Pages

KAPIPI TV

Tuesday, August 4, 2015

"BAADA YA KURA ZA MAONI RAGE KUMFUATA LOWASSA CHADEMA"?



Na Mwandishi wetu,Tabora mjini.


SIKU CHACHE mara baada ya kufanyika uchaguzi wa kura za maoni za kuchagua Mgombea atakayeteuliwa  kuwania  Ubunge wa Jimbo la Tabora mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi,baadhi ya wananchi mjini Tabora wakiwemo wanachama wa CCM wamejikuta wakijiuliza maswali yasiyokuwa na majibu ya haraka kuhusu aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Bw.Aden Rage kuwa ataendelea kuwa mwanachama wa chama hicho au atakihama kutokana na matokeo ya kura za maoni ambapo alipata kura ambazo hakutarajia kuzipata.

Mtazamo huo wa wananchi  wa Jimbo  la  Tabora mjini na pengine wa baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi kuona viongozi wanaoona dalili ya kushindwa kwenye uchaguzi wa kura za maoni na kukimbilia kwenye vyama vya upinzani umekuja kufuatia hasa baadhi ya wabunge ambao walikuwa wakionesha kuwa ni maswahiba wa karibu wa Waziri mkuu mstaafu Bw.Edward Lowassa kumfuata kwenye chama alichohamia sasa Chadema.

Rage baada kupata kura 4133 akiwa  ameshika nafasi ya pili kinyume na matarajio yake  ambapo mshindi wa kwanza Emmanuel Mwakasaka  alipata kura 13,335,Wananchi wamekuwa wakijiuliza kuwa huenda kiongozi huyo akakihama Chama cha Mapinduzi kutokana na matokeo hayo ambayo yanadhihirisha kutokukubalika kwake na wengi kama alivyodhani na pengine kupewa moyo na wapambe wake wa karibu huku dalili za wazi zikidhihirisha kuwa kutokana na ukaribu wake na Bw.Lowassa huenda nae akafanya maamuzi magumu ya kumfuata Chadema.

Aidha mtazamo mwingine wananchi ambao umekuwa ukizidi kuwapa ukweli wa madai kwamba huenda Rage akahamia Chadema na pengine chama chochote cha siasa ni pale wanaposikiliza Redio anayoimiliki ikiendelea kuwaponda baadhi ya viongozi wa CCM na hata kufikia hatua ya kuwashawishi wananchi katika uchaguzi mkuu wa oktoba wachague viongozi wa Upinzani kwa madai kwamba CCM imepoteza dira.

Hata hivyo mtandao huu unaendelea kumtafuta Rage ili aweze kubainisha ukweli wa madai ya kuhamia Chadema kama ilivyozagaa katika maeneo mbalimbali Jimbo la Tabora mjini ikiwemo katika vikundi vya mitandao  ya kijamii  maarufu Whatsap.

Habari za ndani kutoka Chadema:-
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema jimbo la Tabora mjini kimekuwa kikiomba Mungu usiku na mchana CCM iweze kuliteua jina la Bw.Aden Rage ili awe mgombea Ubunge jimbo la Tabora mjini kwakuwa uteuzi huo utakuwa na neema kubwa kwa Chadema kupata kirahisi ushindi mkubwa wa Jimbo hilo.

Habari zaidi zinasema kuwa kutokana na madai kwamba Rage hakufanya lolote katika kipindi chote alichokuwa madarakani hivyo kwa upande wa Chadema itawarahisishia namna ya kumuelezea wakati wa mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Tabora mjini Bw.Simon Lameck akizungumza na Mtandao huu wa KAPIPIJhabari.COM alisema CCM kutokana na kuwakumbatia Wabunge wasiowajibika na kuwatumikia vyema wananchi kitakacho wapata safari hii wasitafute mchawi kwakuwa itakuwa imetokana na mfumo uliopo ndani ya chama hicho wa kushindwa kuwawajibisha Wabunge ambao hawawakilishi wananchi na kero walizonazo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zaidi ya kupongeza kila kitu hata kama kinawaumiza wapiga kura wao.

Habari za ndani kutoka CCM:-
Mmoja kati ya viongozi wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kumekuwa na taarifa hizo zimeenea katika maeneo mengi lakini hawana sababu ya kufuatilia kwani hakuna mtu anayelazimishwa kuwepo ndani ya CCM kwakuwa chama hicho ni chama makini na hakiwezi kushughulikia mtu mmoja anapotaka kuhama kwani hakuna maslahi ya kijamii kufanya hivyo.
 

   

No comments: