CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza kurudiwa kwa kura za maoni kesho katika
majimbo matano nchini, kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza
wakati wa mchakato wa upigaji kura hizo.
Wakati
agizo hilo likitolewa kwa majimbo husika, hatma ya watakaopeperusha
bendera ya CCM katika ubunge, udiwani na Wawakilishi inatarajiwa
kujulikana wakati wowote kuanzia sasa baada ya vikao vya chama kuanza
vikao vyake mjini Dodoma jana.
Kamati
Kuu ya chama hicho, ambacho kimesema kipo vizuri na kwamba vikao vyake
vya kupata wagombea vinakwenda vizuri, ilitoa jana maagizo ya kurudiwa
uchaguzi huo baada ya Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kufungua kikao
hicho.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari kwamba
majimbo yaliyokumbwa na dosari hizo na ambayo yanatakiwa kurudia
uchaguzi kesho ni Rufiji mkoa wa Pwani, Kilolo mkoa wa Iringa, Makete
mkoa wa Njombe, Busega mkoa wa Simiyu na Ukonga mkoa wa Dar es Salaam.
Akitoa
maelekezo hayo ya chama, alisema kikao cha Kamati ya Maadili
kilimalizika juzi usiku na kwamba jana kikao cha Kamati Kuu kilianza.
Alisema kama kitakuwa kimefanikiwa kumaliza, leo kitaanza kikao cha
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
“Majimbo
matano yanatakiwa kurudia kura za maoni Alhamisi Agosti 13 baada ya
kutokea dosari mbalimbali...baada ya marudio ya kura hizo yanatakiwa
kuleta matokeo kwa ajili ya uamuzi,” alisema.
Nape
alisisitiza kwamba kazi ya kupata wagombea wa nafasi ya ubunge,
uwakilishi na udiwani inaendelea vizuri. Hata hivyo, hakuainisha dosari
zilijitokeza katika majimbo hayo matano, kiasi cha kuamua kurudia kura.
Busega
Katika
Jimbo la Busega, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani
alitangazwa kuangushwa kwenye kura za maoni baada ya kupata kura 11,829
wakati Dk Raphael Chegeni aliongoza kwa kupata kura 13,048. Hata hivyo,
matokeo hayo yalipingwa kwa madai ya kugubikwa na uchakachuaji.
Chegeni aliwahi kuwa mbunge kabla ya Dk Kamani, ambaye ndiye mbunge wa sasa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu.
Ukonga
Kwa
upande wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa ndiye alikuwa ametangazwa
kuongoza kwa kupata kura 10,000 akifuatiwa na Ramesh Patel aliyejipatia
kura 7,356. Jimbo hilo lilikuwa na wagombea 13. Silaa ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM na ni Meya wa Ilala.
Kilolo
Venance
Mwamoto ni mgombea aliyekuwa ameibuka na ushindi katika jimbo la Kilolo
na kupata kupata kura 11,200 na kufuatiwa na Profesa Peter Msolla
aliyepata kura 10,014. Wagombea walikuwa 15.
Akizungumza
jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kilolo, Clement Mponzi alisema
uchaguzi huo unarudiwa katika kata zote kumaliza utata uliothibitishwa
katika malalamiko yaliyotolewa kupitia rufani ya Profesa Msolla.
Profesa
Msolla katika rufaa yake, alisema anapinga matokeo hayo kwa sababu
yalitangazwa bila kuridhiwa na wagombea au mawakala wao huku akidai
alikuwa anaongoza kwa kura 13,409.
Msolla
aliwahi kuwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na ndiye
mbunge wa sasa wakati Mwamoto aliwahi kuwa mbunge kabla ya Msolla.
Akizungumzia
dosari zilizosababisha uchaguzi kurudiwa, Katibu wa CCM wa Mkoa wa
Iringa, Hassan Mtenga alisema kuna baadhi ya wagombea hawakuridhika na
matokeo hivyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama, ndiyo maana
imeamriwa kurudiwa kila mmoja apate haki anayostahili.
Makete
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Bilinith Mahenge
anayetetea nafasi yake, alikuwa ameibuka mshindi kwenye kura za maoni
kwa kupata kura 8,534 dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, Dk Norman
Sigala aliyepata kura 8,211.
Wagombea wengine na kura kwenye mabano ni Bonic Muhami ( 500), Fabianus Mkingwa ( 466) na Lufunyo Rafael aliyepata 226.
Rufiji
Kwa
upande wa matokeo ya Rufiji, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif
Rashid, alionekana kuanguka kwa kupata kura 3,000 wakati mpinzani wake
Mohamed Mchengelwa alipata kura 4,000.
Hata
hivyo, akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Kaimu Katibu
Mkuu wa CCM mkoa wa Pwani , Abihudi Shilla alisema kulikuwa na
mkanganyiko wa matokeo hali iliyolazimu wasubiri uamuzi kutoka ngazi ya
taifa.
Mbivu, mbichi
Awali
akifungua kikao cha Kamati Kuu(CC), Rais Kikwete alisema wanatarajia
kufanya kazi jana na leo, kupata watakaopitishwa kwa ajili ya
kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka
huu.
“Mkutano
umefunguliwa tutafanya kazi leo(jana) na kesho(leo) tupate
wataopeperusha bendera, na baada ya kitakachobakia ni CCM iyena iyena
mpaka mwisho,” alisema Rais Kikwete.
Aidha,
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akimkaribisha Mwenyekiti kufungua
kikao hicho, alisema wajumbe waliotakiwa kuhudhuria mkutano huo ni 32,
lakini waliokuwepo wakati kikao kikifunguliwa ni 25 na kwamba akidi
imetimia.
Wajumbe
waliohudhuria katika kikao hicho ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein, Makamu wa Pili wa Rais
Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri Mkuu Mizengo Pinga, Waziri Mkuu
mstaafu Dk Salim Ahmed Salim, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose
Migiro na Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samiha Suluhu
Hassan.
Wengine
ni Spika wa Bunge, Anne Makinda, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu
Ameir Kificho, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia
Simba, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi
Chana; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wasira, Waziri wa
Ardhi, William Lukuvi na Waziri wa Ulinzi Dk Hussein Ali Mwinyi.
Wajumbe
wengine ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Makame Mbarawa, wabunge wa
kuteuliwa, Zakhia Meghji na Shamsi Vuai Nahodha; Mbunge wa Uzini,
Muhammed Seif Khatib, Makamu wa Mwenyekiti CCM, Phillip Mangula na
Katibu Mkuu wa CCM, Kinana.
Wengine
ni Naibu Katibu Mkuu CCM, Zanzibar Vuai Ali Vuai, Katibu wa Itikadi na
Uenezi, Nape, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, Emmanuel
Nchimbi, Meya wa Manispaa Ilala, Jerry Silaa na Hadija Abood.
Wajumbe
ambao hawakuwepo wakati wa ufunguzi wa kikao hicho ni Makamu wa Rais, Dk
Mohammed Ghalib Bilal na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama.
Walioshindwa
maoni Wakati huo huo, katika maeneo ya Makao Makuu ya CCM Dodoma,
makada mbalimbali wa chama hicho wamekuwa wakiingia na kutoka. Wengine ,
wakiwamo walioanguka kwenye kura za maoni, walionekana wakiwa
wamesimama kwenye viwanja vya ofisi hizo, wakibadilishana mawazo.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment