdaiwa anatakiwa kushukuru kitendo cha mdai kujenga nyumba tatu kwa ajili ya watoto kwani wengine hawawezi kufanya kitu kama hicho. Kila mzazi anatakiwa kuwatunza watoto hao, ’’ alisema.
Akizungumzia kuwakilishwa kwa mdaiwa, alisema kwa mujibu wa sheria ya kama mdaiwa ni mgonjwa anaweza akawakilishwa ambapo mtoto wake, Peter ndiye alichukua nafasi ya kumuwakilisha baba yake.
Aidha, alisema haki ya kukata rufaa kwa mdai iko wazi na kwamba inatakiwa kukatwa kwa siku 45.
Katika kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Juni 5, mwaka huu, Mwangu aliiomba mahakama kumuamuru mdaiwa kutoa talaka, matunzo ya watoto na ya machumo ya pamoja yenye thamani ya Sh milioni 800.
Alisema kesi hiyo ilikuwa na jumla ya mashahidi nane ambapo watano kutoka upande wa mdai na watatu upande wa mdaiwa.
Alisema mdai alifungua kesi kupitia ofisi ya Ustawi wa jamii na ilipoanza kusikilizwa mdai alisema walianza mahusiano mwaka 1995 ambapo walizaa watoto watatu na walijenga shule nne, nyumba pamoja na hoteli tatu za Dar es Salaam na Bukoba.

No comments: