Pages

KAPIPI TV

Tuesday, July 28, 2015

WAGOMBEA UBUNGE NDANI YA CCM WAENDELEA KUJINADI KWENYE KATA,WANANCHI WACHAMBUA MBIVU NA MBICHI

Emmanuel Mwakasaka akijinadi mbele ya wakazi wa kata ya Kiloleni ambapo aliwataka wamchague ili aweze kushirikiana nao katika kuleta maendeleo,katika mazungumzo yake wakati wa kujinadi aliepuka ahadi za uongo katika kutekeleza majukumu yake ya Ubunge endapo atapata ridhaa ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini.Amesema kutokana na kutambua vema matatizo yanayowakabili wakazi wa Jimbo la Tabora mjini atahakikisha anayaunganisha makundi ya Wanawake,Vijana na Wazee na kutumia fursa zilizopo katika mfuko wa Jimbo kuwainua kiuchumi pamoja na kuwatafutia fursa nyinginezo zitakazokuwa chachu ya maendeleo kwa kushirikiana nao.Amesema atakuwa Mbunge wa kuwatumikia wananchi na kamwe hatowakimbia kama wanavyofanya Wabunge wengine ambao wanakabiliwa na Uchoyo wa kupindukia.  
Mkangala akijinadi kwa baadhi ya wakazi wa kata ya Kiloleni ambapo alihimiza umuhimu wa kuchagua viongozi wenye nia ya kuwatumikia wananchi huku akieleza kuguswa kwake na namna ambavyo viongozi waliopita walivyoshindwa kuleta maendeleo katika jimbo la Tabora mjini na hata kusababisha huduma za kijamii zikiwemo za Afya na nyinginezo kuwa kero kubwa kwa wananchi hususani akinamama wajawazito wanapokwenda kujifungua hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete ambapo hukosa huduma zinazostahili kwa wakati muafaka.

Kamaliza Kayaga mgombea aliyejinadi kwa kuwataka wanaCCM  wamchague ili aweze kuwania nafasi ya Ubunge Jimbo la Tabora mjini ambalo wananchi wake wamekuwa na migogoro ya ardhi isiyokwisha kwakuwa yeye kitaaluma ni Mwanasheria hivyo amesema atatumia uwezo wake na elimu aliyonayo kusaidia kuondosha adha hiyo ambayo ni kero kubwa kwa wananchi,atafanya hivyo endapo atachaguliwa kuwa Mbunge na kuahidi kuwa akiwa Bungeni  atatetea baadhi ya Sheria kandamizi ziondolewe ili kumpa fursa wananchi kuishi katika mazingira yenye kuzingatia haki na usawa.  
William Masubi akijinadi mbele ya wananchi wa kata ya Kiloleni ambapo alizungumzia suala la elimu bora kwa wanafunzi pamoja na changamoto nyingine zinazokwamisha maendeleo ya Jimbo la Tabora mjini,aliahidi kuwa karibu na wananchi na kusikiliza kero zao kwakuwa yeye ni mkazi wa Tabora na hata kama endapo atachaguliwa kuwa Mbunge kamwe hatokuwa kama walivyo wabunge waliotangulia ambao baada ya kuchaguliwa wanakimbilia kuishi jijini Dar-es-salaam huku wananchi wakiendelea kukosa mtu wa kupokea na kufanyia kazi changamoto zinazowakabili.


Aden Rage ambaye ni mbunge aliyemaliza muda wake wakati akijinadi amewataka wanaCCM wampe ridhaa ya kuwania nafasi ya Ubunge kwa mara nyingine tena huku akidai kuwa yeye tayari ni mzoefu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na kwamba  atawatumikia vyema kwa kuwaletea maendeleo,akipigia mfano wa Ujenzi wa barabara za lami,huduma za maji Tabora mjini,maboresho ya huduma za afya katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete ingawa jambo hilo wananchi waliowengi walionesha kutokubaliana nalo kwakuwa huduma za afya hospitali bado haziridhishi na waathirika wakubwa ni akinamama wajawazito ambao wanalazimika kulala wawili wawili hadi watatu katika kitanda kimoja.

Bandora Mirambo amesema endapo atapata ridhaa ya wanaCCM na kufanikiwa kushinda katika uchaguzi mkuu atashirikiana na wananchi katika masuala mbalimbali ya maendeleo kwakuwa ofisi yake kama mbunge itafungua milango ya dawati la kusikiliza kero za wananchi huku akiwaasa kuwapima wagombea wote kwakumuangalia ambaye ana hofu ya MwenyeziMungu kwani ndiye atakuwa mgombea bora atakayewatumikia wananchi.Amesema tatizo la linalokwamisha maendeleo ya Jimbo la Tabora mjini ni kukosa Mbunge anayeyatambua matatizo yanayowakabili wananchi kwani kila anayechaguliwa kushika nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Tabora mjini anasahau na kutowajali waliomuweka madarakani.



Amon Mkoga amejinadi kwa kuwataka wananchi wamchague kwani yeye ndiye mtu sahihi anayefaa kuwatumikia kwakuwa amekuwa akifanya mambo mengi ya Maendeleo hususani ya elimu kwa kuyahamasisha baadhi ya makampuni na mashirika kusaidia Shule za msingi na Sekondari,amesema endapo atapata ridhaa ya kuwania Ubunge na kufanikiwa atasaidia vikundi mbalimbali vya wajasiliamali kwa kuwapa elimu itakayowawezesha kuondokana na umasikini.

No comments: