Pages

KAPIPI TV

Friday, June 19, 2015

UDHIBITI WA KUCHEPUSHA DAWA ZA SERIKALI WAANZA KUTEKELEZWA


 Ofisa Uhusiano Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bi Etty Kusiluka (kushoto), akizungumza na mwananchi Juma Nyingi aliyetembelea banda la MSD katika maonyesho hayo.
 Ofisa Uhusiano wa MSD, Benjamin Massangya (kulia), akimueleza mkazi wa Utete kutoka wilaya ya Rufiji, Omary Abdallah shughuli mbalimbali zinazofanywa na MSD baada ya kutembelea banda la MSD leo mchana.
 Vitanda vya hospitali vilivyopo katika banda la MSD.



Na Dotto Mwaibale

IDADI ya vidonge vinavyosambazwa na Bohari ya Dawa (MSD) ambavyo vimewekewa nembo ya Serikali (GOT)  imefikia 42 hadi sasa huku wazabuni wanaoshinda tenda kwaajili ya dawa na vifaa tiba vya MSD wakiendelea kuelekezwa kukidhi utaratibu huo wa kuweka nembo ya GOT ili kuepusha uchepushaji wa dawa za serikali.

Bohari ya Dawa ilianza utekelezaji huo wa uwekaji wa nembo ya GOT kwenye vidonge katika mwaka wa fedha uliopita, ambapo awali walikuwa wakiweka nembo ya MSD kwenye vifungashio tu, na kusababisha dawa hizo kuishia kuchepushwa.

Akizungumza wakati wa maonyesho ya Utumishi wa Umma, yanayofanyika jijini Dar es Salaam Ofisa Uhusiano Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bi. Etty Kusiluka ameeleza kuwa  zaidi  ya vifaa tiba na dawa 650 za serikali  ambazo zinasambazwa na Bohari ya Dawa zinapaswa zote kuwa na nembo ya 
MSD na GOT, na zoezi hili litakamilika kadri wazabuni wanavyoendelea kupokea maelekezo.

Baadhi ya dawa ambazo tayari zina nembo hiyo ni pamoja na Mgnesium, Amoxicillin, Pracetamol, Diclofenac, Ciprofloxacin na Cotrimoxazole.

Katika hatua nyingine, Bi Kusiluka ameeleza kuwa Bohari ya Dawa (MSD) inaendelea na mipango ya kusogeza huduma karibu zaidi na mwananchi kwa kuanzisha huduma ya uuzaji wa dawa katika maeneo ya hospitali na karibu na maeneo yenye uhitaji wa dawa, ambapo mauzo hayo yatafanyika kwa saa 24. Huduma hizi zitaanza katika miji mikubwa nchini ambayo ni pamoja na Mbeya, Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha. Mkoa wa Mbeya ndio utakuwa wa  kwanza kutoa huduma hizi, ambapo hadi sasa maandalizi yako katika  hatua za mwisho.


Maduka haya yataiongezea Bohari ya Dawa wigo wa utendaji wa utoaji huduma kwa wananchi, ambapo hadi sasa huduma ya usambazaji wa dawa na Vifaa tiba na vitendanishi vya maabara inatolewa kupitia mali inayohifadhiwa kwenye maghala ya MSD ya kanda zake nane zilizopo mikoa ya Mwanza, Tabora, Mtwara, Mbeya, Iringa, Dar Es Salaam, Dodoma na Moshi pamoja na vituo vyake viwili vya mauzo vya Muleba na Tanga. 

No comments: