MSANII maarufu wa filamu nchini,
Mohamed Mwikongi jina la sanaa ‘Frank’ amejiunga na chama kipya cha
siasa cha ACT Wazalendo. Frank amejiunga na chama hicho leo jijini Dar
es Salaam akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika hafla hiyo ya utambulisho
kiongozi mwingine ambaye ni Mwenyekiti wa kitengo cha vijana Taifa wa
NCCR Mageuzi, Deo Meck pia amejiunga na chama cha ACT Wazalendo na
kukabidhiwa kadi za chama hicho.
Akiwakabidhi kadi za
ACT-Wazalendo, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Msafiri Mtemelwa leo
Makao Makuu ya ACT alisema wamewapokea wanachama hao wapya kwa mikono
miwili na wapo tayari kushirikiana nao ndani ya chama hicho. Alisema
kuna idadi kubwa ya vigogo kutoka vyama vingine ambao tayari wameomba
kujiunga na chama chao na taratibu zinafanywa kutambulishwa.
“…tendo hili la leo la
kuwakaribisha vijana hawa ni mwanzo wa kuwatambulisha wanachama
mbalimbali wakiwemo wabunge na viongozi wa vyama waliojiunga nasi baada
ya kuvunjwa kwa Bunge. Tayari tunao baadhi ya watu waliokuwa wabunge na
wameshajiunga nasi na mchakato wa kuwatambulisha unaendelea katika
maeneo mbali mbali nchini,” alisema Mtemelwa.
Akizungumzia mchakato wa uchukuaji
fomu kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho,
Mtemelwa alisema Julai mosi mwaka huu Chama Cha ACT-Wazalendo kilifungua
rasmi pazia la uchukuaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali zikiweno za
Udiwani, Ubunge na Urais.
Alisema tangu kuanza kwa uchukuaji
huo wa fomu kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wanachama kuchukua fomu na
hadi sasa kuna baadhi ya majimbo na kata zina watia azma kuanzia wanne
mpaka tisa jambo ambalo alidai ni faraja kwa ACT Wazalendo.
“Kati ya majimbo 265 yakiwamo
majimbo mapya 26 yaliyoongezwa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi(NEC), ACT-Wazalendo tumeshakuwa na waweka azma zaidi ya mmoja
katika majimbo 226 kwa nchi nzima na tunaamini mpaka kufikia mwisho wa
uchukuaji fomu ndani ya Chama majimbo yote 265 yatakuwa yanawatia azma
mbalimbali wanaosubiri kupitishwa na chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu,”
aliongeza Naibu Katibu Mkuu huyo wa ACT Wazalendo.
Alibainisha kuwa kichama mwisho wa
kuchukua na kurudisha fomu kwa nafasi ya udiwani ni julai 24, kwa
nafasi ya Ubunge mwisho ni Julai 31 na kwa nafasi ya Urais mwisho wa
kuchukua na kurudisha fomu ni Agosti Mosi, 2015.
“Kwa ngazi ya Taifa
Halmashauri kuu itakutana Agosti 13 kwa ajili ya kuteua jina la mgombea
Urais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na kupendekeza majina
ya wagombea Urais kwenye mkutano mkuu. Agosti 13, Mkutano mkuu
utamchagua mtu atakayepeperusha bendera ya Chama cha ACT Wazalendo
katika mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
“Hivi karibuni tumepokea taarifa
kutoka katika miji ya Tarime na Rorya Mkoani Mara kuwa kuna watu
wanapita na kutangaza kuwa Chama chetu kimezuiwa kushiriki Uchaguzi kwa
muda wa miezi sita.
Tumebaini lengo la upotoshaji huu ni kuwakatisha watanzania
tamaa juu ya ukuaji wa Chama Cha ACT-Wazalendo pamoja na dhamira yake
nzuri ya kuirudisha nchi katika misingi iliyoachwa na hayati Mwalimu
Julius Nyerere.
“Tunawataarifu wananchi kuwa Chama
chetu kitashiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu kwa kuweka
wagombea wa nafasi zote na Chama hakitakuwa tayari kuona sehemu yoyote
ya nchi mgombea wa CCM anapita bila kupingwa,” alisisitiza Naibu Katibu
Mkuu huyo wa ACT Wazalendo.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment